Utata wa Jaji Aloysius Mujulizi

Wiki iliyopita Ikulu jijini Dar es Salaam ilitoa taarifa ya kile kilichoelezwa kuwa ni kuridhia kwa Rais John Magufuli, kujizulu kwa viongozi watatu.
Viongozi hao ni Jaji wa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Aloysius Mujulizi; Jaji wa Mahakama Kuu, Upendo Msuya; na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Sadiki.
Ikulu haikutoa sababu za watatu hao kuomba kujiuzulu. Hata hivyo, mambo kadhaa yametajwa kuwa yamesababisha kujiuzulu kwao. Sadiki yeye amesema ameamua kuondoka ili kupisha ‘damu mpya’; hasa akirejea hali yake ya afya kuwa haimpi fursa ya kutekeleza dhima zake kwa kadri ya kasi ya Rais Magufuli.
Jaji Msuya, naye anatajwa kuwa siha yake si njema. Pamoja na suala la siha yake, kwa muda sasa Jaji Msuya amekuwa akihusishwa na kuyumba au pengine kutupwa kwa kesi zinazowahusu watuhumiwa wa dawa za kulenya.
Mara kadhaa uamuzi wake kwenye kesi hizo uliwezesha, ama watuhumiwa kukimbia nchi wakiwa bado wakiwa na kesi, au kesi zao kufutwa katika namna inayozua maswali mengi kisheria.
Kwa upande wa Jaji Mujulizi, kuna habari za ndani zinazothibitisha kuwa vyombo vya dola vinachunguza uraia wake. Bado haijajulikana kama kweli ameomba mwenye, au ametakiwa ajiuzulu.
Mbali ya suala hilo, amekuwa akihusishwa na kupokea fedha katika matukio mawili makubwa ya ufisadi yaliyowahi kulitikiza Taifa.
Julai 13, 2012 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliwasilisha maoni yake kuhusu Mpango na Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013.
Pamoja na mambo mengine, maoni hayo ya Kambi Rasmi ya Upinzani yaliyowasilishwa na Msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, yalikosoa utaratibu wa uteuzi wa majaji wa Mahakama ya Tanzania.
Lissu alieleza kwa kirefu uteuzi huo, na kwenye aya kadhaa, alimgusa pia Jaji Mujulizi.
Alisema: “Jaji Aloysius Mujulizi alikuwa miongoni mwa watu ishirini walioteuliwa Majaji wa Mahakama Kuu mwezi Februari, 2006. Kabla ya uteuzi wake, Jaji Mujulizi alikuwa wakili wa kujitegemea katika kampuni ya mawakili ya Ishengoma, Masha, Magai & Mujulizi Advocates (IMMMA) ya Dar es Salaam. Kampuni hii ya mawakili ndiyo iliyoshiriki katika kuanzishwa kwa kampuni iitwayo Deep Green Finance Co. Ltd. mnamo tarehe 18 Machi 2004. IMMMA Advocates vile vile walikuwa mawakili wa TANGOLD LTD.
“Makampuni haya mawili yanatuhumiwa kutumika kupitishia mabilioni ya fedha zilizoibiwa Benki Kuu ya Tanzania kati ya mwaka 2005 na 2006. Kwa mfano, katika kipindi kifupi cha miezi minne kati ya Agosti 1 na Desemba 10, 2005 kampuni ya Deep Green Finance ilipokea jumla ya shilingi 10,484,005,815.39 kutoka akaunti ya kulipia madeni ya nje (EPA) iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania.
“Katika kipindi hicho hicho, kampuni ya TANGOLD LTD. ililipwa dola za Marekani 13,736,628.73 kutoka kwenye akaunti hiyo ya EPA. Nyaraka zilizowasilishwa BRELA na mawakili wa IMMMA Advocates na kusainiwa na Gavana wa Benki Kuu wa wakati huo Daudi Ballali tarehe 20 Mei 2005 zinaonyesha kwamba TANGOLD LTD ilikuwa kampuni ya kigeni kutoka Jamhuri ya Mauritius. Haya yote yalitokea wakati Jaji Mujulizi akiwa wakili mwenza wa IMMMA Advocates.”
 
Majibu ya Jaji Mujulizi
Baada ya maelezo hayo ya Lissu, Jaji Mujulizi, kupitia kundi la Wanabidii, alimjibu Lissu. JAMHURI limefanikiwa kupata majibu hayo na kuonelea vema kuyachapisha neno kwa neno bila kuyahariri ili kutopoteza maana. Hapa chini ni majibu hayo kama yalivyoandikwa na Jaji Mujulizi mwenyewe mwaka 2012. Makosa ya kisarufi na ki-muundo yanaoonekana kwenye majibu hayo ni ya mwandishi mwenyewe.  
