Ni kweli, matumizi ya vidonge vya kupangilia uzazi yana madhara? Swali hili nimeulizwa mara nyingi sana na wasomaji wa JAMHURI.

Hivyo, leo kupitia makala hii utapata fursa ya kujua kama njia hii ya vidonge vya kupangilia uzazi ina madhara  au la. Na kama yapo basi ni yapi.

Matumizi ya njia mbalimbali za uzazi wa mpango hasa ya vidonge, ni moja ya njia salama na nafuu zaidi, lakini usalama huu utaimarika zaidi iwapo itatumika chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya.

Hata hivyo, ni dhahiri kuwa wakati wa matumizi ya njia za uzazi wa mpango, mwanamke atapitia matatizo madogo ya kiafya yanayoweza kumfanya kushindwa kuendelea na shughuli zake za kila siku.

Kwa hiyo, naona ieleweke ni kweli kuwa matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango yanaweza kusababisha matatizo madogo madogo ya kiafya japo si kwa wote, lakini kwa walio wengi huyapata na kwa msaada wa watoa huduma za afya, matatizo haya hutatuliwa.

Kwanza kabisa mwanamke anaweza akawa anapata kichefuchefu mara kwa mara na kuhisi kama ana homa baada ya kuanza kutumia vidonge hivyo.

Lakini dalili hizi hupungua taratibu baada ya muda fulani. Kwa kipindi hiki mwanamke anashauriwa kunywa vidonge hivyo wakati wa usiku ambapo anakaribia kulala ili kupunguza kichefuchefu na uchofu.

Aidha, iwapo dalili hizi zitadumu kwa muda mrefu, basi ni vyema kupata ushauri wa daktari.

Mabadiliko yanayojitokeza kwenye matiti pia ni madhara mengine madogo yanayotokana na matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango.

Katika kipindi hiki, mwanamke anaweza kuyaona mabadiliko yakijitokeza kwenye matiti, kama vile kuonekana kama yamevimba na kuongezeka ukubwa na kupata maumivu.

Mabadiliko haya hujitokeza wiki chache baada ya kuanza kutumia vidonge hivyo. Wengi wameniambia kuwa wanahofia dalili hizi huenda zikawa za saratani ya matiti.

Naomba niwatoe hofu kuwa, maadiliko haya kwenye matiti  yanasababishwa tu na mabadiliko yaliyojitokeza kwenye mfumo wa homoni, baada ya kuanza kutumia vidonge hivyo, na wala hayahusiani kabisa na saratani ya matiti.

Lakini pia ni vyema kumuona daktari haraka iwapo mabadiliko haya kwenye matiti yatadumu kwa wiki kadhaa.

Madhara mengine yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango ni uke kutokwa na ute usio wa kawaida ukeni.

Baadhi ya wanawake wanapatwa na hali hii wakati wa matumizi ya vidonge hivyo, hii ni kutokana pia na mabadiliko ya mfumo wa homoni.

Hivyo, matumizi ya vidonge hivyo husababisha mfumo wa homoni kuyumba, na kusababisha mabadiliko fulani kwenye mfumo wa uzazi ikiwamo ya kutokwa na ute usio wa kawaida ukeni.

Lakini pia inaweza kumsababishia mwanamke kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa, kutokana na maumivu anayokutana nayo baada ya mabadiliko madogo yaliyojitokeza ukeni.

Pia, matatizo mengine yanayotokana na matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango ambayo wanawake wengi huwapata ni kama vile kuongezeka uzito wa mwili kwa kasi.

Kutokana na vidonge kuchochea  homoni za kike, mabadiliko ya kihisia, kukosa hedhi kwa baadhi ya miezi, na hata maumivu ya kichwa ya mara kwa mara ambayo baada ya muda hutoweka.

Baadhi ya matatizo haya huwa ni ya muda mfupi, lakini kuna baadhi matatizo huwa ni ya kudumu ikiwamo lile la kuongezeka uzito kupita kiasi.

Hivyo, ili kujiepusha na matatizo ya kudumu yanayotokana na matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango, ni vyema kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kuanza kutumia njia za uzazi wa mpango.

3028 Total Views 14 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!