Naam! Alhamisi ya Novemba 5, 2015, Watanzania tuliwashangaza, tuliwaelimisha na tuliwathibitishia Walimwengu kuwa madaraka ya kisiasa yanawezekana kuachwa kwa kupokezana kwa hiyari, upendo na amani bila ya kutumia ubabe, ung’ang’anizi wala mtutu kumwaga damu ya Wananchi.

Uthibitisho huo ulionekana mbele ya mataifa mbalimbali kutoka barani Afrika, Arabia, Asia, Amerika na Ulaya yalipohudhuria sherehe ya kukabidhiana madaraka wakati Rais wa awamu ya nne wa Serikali ya Tanzania Dk. Jakaya Kikwete alipomkabidhi madaraka ya urais Dk. John Pombe Magufuli kuongoza awamu ya tano ya serikali hiyo.

Utamaduni huo ulianza tangu enzi ya uongozi ya chama kimoja cha siasa; TANU kwa Tanganyika na ASP kwa Zanzibar (1961-1995) na kujikita ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa katika chaguzi za mwaka 1995.

Ni utaratibu uliobuniwa na kudumishwa na Watanzania wenyewe tangu enzi ya awamu ya kwanza ya Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenda awamu ya pili kwa Rais Alhaj Ali Hassani Mwinyi, mwaka 1985.

Naye, Rais Mwinyi alikabidhi madaraka hayo kwa Rais Benjamin Mkapa mnamo mwaka 1995. Kwa desturi hiyo hiyo Mkapa naye alimkabidhi madaraja ya urais Dk. Kikwete mwaka 2005.

Utamaduni huu una asili na sababu kadhaa zikiwamo kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu; imani ya upendo na utii mbele ya Mwenyezi Mungu; kutambua na kufuata kanuni za demokrasia kwa kutumia sanduku la kura na kuamini kwamba cheo au madaraka  ni dhamana anayopewa mtu yeyote kuwa kiongozi kutoka kwa jamii ya watanzania.

Naamini, Watanzania tuliwashangaza baadhi ya viongozi  na marais kutoka mataifa mbalimbali waliposhuhudia  na kuona viongozi wetu wakiachiana na kukabidhiana madaraka ya juu ya Nchi  kwa vicheko, furaha na amani mbele ya kadamnasi ya watu pale Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Ni ukweli usio na mashaka baadhi ya marais waliohudhuria sherehe ile huko makwao hawataki kuachia madaraka ya kuongoza nchi kwa hiyari na upendo. Wanataka kuendelea kuongoza kana kwaba wao tu ndiyo wenye uwezo, hisa na stahiki ya kuongoza na wengine hawana haki hiyo.

Ninaposikia nchi jirani au ya mbali inapoingia katika mapigano ya kugombea na kung’ang’ania madaraka hupatwa na huzuni na masikitiko kwa nini nafsi ya viongozi kupenda kuangamiza  wananchi bila ya sababu. Kuwatia ndani wanasiasa na kuelekezewa mitutu na kuuawa pale Wananchi wanaposema kiongozi fulani muda na uwezo wake umeisha.

Nchi hizo amani yaoni ni nusu ya mashaka. Sisi watanzania hatuna budi kuendelea kutunza amani yetu ambayo ni lulu ya thamani. Pindi tutapoichezea na ikituponyoka mikononi, ukweli kuirejesha kwake itakuwa ni gharama bini muhali.

Ninachoweza kusema kwa Watanzania wenzangu tuzidi kuendeleza utamaduni huu wa kuachiana madaraka kwa upendo na amani. Tunapofanya hivyo tunajenga na kuimarisha umoja wetu na utulivu wa nchi ambao unatupatia fursa ya kupanga  mipango bora ya maendeleo na kubaini hitilafu; na kuzirekebisha.

Tangu awamu ya kwanza hadi ya nne ya uongozi wa nchi yetu, tumeweza kufanya mambo mengi ya maendeleo katika uchumi, siasa na kijamii. Hili halina ubishi hata kama baadhi ya ndugu zetu eti wanaimba hakuna kilichofanyika, (1961-2015). Ni ubwege, ujinga na uzandiki. Nafsi zao zinawasuta kwa upuuzi wao.

Leo tusingekuwa na maendeleo katika afya zetu, elimu yetu wala katika uchumi wetu. Kamwe tusingesema na kuimba tunataka mabadiliko. Kutaka mabadiliko ni matokeo ya kujitambua tuna kiasi gani cha maendeleo na mafanikio na hivyo tunataka hicho kilichobaki. Tunahitaji sampuli nyingine ya maendeleo na hayo ndiyo mabadiliko yenyewe. mabadiliko ya kupambana zaidi na maadui wetu ujinga umaskini na maradhi.

Tunapohitaji kuondoa ujinga sio kama watanzania wa leo hawana elimi. Hapana. Elimu tunayo hadi ya chuo kikuu lakini bado haijatufikisha ndani ya kiini cha maendeleo ya sayansi na teknolojia.Hatuna maabala ya utafiti uliyopea na kuaminika duniani.

Elimu yetuni pana kiasi gani katika kinga na tiba ya maradhi mbalimbali yanayosumbua wananchi  kama vile macho saratani ya damu matiti koo mkojo n.k. Matabibu na mabingwa wa magonjwa hatari wapo kiaasi gani kukidhi matibabu. 

Elimu yetu imetupatia utaalamu wa kiwango gani katika viwanda vikubwa, vya kati hadi vidogo vya kufua chuma, kutengeneza mitambo na mashine, utafiti wa zana bora za ulinzi, kilimo, uvuvi  hata ufugaji. Kwa kiasi gani tumechepea katika vyombo vya usafiri, mawasiliano n.k. Hapa nazungumzia utengenezaji wa vifaa na zana mbalimbali. Sio ukarafati wala uunganishaji mashine na mitambo.

Elimu tuliyonayo ndani ya miaka 54 ya Uhuru imetufikisha wapi katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara kwa kujikita katika mashamba makubwa na kutumia masine na mitambo ya kisasa ya kilimo. 

Ndani ya mchakato wa kukabidhiana madaraka ya viongozi tangu ngazi ya udiwani ubunge na urais tumeweza kuwa na mabadiliko mengi katika sekta za kilimo uvuvi na ufugaji; ufundi na uhandisi; dawa na tiba; usafiri na mawasiliano bila kusahau siasa na michezo.

Narudia kusema kiwango tulichofikia katika maendeleo hayo bado hakijaturidhisha. Ndiyo maana sasa tunahitaji mno mabadiliko ya kweli; ya kujenga Tanzania ya kisayansi na kiteknolojia.

1105 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!