ALISEMA: Sina shaka kwamba pengine Mh. Lissu ana nia njema yakutaka kuuweka Muhimili wa Mahakama sawa! Lakini nina wasiwasi na usahihi wa njia aliyoichagua kuitumia!  Zipo njia mbadala za kushugulikia suala ili bila kujenga mazingira ya kashifa kwanza kwa wote wanohusika na huku yeye akiwa ni Wakili msomi, ambae anapasua kufahamu zaidi, na kama anavyopenda yeye kujisifu kwamba ni mweredi!
Ujaji ni taasisi na ni ofisi inayoanzishwa kikatiba na sababu za msingi kuiwekea masharti, miiko na taratibu mahsusi za uteuzi ni ili kuifanya taasisi hiyo iaminike mbele ya macho ya jamii. Inatokea mara nyingi tu kwamba mtu aliyeteuliwa kwa ushika mamlaka hayo makubwa, kinyume na ilivyotegemewa hana uwezo kwa muudu vyema kazi za ofisi hiyo! lakini kwa kuzingatia unyeti wa ofisi hiyo, na ili kuilinda ofisi hiyo isijeikatumiwa vibaya, hupo utaratibu mzuri wa kumfanyia uchunguzi mhusika na inapothibiti anaondolewa. Imewahi kutokea katika historia fupi ya mahakama kuu yetu kushikwa na wazawa. Wapo majaji waliojiuzulu mara tu baada ya tume kuundwa kuwachunguza, lakini wengine walivuliwa madaraka.
Kama anavyotowa mfano Mh. Lissu wa Mzee Aluthe kule Singida, mtu yoyote anweza kumlalamikia Jaji kupitia taratibu mahsusi na akachukuliwa hatua! Lakini, Mh. Lissu kama Wakili, ni mwanakyama wa Tanganyika Law Society, asasi ya kisheria amabayo inatakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba hawateiuliwi watu wasio faa katika nafasi nyeti ya ujaji! Siyo hivyo tu lakini kuhakikisha hata baada ya kuteuliwa Jaji anaendesha ofisi hiyo kwa mujibu wa sheria. Ndani ya Tume ya Ajira ya Mahakama yupo mwakilishi wa asasi hiyo. mawakili wanaelewa taratibu zinazotakiwa kufuatwa katika kutimiza wajibu wao huo hadhimu ambao wamekabidhiwa kwa mujibu wa sheria. Pengine wale wabunge waliomshangaa Mh. Lissu walikuwa na maana hiyo!
Ustaraabu wa kawaida unatuelekeza kwamaba kila jambo lina mahali na wakati wake! Kuna msingi mkuu wa haki ndani ya katiba na convetion za kimataifa nayo ni kutokumuhukumu mtu yeyote pasipo kwanza kumpa nafasi na fursa ya kujitetea kwa mujibu wa sheria! Kanuni za bunge pia zinazingatia haki hiyo!
Mimi sijui ni namna gani Tume ya Ajira ya Mahakama inavyowapata, kuwatathimini na hatimae kuwapendekeza watu wenye sifa kuteuliwa kuwa Jaji au Jaji Kiongozi. Bahati mbaya katika maelezo ya Mh. Lissu,ambayo yamenakiliwa hapo chini hajaonesha mihtasari ya vikao vya Tume vikionesha majina waliyoyapendekeza na kupelekwa kwa Mh. Rais ili kuthibitisha ni nani aliongezwa au aliyeachwa! Mimi sijui kama nilipendekezwa au la kwa kuwa sikuwahi kuitwa kwenye kiako chochote cha Tume au mjumbe wa Tume.
Hivyo siwezi kusema lolote juu ya hilo. lakini ingeundwa TUME ya uchunguzi pengine ingeweza kubaini hivyo. Ninalo weza kusema ni kwamba sikuwahi kujipendekeza wala kuombwa na mtu yeyote kuteuliwa kuwa Jaji. Lakini nilikubali kutumika baada ya kuteuliwa kama afisa wa mahakama na mzalendo mwenye wajibu wakutumikia taifa lake kwa nafasi anyopewa kwa mjibu wa sheria.
Wewe kama msaidizi wangu katika shuguli zangu binafsi, unafahamu khasara ambayo nimeipata tangia kukubali nafasi hiyo. Nilijitoa kwenye ushirika wa IMMMA, nililazimika kuuza mali zangu ili wanangu waendelee kusoma. Kampuni yangu ya Inurance Bokerage iliyumba na hatimae kufungiwa mara tu baada ya mimi kujitoa kwenye uendeshaji wake wa moja kwa moja! Nimepoteza mamillioni ya shillingi katika biashara mbalimbali kutokana kukosekana usimamizi!
Kwetu,, mimi na familia tumelipa gharama kubwa ili mradi tu niweze kuuimikia taifa! Nilikaa miezi minane bila kulipwa mshahara kiduchu wa Jaji wakati huo! Kiduchu kuringanisha na mapato yangu wakati nikijitegemea!

