DAR ES SALAAM

Na Dennis Luambano

Kampuni ya Tanga Cement PLC imeendelea kutoa malalamiko yake kwa Idara ya Kazi Mkoa wa Tanga baada ya wataalamu saba kutoka Afrika Kusini waliokuja kutoa mafunzo ya uendeshaji mitambo kwa wafanyakazi wao kukamatwa tena kwa mara ya pili baada ya kuachiwa, kisha wamefikishwa mahakamani.

Awamu hii si wataalamu hao tu waliokamatwa (vibali vyao vya kazi katika mabano) ambao ni Francois Kleyn (0062818), John Pienaar (0062815), Keith Randall (00062998), Charles Albert (00062817), Jan Andries Van Der Westhuizen (00062691), Wayne Van Niekerk (0062822) na Charles Thoneson (00062692), bali pia maofisa waandamizi wa kampuni hiyo, Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu, Diana Mwakitwange na Kaimu Meneja wa Mitambo na Uzalishaji, Mhandisi Gadiel Benjamin, nao wamekamatwa.

Kisa cha kukamatwa wataalamu hao kwa mara nyingine ni tuhuma zilezile kama Gazeti la JAMHURI lilivyoripoti Oktoba 5, mwaka huu kwamba wanadaiwa kufanya kazi nchini bila kuwa na vibali vya kazi vinavyotolewa na idara hiyo.

Awali, wataalamu hao kutoka Kampuni ya Multi Tegnik ya Afrika Kusini walikamatwa Septemba 6, mwaka huu na maofisa wa idara hiyo na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Chumbageni kwa mahojiano kisha Septemba 29, mwaka huu ikawafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga na kesi hiyo ikatajwa kwa mara ya kwanza na kuahirishwa hadi Oktoba 20, mwaka huu ilipotajwa tena.

Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita, Ofisa Masoko na Mawasiliano wa Tanga Cement PLC, Mtanga Noor, anasema licha ya kufutiwa mashitaka na mwendesha mashitaka baada ya wataalamu hao kwenda mahakamani siku hiyo (Oktoba 20, mwaka huu) kusikiliza mwenendo wa kesi yao inayowakabili baada ya kutajwa kwa mara ya pili lakini wakakamatwa tena hapo hapo na askari waliovaa kiraia kisha wakawapeleka katika Kituo cha Chumbageni.

Mtanga anasema baada ya wataalamu hao kufikishwa kituoni hapo ndipo maofisa wengine wa kampuni hiyo, Diana na Gadiel, wakaitwa na kuunganishwa katika kesi hiyo na Oktoba 21, mwaka huu wakafikishwa tena mahakamani hapo na kusomewa mashitaka ya awali ya kutokuwa na vibali vya kufanya kazi huku wale maofisa mashitaka yao ni kuwaruhusu kuja nchini kufanya kazi bila kuwa na vibali hivyo.

Pia anasema baada ya kusomewa mashitaka hayo, watuhumiwa hao wakaachiwa kwa dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 25, mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Kutokana na sakata hilo kutopatiwa ufumbuzi, Mtanga, anasema Septemba 30, mwaka huu wamemwandikia barua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenister Mhagama, kumuomba aingilie kati lakini hadi sasa bado hawajajibiwa.

Mtanga akinukuu barua hiyo iliyoandikwa na Diana na nakala kwenda kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, anasema kutokana na wataalamu hao kuzuiwa kutoa mafunzo kwa vitendo (on job training) kwa wafanyakazi wao, hali ya kuharibika kwa mitambo mara kwa mara imeanza kujirudia kama mwanzo.

“Hali hii inasababisha kuzorota kwa uzalishaji wa saruji, serikali itakosa mapato, kukosekana kwa ajira kwa wafanyakazi, makandarasi na wadau wengine pamoja na shughuli nyingine zote za kiuchumi zinazotokana na uzalishaji wa saruji. 

“Tunapenda kuwasilisha ombi katika ofisi yako la kusaidia wataalamu hao saba wa kigeni kuruhusiwa kuendelea kurekebisha mitambo na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wetu. Ni matumaini yetu kuwa hatua hii itasaidia kuepusha athari zinazotokana na kuharibika kwa mitambo,” anasema Mtanga.

Anasema kutokana na changamoto kubwa ya kuharibika kwa mitambo yao waliyoipata Julai, mwaka jana na kusababisha uhaba wa saruji ndipo wakafanya jitihada za kuhakikisha hali hiyo haijirudii, kwa kuamua kununua mitambo mipya ya kisasa.

