ManyerereWabunge wazoefu wamelia na kuiomba Serikali isibariki “mauaji” haya kwa wakulima wetu. Wametumia kila aina ya maneno kuwashawishi wakubwa serikalini, lakini mwishowe wameshindwa. Historia itawahukumu kwa haki. Hansard zipo. Nani hawezi kuamini kuwa ushindi ambao serikali imeibuka nao bungeni umetokana na nguvu za fedha?

Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya, alizungumza vizuri sana suala la haya yanayoitwa mafuta ghafi. Akasema hakuna kitu kinachoitwa “mafuta ghafi”. Wanachofanya wafanyabiashara ni kuleta mafuta yaliyokwishasafishwa. Kwa kufanya mambo kwa uhakika, na kusema lililo la kweli, daktari huyu akasema alisafiri hadi Indonesia, Malaysia na kila kulikostahili, kwa ajili ya kufanya uchunguzi. Akasema kwamba hicho kinachosemwa kwamba ni ghafi, ni uongo. Hakuna mafuta ghafi yanayoingizwa Tanzania, bali ni mafuta halisi ya kula yaliyokwishapitia usindikaji kwa asilimia 95! Huyu hawakumsikia.

Mbunge wa Kibaha Mjini, Dk. Gama, juzi alitumia kila aina ya maneno kuonyesha kuwa uamuzi wa serikali ni mauaji kwa wakulima wetu masikini. Hawakumsikia.

Mbunge wa Tabora Mjini, Silaju Kaboyonga, akahoji kama kweli ni akili kufanya hicho kilichokuwa kimeandaliwa na serikali. Hakuna kiongozi wa serikali aliyefungua masikio kuwasikiliza, wala hakuna aliyefungua akili kufanya tafakuri ya maneno hayo.

Mbunge wa Kasulu Magharibi Kilontsi Mporogomyi, yeye alikwenda mbali zaidi. Akatoboa kwamba kuna dalili zote za rushwa kwenye suala hilo. Yeye pia alishakwenda huko nje kujiridhisha kama kweli kinacholetwa ni mafuta ghafi. Akakuta ni uongo. Hakuna mafuta ghafi, bali ni mafuta yaliyokwishasindikwa. Akafikia hatua ya kupendekeza Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza hujuma hii. Sijui kama Bunge litakuwa na ubavu huo.

Hawa ni sehemu ndogo tu ya wabunge wengi sana waliopinga uondoaji ushuru wa asilimia 10 kwenye mafuta hayo. Awali, nilidhani kuwa busara za wabunge wapinzani ndizo hubezwa, kumbe hata wa CCM nao yanawakuta!

Kauli za serikali, kupitia kwa Naibu Mawaziri wa Fedha na Uchumi juzi ni kwamba kama hawataondoa ushuru wa asilimia 10 kwenye mafuta hayo, maana yake ni kwamba viwanda “vyetu” vitakufa! Viwanda gani? Vya kina nani? Wenye viwanda hivi ni wengi kuliko wakulima wa nafaka?

Mwenyekiti Mao Tse Tung wa China aliwahi kupiga marufuku uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi hiyo. Alipiga marufuku akilenga kuhakikisha Wachina wenyewe wanabangua bongo, wasomi wanakesha, wana sayansi wanakuna vichwa kupata njia sahihi ya kujitegemea. Alipiga marufuku hata uagizaji viatu.

Watu walipiga kelele. Wakasema Mao alikuwa mtesaji. Wakamtukana. Wakampa majina mabaya ya kila aina. Nchi za Magharibi, kwa kujua Mwenyekiti Mao alikuwa akipeleka ukombozi kwa wananchi wake, zikapandikiza uongo na chuki. Eti huo ulikuwa ukiukaji haki za binadamu. Yote hayo yalikuwa ni kutaka kuhakikisha China inaendelea kuwa soko la Ulaya na Marekani. Na ili iendelee kuwa soko, lazima kuwapumbaza Wachina waendelee kununua vitu vya nje. Lakini wapi? Mwenyekiti Mao akawa imara.

Alipofariki dunia, viongozi waliomfuata waliboresha mawazo yake. Wakayachanganya na mawazo mapya. Wakapata sera nzuri za kujenga uchumi wao. Lakini kubwa walilokuwa wameweka mbele ni suala la kujitegemea. Mwenyekiti Mao na viongozi hao waliomfuata, waliamini kuwa katika kujitegemea lazima kuwe na mahali pa kuanzia!

Akili kama hiyo haimo miongoni mwa viongozi wetu wengi. Waziri anapoamini kuwa ukombozi wa wananchi wake, ukombozi wa wakulima makabwela wa nchi yake ni kuruhusu kuingizwa kwa mafuta yasiyolipiwa ushuru, huyo haitakuwa dhambi kumpeleka Mirembe.

Mawazo tegemezi yametufanya tuwafunge watengeneza magobore, badala ya kuwaendeleza. Gongo tumeendelea kuiita kuwa ni pombe haramu. Tunaagiza kila kitu hadi njiti za meno. Akili na uongozi wa aina hii haviwezi kuleta mapinduzi katika nchi yetu.

Waziri mwenye akili ya ukombozi kwa wananchi na nchi yake ni yule anayezuia mbinu zozote za kuwanufaisha wakulima wa nchi ngeni wasipate mwanya wa kuwaua wakulima katika nchi yake.

Waziri wa aina hiyo, atakachofanya ni kuhakikisha anapiga marufuku uingizaji bidhaa kadhaa, na kwa sababu hiyo, atapandisha thamani ya bidhaa hiyo. Wananchi wakishaona thamani ya karanga, pamba, alizeti, mawese imepanda, wengi watajiingiza kwenye kilimo. Watazalisha nafaka nyingi. Zitaijaza nchi. Ziada itapelekwa kuuzwa ughaibuni. Hiyo ndiyo akili inayoweza kumkomboa mkulima masikini wa nchi hii.

Waziri anaposema hatuna malighafi ya kutosheleza mahitaji, kisha akaua mbinu halali ya kuongeza uzalishaji nchini, huyo ni msaliti, na kama kuna hukumu, huyo anastahili kuhukumiwa hata kama ni kwenye sanduku la kura.

Kama hatuna malighafi ya kutosheleza, ni muujiza gani utafanya malighafi hiyo iongezeke kwa kuruhusu kuingiza nchini mafuta ambayo wakulima wake wanalipwa ruzuku?

Kwa aina hii ya uongozi (wa mwaka 2009), sioni kama kuna ukombozi wa mkulima katika nchi hii. Tanzania itabaki kuwa nchi yenye maneno mengi yasiyokuwa na tija kwa wananchi. Tutabaki kuwa nchi ya upembuzi, upembuzi yakinifu, programu, mipango, sera, ilani, mkukuta, mkurabita na kila aina ya misamiati ambayo inachusa kuisikia.

Kama kweli Serikali na Bunge wanapuuza kuona faida za kuwa na wakulima hawa wadogo, tunakoelekea ni kubaya. Kama viongozi wetu hawaoni mafuta mazuri ya alizeti yanayouzwa pale Singida, mafuta yanayotokana na teknolojia ya mikono; tuna sababu gani ya kuwaamini?

Nawapa pole wakulima. Wamenyongwa na watu waliowachagua. Wamepuuzwa na watoto wao waliowasomesha kwa fedha hizo hizo za alizeti na ufuta! Wametiwa kitanzi cha maisha na hao hao walioapa kuwatetea.

Wakulima wasikate tamaa wala kuhuzunika. Huu ni mchakato wa mapambano ya kuelekea kwenye ukombozi wa haki. Wengine migongo yao imepinda kwa kutumia jembe la mkono. Wengine wamepoteza jicho au macho kutokana na kuumizwa wakati wa kulima au kuvuna. Wengine wana makovu yanayotokana na visiki mashambani. Wengine wanang’atwa nyoka au kuliwa na simba au mamba wakihangaika mashambani.

Kana kwamba hayo hayatoshi, wameongezwa maumivu mengine. Watawala wameamua kuwabebesha mzigo wa wakulima wa Indonesia na Malaysia. Wakulima wetu wasikate tamaa. Kuna siku, kama si wao, basi watoto na wajukuu wao watafurahi. Hatutarajii kudumu milele na viongozi wasiokuwa na huruma kwa wakulima. Yana mwisho.

Kama ushuru huo ni matokeo ya mlungula miongoni mwa viongozi wetu, Mungu wa haki ataamua.

Hadi hapo hayo yatakapotimia, kizazi cha wakulima kitakachokuwa kimejaa furaha kitaimba kwa kusema:

Mkulo ulitutesa, Wakulima tukalia

Ulitufanya matasa, Maisha tulililia

Njoo utuone sasa, pepo tumefungulia

Mwenyezi Mungu wa haki, Hawatupi waja wake.

 

Wakulima ughaibu, Uliwaona nduguzo

Pesa ziliwaghiribu, Tukafanana uozo

Wote mkawa mabubu, Maisha yetu mzozo

Mungu yule wa Yakobo, Ndiye wa Abrahamu.

 

Mashangingi mlipanda, Mkapuza makabwela

Zamu ni yetu kudanda, Jehanamu mtalala

Taadhima imepanda, Mapochopocho twayala

Kumwonea mkulima, Laana mmeipata.

By Jamhuri