Matajiri wakubwa nchini wanaojihusisha na biashara ya mafuta ya petroli, mafuta mazito ya viwandani na kampuni kubwa za kimataifa, ni miongoni mwa wanaochochea mgogoro wa kupinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam , JAMHURI imethibitishiwa.

Kwenye mgogoro huo, zimo kampuni zinazoingiza nchini gesi ya matumizi ya nyumbani (LPG), pamoja na mataifa makubwa ya Magharibi ambao kwa desturi yamekuwa yakijitahidi kuhakikisha mataifa machanga, ikiwamo Tanzania , yanaendelea kuyanyenyekea kwa misaada.


Pamoja na ukweli huo kujulikana, tatizo jingine kubwa limebainika kuwapo kwa viongozi wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao, ama kwa woga au kwa kutotaka kuwachukiza “wakubwa”, wameshindwa kuwapasulia jipu wahusika wakuu kwenye mgogoro huu.

 

Badala yake, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Rais Jakaya Kikwete wametajwa kwamba wamekuwa na kauli za kuwalenga wanasiasa wa hapa nchini na viongozi wa kidini kama wachochezi wakuu.

 

Miongoni mwa wanasiasa walio mstari wa mbele kupinga ujenzi wa bomba la gesi kwa kudai anawatetea wananchi wa Mtwara, ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).

 

Habari zilizopatikana mwishoni mwa wiki zinasema Serikali inajiandaa kukabiliana na “wakubwa” wanaopinga mradi huo, kwa kuwaandikia barua na wengine kuwaita. Miongoni mwao kuna mabalozi (majina tunayo) ambao wamebainika kuwa nyuma ya mgogoro huo.

 

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini pasi na shaka kwamba lipo kundi la wanasiasa linalotumiwa na wafanyabiashara ya mafuta ya petroli na mafuta mazito, ambao wanaamini kuwa mwisho wa biashara yao utatokana na ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara.

 

Hofu hiyo imewafanya wafanyabiashara hao wahahe huku na kule, lengo likiwa kukwamisha mpango huo ambao kiuchumi unatajwa kama mwarobaini maridhawa.

 

Habari za uhakika kutoka serikalini zinasema kwamba Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) pamoja na Benki ya Dunia ni miongoni mwa wachochezi wakuu kwenye mgogoro huu. Pamoja nao, ni mataifa ya Magharibi ambayo ndiyo yanayoshikilia na kuongoza taasisi hizo za fedha.

 

“Wanahoji iweje mradi huu ujengwe na Tanzania kwa fedha za mkopo kutoka China . Si hivyo tu, wanahoji kwanini usimamizi ufanywe na shirika la umma (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ). Walitaka kazi hiyo iangukie kwenye mikataba ya kudumu ya kampuni zao kama walivyofanya kwenye Songas na Pan African,” kimesema chanzo chetu.

 

Chanzo hicho kimesema hofu nyingine iliyo wazi ni kasi ya ushirikiano wa China na mataifa ya Afrika, hasa Tanzania ; huku mataifa ya Magharibi yakionekana kutopewa kipaumbele katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Wafanyabiashara ya mafuta wahaha

Kundi la wafanyabiashara ya mafuta ya petroli na mafuta mazito ya viwandani, ndilo linaloonekana kuwa kwenye wakati mgumu. Hawa wanashirikiana na kampuni za mafuta za kimataifa ambazo aghalabu huingiza mafuta na kuyauza nchini kupitia ukwepaji kodi.

 

Kwa upande wa matumizi ya mafuta kwa magari, baada ya ujio wa gesi jijini Dar es Salaam, magari mengi yatatumia nishati hiyo badala ya petroli na dizeli.

 

“Kwa sasa Serikali inatumia dola za Marekani zaidi ya milioni 200 kuagiza mafuta ya magari kila mwaka. Hizi ni fedha nyingi sana.


Ukisambaza mtandao wa gesi hadi katika magari utaokoa kiasi hiki cha fedha. Ni wazi wafanyabiashara wataathirika, kwa hiyo uamuzi huu wa ujenzi wa bomba la gesi kwenda katika jiji kubwa lenye viwanda na magari mengi kama Dar es Salaam hawautaki,” kimesema chanzo chetu.

 

Wafanyabiashara hao wanatambua kuwa matumizi ya gesi viwandani yatashusha mapato yao kwa sababu gharama ya matumizi ya gesi ni madogo mno kuliko mafuta.


Mfano halisi ni Kiwanda cha Saruji cha Twiga ambacho baada ya kuanza kutumia gesi, sasa gharama zake za umeme ni Sh bilioni 1.5; ilhali awali wakati wakitumia umeme walikuwa wanalipa Sh bilioni 8 kwa mwezi. Hadi sasa kuna viwanda 37 vinavyotumia gesi Dar es Salaam. Kwa sasa Tanzania inatumia nusu ya mapato yake ya fedha za kigeni kugharimia ununuzi wa mafuta.


Wengine wanaohaha kuhakikisha gesi haifiki Dar es Salaam , ni wafanyabiashara wa gesi ya LPG. Gharama ya mtungi mmoja wa kilogramu 15 inauzwa Sh 54,000 jijini Dar es Salaam.


Mapato ya wenye gesi pamoja na wafanyabiashara wa bidhaa hiyo yanatarajiwa kushuka hadi robo ya kiasi hicho, yaani mtungi huo huo utauzwa Sh 13,500 kwa ujazo huo endapo gesi itafika Dar es Salaam .


“Wanajua watakosa mapato makubwa, wananchi watapata nafuu kubwa sana . Ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa utapungua sana …Haya mambo wanayajua ndiyo maana hawataki kabisa,” kimesema chanzo kingine kutoka Wizara ya Nishati na Madini.


By Jamhuri