“Mwaka 2016 tulizindua mtambo unaotumia teknolojia ya kisasa huku tukiendelea kutegemea uzoefu wa wafanyakazi wetu, kwa sasa, wengi wenye uzoefu walishastaafu na waliobaki ni vijana wasio na uzoefu wa kutosha. Changamoto hii ya uzoefu mdogo inasababisha kuharibika mara kwa mara kwa mtambo na vipuri vyake,” anasema na kuongeza: 

“Mtambo wa zamani nao unahitaji ukaguzi wa mara kwa mara na uangalizi wa karibu, kwa sababu ya uchakavu. Kwa bahati mbaya, hakuna taasisi hapa nchini inayotoa mafunzo mahususi ya saruji ili kutoa mafunzo ya mabadiliko ya kiteknolojia.” 

Pia anasema baada ya wataalamu hao kuanza kutoa mafunzo kwa vitendo, mitambo yao ilitengemaa na ilipoharibika matengenezo yalichukua muda mfupi.

Katika hatua nyingine, anasema Oktoba Mosi, mwaka huu pia wamemwandikia Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima, barua kama hiyo wakielezea malalamiko yao kuhusu wataalamu hao kuzuiliwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wao na kusababisha kushuka kwa uzalishaji wa saruji kutokana na ubovu wa mitambo yao lakini naye hakuchukua hatua zozote.

Aidha, anasema mwekezaji wa kampuni hiyo anaona hatendewi haki na Idara ya Kazi kutokana na sakata hilo kwa kuwa uzalishaji wa saruji unashuka na kabla wataalamu hao hawajafikishwa mahakamani ameomba mara kadhaa nafasi ya kujieleza kwa mamlaka husika lakini hakupewa nafasi.

“Mwekezaji anaona endapo mitambo itaendelea kusumbua tena na hakuna mafundi hapa nchini atafanyaje? Afunge kiwanda? Akifunga athari zake zitakuwa kubwa, kwa sababu sasa hivi serikali ina miradi mikubwa inayohitaji saruji,” anasema Mtanga. 

Kwanini sakata la wataalamu hao limeibuka? 

Oktoba 5, mwaka huu JAMHURI tuliripoti kwamba sakata hilo limesababishwa na kukinzana na kugongana kwa taratibu na sheria kati ya idara mbili nyeti za serikali ambazo ni Idara ya Uhamiaji na Idara ya Kazi mkoani Tanga, baada ya Idara ya Kazi kuwakamata na kuwafungulia mashitaka.

Mtanga amelieleza JAMHURI kuwa si mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kuwaleta nchini wataalamu kutoa mafunzo ya ukarabati wa mitambo ya kuzalisha saruji na klinka.

Anasema walifuata taratibu zote za Uhamiaji kuhakikisha hakuna usumbufu utakaowapata, ikiwamo vibali kwa ajili ya ‘kazi maalumu’.

Vibali hivyo ni maalumu kwa wafanyakazi ambao si waajiriwa rasmi kufanya kazi kwa muda usiozidi miezi mitatu.

“Tanga Cement inaendeshwa kwa weledi mkubwa na kwa kufuata sheria zote za nchi ndiyo maana inaaminika katika utendaji wake,” anasema.

JAMHURI linafahamu kwamba wataalamu hao waliingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, wakapatiwa vibali (business visa) na Idara ya Uhamiaji na kutimiza masharti yote ya kuingia nchini. 

Vibali kama hivi hutolewa kwa wageni kwa ajili ya kazi maalumu kama kurekebisha mitambao na kuendesha mafunzo maalumu ya muda mfupi na kazi nyingine kwa mujibu wa sheria za Uhamiaji.

“Waliwasili nchini Agosti 9 na 19, mwaka huu, hivyo hawajavusha muda waliopewa na Uhamiaji, yaani miezi mitatu,” anasema.

Kwanini wamekuja nchini?

Kuhusu sababu za kampuni kuwaleta nchini wataalamu hao, Mtanga, anasema wakati taifa lilipokumbwa na uhaba wa saruji katika siku za hivi karibuni, Tanga Cement wakajikuta wakikumbana pia na changamoto ya mitambo.

“Hapo tukalazimika kuwaita wataalamu kuja kufanya ukarabati wa mitambo. Sisi ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa saruji nchini, hivyo inapotokea changamoto ya kiuzalishaji au usambazaji, athari yake huonekana wazi. 

“Tukaamua kuleta wataalamu watakaowafundisha wafanyakazi wa Kitanzania ili tatizo kama hilo lisijitokeze tena,” anasema Mtanga.

Baada ya kampuni kununua vipuri kwa fedha nyingi, Mtanga anasema wakalazimika kuwapa kazi ya kuvifunga vipuri hivyo kampuni ilivyovileta.  

“Kwa maana hiyo hawa si waajiriwa wa Tanga Cement ila ni waajiriwa wa Kampuni ya Multi Tegnik ya Afrika Kusini iliyotuuzia vipuri, kisha tukaipa kazi ya kuvifunga na kuwapatia mafunzo wafanyakazi wetu, huku wakibadilishana utaalamu,” anasema. 

Ni wafanyakazi watano tu miongoni mwa 267 walioajiriwa na Tanga Cement ndio wageni wenye kuhitaji vibali vya Uhamiaji.

Jinsi walivyokamatwa kwa mara ya kwanza

Septemba 6, mwaka huu, maofisa wa Idara ya Kazi Mkoa wa Tanga wakiongozwa na Janeth Omolo, walifika kiwandani hapo kufanya kile kilichoelezwa awali kama ‘ukaguzi wa kawaida’.

Huku Janeth akionekana kupewa maelekezo kwa njia ya simu, anasema Mtanga, akawa akiwataka wenyeji wake kumpeleka idara moja hadi nyingine na kila alipokuta mgeni, alimuamuru kuandamana naye.

“Tukamwambia ni vema tumuitie wageni wote, kwa sababu tunafahamu kuwa wapo kihalali. Wana vibali vinavyowaruhusu kufanya kazi.

“Akawachukua wale wageni wataalamu saba na kwenda nao Kituo cha Polisi Chumbageni, wakatoa maelezo, wakaachiwa kwa dhamana.

“Tukaanza kutafuta miongozo bila mafanikio. Tulikwenda hadi Dodoma kuonana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi akiwa na Kamishna wa Kazi na Ofisa wa Kazi. Tukaelekezwa kurudi Tanga kutafuta ufumbuzi,” anasema.

Anasema wamekuwa wakikutana mara kadhaa na Janeth lakini hakuna ufumbuzi uliopatikana. 

Anasema Idara ya Kazi mkoani Tanga inataka wataalamu hao watafutiwe vibali vya kazi, suala ambalo ni kinyume cha sheria na utaratibu. 

“Moja ya mahitaji ya kupata vibali vya kazi ni kuwa na mkataba kati ya mwajiri na mfanyakazi. Hawa sisi si wafanyakazi wetu. Tanga Cement haina mkataba nao wala haijawaajiri wataalamu hawa, hivyo hatuwezi kuomba vibali vya kazi kwa ajili ya watu ambao hatuna mkataba nao wa ajira,” anasema.

Idara ya Kazi, Uhamiaji wagoma kuzungumza

Septemba 29, mwaka huu JAMHURI lilimtafuta Ofisa Kazi Mkoa wa Tanga, Janeth Omolo, kujua kwa nini wataalamu hao wamefikishwa mahakamani licha ya kuwa na vibali vya Uhamiaji, na akajibu kwa kifupi:

“Suala lililopo mahakamani siwezi kulizungumzia, tuiache mahakama ifanye kazi yake.”

Kwa upande mwingine, JAMHURI limezungumza na Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga, Petro Malima, kujua sababu za wataalamu hao kukamatwa licha ya kuwa na vibali vinavyodaiwa kuwa ni halali na vimetolewa na Idara ya Uhamiaji.

“Ni vema ukamuuliza mtu wa ‘Labour’ (Idara ya Kazi) kwa sababu (wageni hao) wana vibali vya Uhamiaji. Lakini ukiona ni muhimu kuniona, basi ninaomba tuonane kesho (Jumatano ya wiki iliyopita),” anasema Malima.

Katika hatua nyingine, Tovuti ya Idara ya Uhamiaji (www.immigration.go.tz) inasema kibali (business visa) kinatolewa kwa raia wa kigeni kuingia nchini kwa madhumuni ya kufanya kazi maalumu kama kukarabati mitambo au kuendesha mafunzo ya muda mfupi.

Pamoja na mambo mengine, pia kufanya kazi za kitaaluma kama uhasibu au kufanya shughuli halali iliyoruhusiwa kisheria huku kampuni inayomleta nayo inatakiwa kuwasilisha nyaraka halali, ikiwamo leseni ya biashara na cheti cha kampuni na mkataba unaoonyesha shughuli maalumu atakazofanya raia huyo wa kigeni.

Hii si mara ya kwanza

Migongano kama hii ya kiidara imekuwa ikitokea mara kwa mara na kuwasababishia usumbufu mkubwa wataalamu kutoka nje pamoja na wawekezaji.

Miaka kadhaa iliyopita wataalamu walioletwa nchini na Kampuni ya uwindaji wa kitalii, Ortello Business Cooperation (OBC), walijikuta wakikamatwa na maofisa wa serikali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Wataalamu hao walidaiwa kufanya kazi bila kuwa na vibali halali, pamoja na ukweli kwamba waliletwa nchini kwa kazi maalumu na ya muda mfupi, ambayo hadi wanakamatwa walikuwa wamekwisha kuikamilisha.

Baada ya mivutano ya kisheria na makubaliano waliachiwa ingawa tayari jina la Tanzania kwa wawekezaji kutoka nje lilikuwa limekwisha kuchafuliwa.

By Jamhuri