DEEPGREEN
Mhe. Lissu pamoja na wenzake wanalifanya jambo ili liwe kubwa kwa upande wangu na uteuzi wangu pasipo kuliweka bayana. Sina taarifa yoyote rasmi ya ni lini suala hili lilikuja kuthibitika kuwa kashfa. Nasema hivyo kwa sababu, suala la usajiri wa makampuni ni suala dogo sana kiutratibu kwani harihitaji mtu awe wakili kwanza ndipo aweze kutengenez MEMATS. Ni kazi ya uhaziri au ukalani tu! Raia wengi wanasajiri makampuni yao yenyewe. Vivyo suala la kisajiri kampuni ndani ya Kampuni ya uwakili yenye wabia na watumishi wengi siyo suala nyeti amabalo linatakiwa kuidhinishwa na wabia wote, kama ilivyo matharani kwenye kukubali kufungua kesi mahakamani, ambapo pana uwezekano mkubwa wa kutokea mgingano wa masirahi!
Mimi IMMMA nillkuwa kwa miaka yote 9 idara ya Litigation, yaani mambo ya Mahakama. Hapakuwepo  na sababu mahususi ya mimi kulazimika kufahamu mambo ya usajiri wa makampuni.
Lakini, kashifa ya ni ya kusajiri kampuni kinyume cha sheria, au kwa njia za udanganyifu! Kama ndivyo ni lini Mh. Lissu alipereka malalamiko rasmi dhidi yangu au yoyote kati ya mapartner wangu mbele ya Kamati ya nidhamu ya asasi ya TLS na ikathibiti kwamba tulikiuka miiko na utaratibu wa kimaadiri na tukapata kuadhibiwa? Au kashifa ni ya kampuni hiyo kutokana na kile inachodaiwa kukifanya baada ya kuwa na uhai? kama ndivyo mimi au wenzangu walihusika vipi na uendeshaji wa kampuni hiyo kinyume cha utaratibu hadi tusitayiri kuchkuliwa hatua ama za kinidhaam katika ngazi ya taaluma au za kisheria ikithibit kwamba palikuwa na jinai?
Lakini ni lini niliteuliwa na ni lini TUME au Mh. Rais aliwahi kupelekewa taarifa za uhusika wangu unaokiuka maadili, ili kuwataadharisha ya kwamba sikuwa na sifa, kwa kukosa maadili au kwa kutuhumiwa kukosa maadili na wao wa kapuuza wakaniteuwa tu?
 Sina uhakika ni lini, suala hilo liliibuliwa lakini mimi wakati huo nilikuwa nimeisha teuliwa! Kwa maana ya tarehe 28 November 2006. Sasa hapo TUME au Mh. Rais wangejuaje juu ya tuhuma hizo hata kabla hazijaibuliwa?
Katika kesi ya kupinga Uteuzi wa Matokeo ya Uchaguzi ya Ubunge Arusha Mjini, Mbunge amabae ushindi wake ulikuwa ukipingwa alinitaka nijitoe kwa sababu eti CHADEMA waliwahi kuituhumu iliyokuwa kampuni yangu IMMMA kwa kuhusika na sula la DEEPGREEN. Niliwataka pamoja na kujitoa wawasilishe ushahidi wao juu ya tuhuma hizo mahakamani na wanipe nakala nami nipate kuupitia niweze kubaini kosa langu, na wao pia wamuombe Mh. Rais aniundie TUME ya uchunguzi ili ikidhibiti nivuliwe huo Ujaji kwa mujibu wa sheria, vinginevyo waache kunikashifu na kunivunjia heshima machoni mwa umma! Suala hilo lipo Mahakamani, hwakuwahi kuniletea ushahidi hadi wa leo!
Sasa kama siyo visa vya kisiasa tu, kwa nini tena Mh. Lissu aniunganishe kwenye orodha ya majaji anaodai waliteuliwa bila kupendekezwa na TUME? Mbona hili halina uhusiano wowote na alichotakiwa kuthibitisha?
Ni dhahiri kwamba, Mh. Lissu, akiwa ni msomi mweledi, anafahamu kwamba mtu aliyesaidia kama wakala tu kusajili kosa, awezi kuwajibika kwa makosa ya jinai itakayoyafanya kampuni hiyo baada ya kuzaliwa kwake, kama ilivyo kwa ,mkunga, hawajibiki kijinai kwa makosa ya watoto aliosaidia kuja duniani wakati mama zao wanjifungua! Lakini pia hata wazazi hawusiki moja kwa moja na jinai za watoto wao kwa sababu tu ya kuwazaa! Kwa hiyo katika hili Mh. Lissu, na wenzake hadi hapo watakapothibitisha kosa langu kupitia njia muafuaka, wataubeba mzigo mziti ya kunizulia na kisha kusambaza kashifa dhidi yangu pasipo na haki! Mungu ninaye mwaabudu ni MUNGU wa HAKI. Insh›Allah. Atanijibia duniani na Akhera!
Kama Jaji sina namna nyingine ya haki nje ya TUME huru, yakuweza kujitetea maana haki duniani utolewa na Mahakama na Mahkama ndiyo mtuhumiwa, siwezi kupata haki mbele ya Mahakama na watu wakaamini, haki imetendeka!

3844 Total Views 5 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons