Juzi nilishiriki mjadala mfupi katika mtandao wa kijamii wa Facebook. Niliweka picha ya wachuuzi waliovamia eneo la waenda kwa miguu katika eneo la Ubungo, Dar es Salaam.

Maudhui ya picha hiyo yalikuwa kuwafikishia taarifa (kana kwamba hawazioni wala hawazijui) viongozi wetu juu ya hatari ya kuwapo vilio na uvunjifu wa amani katika eneo hilo.

Polepole, wachuuzi wengi wameanza kuhodhi eneo la waenda kwa miguu kando ya barabara hiyo ambayo ufunguzi wake bado unasubiriwa kwa hamu.

Wachuuzi hawa wamejitwalia eneo hilo ilhali mamlaka zinazohusika zikiwa kimya. Kwa kuwa mamlaka husika zimekaa kimya, hicho kimekuwa kivutio kwa wachuuzi wengi zaidi kusogea eneo hilo kuendesha biashara zao. 

Haya yanayoonekana Ubungo yapo maeneo mengi katika Jiji la Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Shinyanga na maeneo mengi yanayokua kwa kasi kama Shinyanga na kote nchini.

Katika Jiji la Dar es Salaam tatizo hili ni kubwa zaidi. Mitaa mingi katika maeneo ya Kariakoo, na hasa Posta, sehemu zilizotengwa kwa waenda kwa miguu zimevamiwa na wachuuzi hawa. Watu wanalazimika kuyakwepa magari, bodaboda na aina nyingine za usafiri.

Leo Dar es Salaam huwezi kujua wapi ni sehemu ya gulio, wapi ni mahali maalumu kwa ajili ya kupata chakula, vinywaji na kadhalika. Kila kitu kinapatikana kila mahali! 

Dar es Salaam limekuwa jiji lisilokuwa na mpangilio wa kitu chochote kuanzia uchuuzi, ujenzi holela na hata uendeshaji vyombo vya moto, hasa pikipiki.

Leo hii si jambo la uvunjifu wa sheria, kuziona pikipiki zikiendeshwa upande ambao hauruhusiwi kwa mujibu wa Sheria za Usalama Barabarani. Njia ya kupanda wanashuka, ya kushuka wanapanda ilimradi vurugu kila mahali.

Nalizungumza suala hili, na hasa la Ubungo, katika kuonesha kuwa matatizo mengi katika nchi yetu tumeyalea sisi wenyewe. Tatizo linaanza kujionesha mapema likiwa bichi kabisa, lakini mamlaka husika zitajifanya hamnazo na kuliacha lipevuke na mwishowe liwe chanzo cha uvunjifu wa amani katika jamii.

Matokeo ya vilio, vifo na kelele vinavyoendelea kutokana na bomoabomoa ni matokeo ya uzembe huu huu wa watendaji katika Serikali za Mitaa hadi Serikali Kuu. Ni matokeo ya uzembe kwa sababu viongozi wa ngazi zote walikuwapo wakati wananchi wakijongea maeneo hayo na kujitwalia ardhi hadi wakaanza kujenga.

Rushwa na pengine hofu ya kipuuzi ya kuogopwa kulogwa zimewafanya baadhi ya watendaji wasite kuchukua hatua kukabiliana na matatizo yakingali madogo.

Matokeo ya uzembe huu ni lawama zinazoelekwa katika Serikali ya Awamu ya Tano, lakini ukweli ni kuwa kinachoonekana sasa ni matokeo ya uongozi mbovu wa awamu zilizopita.

Nini kifanyike? Hatuwezi kubaki kuwa watu wa kulalama tu. Rais John Magufuli hawezi kufumbia macho mambo ya ovyo yaliyofanywa na watangulizi wake kwa sababu ya kuogopa lawama! Akiogopa lawama hawezi kuongoza nchi. Rais lazima awe na roho ngumu yenye kumwongoza kuiokoa jamii yake ili ifikie kiwango cha ustaarabu kinachokubalika.

Kuanza kuwaondoa wavamizi wa maeneo ya waenda kwa miguu si jambo linalohitaji amri ya Rais Magufuli, au mawaziri wenye dhamana na masuala ya mipango miji.

Viongozi wa Serikali za Mitaa wasiwe watu wa kusubiri kupokea amri na maelekezo kutoka juu. Waamke waone hatari inayolikabili Taifa na wapate njia sahihi za kukabiliana nayo kabla haijalipuka.

Ni kwa kulitambua hilo, Serikali za Mitaa watakuwa na fursa ya kuketi na kuona ni maeneo gani yanayopaswa kutengwa kwa ajili ya wachuuzi, mafundi magari, watengeneza majeneza, kina mama na baba ntilie, na wafanyabiashara wa kila aina.

Biashara kama ya majeneza pale Manzese, si biashara ya kufanyiwa maonesho. Kisaikolojia biashara hiyo inaweza kuwa na athari kubwa kwa wapita njia, kwa hiyo ni wajibu wa watendaji kuweka sheria ndogo ndogo za uendeshaji biashara hiyo. Hilo halihitaji ushauri kutoka Benki ya Dunia.

Maeneo kama ya Mbezi Mwisho (Barabara ya Morogoro), kila anayepita eneo lile asubuhi au jioni ataona namna idadi ya watu ilivyo na inavyoendelea kuongezeka.

Ataona namna wachuuzi walivyoamua kuingia hadi kwenye barabara kuendesha biashara zao. Watendaji wa Serikali za Mitaa wenye bongo zinazofanya kazi, bila shaka watatambua kuwa muda wa eneo hilo kuwa na soko kubwa la kisasa umeshawadia; na kwa hiyo kinachotakiwa ni kufanya mipango ya kutwaa eneo na kufungua soko. Mawazo ya aina hii hayahitaji msaada au hisani ya ‘Watu wa Marekani’. Ni jambo la watu wenye nia njema na nchi yao kuamua mara moja ujenzi wa soko la kisasa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wananchi.

Kufanya hivyo ni muhimu kwa sababu huwezi kuiacha Mbezi Mwisho iendelee na hali hii inayoonekana sasa.

Watu waungwana hawawezi kujenga nyumba, wakajenga jiko, lakini wakapuuza kujenga mahali pa kutunzia kinachotokana na chakula kilicholiwa!

Kama Serikali za Mitaa zingekuwa makini, bila shaka lawama na vilio vingi katika nchi yetu visingekuwapo, ingawa bado muda wa kuvikomesha tunao.

Wakishatenga maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali, hapo watakuwa na sababu zenye mashiko za kuwaondoa wavamizi, wakiwamo hawa wa njia za waenda kwa miguu.

Serikali za Mitaa na hata Serikali Kuu wawe na utaratibu wa kukabiliana na viashiria vya vurugu, badala ya kusubiri mambo yawe makubwa.

Kinachoendelea Ubungo sasa endapo kitaachwa kidumu, siku ya kuwaondoa wavamizi wake kutakuwa na vilio na hata umwagaji damu (Mungu atuepushe). Inawezekana kabisa watu wakapoteza mali zao, lakini huenda wakawapo watakaojeruhiwa kama matokeo ya mapambano kati ya vyombo vya dola na wachuuzi hao.

Lakini ili hilo lifanyike, zitahitajika fedha na rasilimali watu. Magari ya Manispaa/Jiji, Polisi na vyombo vingine yatahitaji mafuta. Posho zitalipwa. Gesi za machozi zile ni pesa za walipa kodi. Shughuli za kiuchumi zitasimama. Kadhia hiyo inaweza kuamsha hasira za wananchi kwa Serikali yao. Hizi zitakuwa gharama zilizosababishwa na uzembe wa watendaji katika Serikali zetu za Mitaa wasiotaka kukabiliana na dalili, isipokuwa ugonjwa kamili! Wahenga walisema kinga ni bora (nafuu) kuliko tiba! Hatuna sababu ya kuyapuuza kwa maneno hayo.

Tujitahidi kuwa na Serikali isiyotegemea kuendesha mambo yake kwa ‘operesheni’ za mara kwa mara. Tujenge utaratibu wa watu kuheshimu taratibu, na hilo litawezekana endapo tutakuwa na viongozi na watendaji walio makini katika kukabiliana na dalili zozote za uvunjifu wa taratibu katika nyanja na maeneo mbalimbali.

Watu wanapovamia misitu wanapaswa kuondolewa mapema iwezekanavyo, badala ya kusubiri wateketeze miti ndipo umuhimu wa kuwaondoa uonekane.

Nchi zote duniani zilizostaarabika watu wake wanaendesha mambo yao na kuishi kustaarabu. Wanafuata sheria na kanuni mbalimbali zinazotawala maisha yao ya kila siku. Watendaji katika nchi hizo ni wepesi wa kukabiliana na hatari wanayoiona kabla haijazaa matatizo makubwa.

Hayo yamewezekana kwa sababu wananchi katika mataifa hayo wametambua na kusimamia haki na wajibu wao.

Wamekuwa mstari wa mbele kuwadhibiti watu wanaoona wanataka kupindisha mambo. Kwa mfano, wanapoona uchafuzi wa mazingira, hawasubiri watendaji wakabiliane na jambo hilo kwa kupita eneo husika, isipokuwa wao wanakuwa na wajibu wa kuzitaarifu mamlaka zinazohusika.

Hapa kwetu moyo wa uzalendo wa aina hiyo ulikuwapo miaka ya 1960, 1970 hadi miaka ya 1980 wakati uongozi wa nchi ulipokuwa ukijitahidi kuwafanya Watanzania waione Tanzania ni yao; na kwamba kila raia ana wajibu wa kuilinda nchi yake.

Moyo huo umefifishwa na mambo mengi, lakini kubwa ni unafsi miongoni mwetu.

Mara zote nimependa kukisoma kijitabu cha TUJISAHIHISHE kilichoandikwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mei 1962.

Sehemu ya kijitabu hicho, Mwalimu anasema: Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga ni unafsi. Pengine huwa tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine twaweza kuwa hatuna cheo chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tamaa yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni unafsi mbaya sana”.

Maneno haya ya Mwalimu yatupasa tuyatumie kama dira ya kuijenga nchi yetu. Tunapaswa kurekebisha kasoro zetu nyingi bila unafsi wala woga.

Bahati nzuri Tanzania tumempata Rais Magufuli, ambaye amedhamiria kwa vitendo kufuata nyayo na maandiko ya aina hii kutoka kwenye hazina kubwa ya maandishi ya Baba wa Taifa.

Tukiweka unafsi na woga pembeni – iwe kwa viongozi, watumishi wa umma hadi kwa mwananchi mmoja mmoja – Tanzania itabadilika na kuwa nchi nzuri zaidi. Wajibu wa kuyapata mabadiliko haya upo kwa kila mmoja wetu na kwa nafasi aliyonayo.

1166 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!