Nionavyo mimi, jiji la Dar es Salaam limejaa. Watu, magari, na changamoto za kila aina.
 Takwimu za Sensa ya Taifa ya mwaka 2012 ilionesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na wakazi 3,133 kwa kilomita ya mraba wakati wastani wa Taifa ulikuwa watu 51 kwa kilomita ya mraba. Ni Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar pekee ndiyo unakaribia wingi huu wa watu kutokana na takwimu hizo: watu 2,581 kwa kilomita za mraba.


 Mkoa wa Dar es Salaam ulikadiriwa kuwa na wakazi 4,360,000 na ndiyo unaoongoza kwa kuwa na wakazi wengi ukilinganisha na mikoa mingine ya Tanzania.
 Leo, idadi itakuwa imeongezeka kiasi fulani. Sensa hiyo hiyo ilikadiria ongezeko la asilimia 5.6 kwa kipindi cha mwaka 2012 hadi 2012. Imekadiriwa kuwa idadi ya Watanzania itafikia milioni 100 ifikapo mwaka 2050. Kwa hiyo tutarajie kuwa mijini pia, ambako sensa ya 2012 imekadiria wakazi kufikia asilimia 29.1 itaongezeka kwa kiasi fulani.


 Sababu kubwa ya msingi inayofanya watu kuhama vijijini ni kukosa kazi ambazo zitawapa kipato cha kugharamia maisha yao. Wahamiaji wengi ni vijana ambao huhamia mijini kutafuta ajira. Kwa uzoefu wangu, kwenye baadhi ya maeneo vijana wachache ambao wamebaki vijijini hawana ari ya kufanya kazi kama waliokuwa nayo wazazi wao. Shughuli kubwa ya vijijini ni kilimo, lakini vikwazo mbalimbali vinawafanya vijana kuamua kuwa ni bora kutafuta ajira za mijini kuliko kushiriki kwenye shughuli za kilimo. Kikwazo kimoja ni kuwa bei za mazao mengi hazipandi kwa kasi inayolingana na kupanda kwa gharama za maisha, kwa hiyo kila miaka inavyozidi kusonga mbele, ndivyo mkulima anavyojikuta anakabiliwa na gharama ambazo hupanda — za mbegu au pembejeo — lakini zisizoambatana na kupanda kwa bei za mazao yake. Ni wakulima wa maua au bangi tu, na mazao machache ambayo hayalimwi na Watanzania wengi, ndiyo hawaathiriki na bei ndogo za mazao yao.


 Lakini kuna matatizo mengine mengi ndani ya mazingira hayo hayo ya kilimo, kwa mujibu wa tafiti za IFAD, shirika la kimataifa linalojihusisha na maendeleo ya kilimo: Uzalishaji duni, kukosekana kwa masoko, uchakavu wa ardhi inayotumiwa kwa kilimo, kuteketea kwa misitu, na uwepo wa mifugo mingi kulinganisha na ufinyu wa malisho kwa mifugo.
Aidha, kwa mujibu wa IFAD tena: Umasikini wa vijijini unatokana na upungufu wa ardhi nzuri ya kilimo na vyanzo vya maji, matatizo ya ukame na mafuriko, kukosekana kwa miundombinu ya usafiri inayounganisha maeneo ya vijiji na masoko, taasisi changa zisizo na uzoefu wa kutetea maslahi ya wakazi wa vijijini, na kukosekana kwa kiungo cha moja kwa moja kati ya shughuli za kiuchumi za vijijini na zile za uchumi wa Taifa.


 Kuna sababu nyingine inayohamisha watu vijijini. Vijana wengi huhamia mijini kwa ajili ya kufuata elimu na wanapomaliza elimu zao hubaki mijini kwa sababu hawaoni fursa za kazi vijijini zinazolingana na elimu yao. Hapa yafaa kukumbuka aliyoyasisitiza Mwalimu Nyerere kwenye Sera ya Elimu ya Kujitegemea kwamba ni muhimu elimu iwaandae wanafunzi kukabiliana na mahitaji na changamoto zilizopo kwenye maeneo wanaoyoishi.
 Unapoishi Dar es Salaam wakati wote unaweza usitambue athari za ongezeko kubwa la wahamiaji, lakini ni pale unapokuwa unaishi sehemu nyingine na kufika Dar baada ya muda ndiyo athari hizo zinaonekana vizuri. Sasa hivi jijini Dar es Salaam unapoalikwa kumtembelea mtu nyumbani kwake ni adhabu. Muda ninaotumia kusafiri kati ya Butiama na Mwanza ni mdogo kuliko muda ambao najaribu kutoka eneo moja la jiji la Dar kwenda eneo jingine.
 Mwaka 2012, Waziri John Magufuli alitamka kuwa kuna magari milioni moja Dar es Salaam na yanaongezeka kila siku. Kila mtu mwenye uwezo ananunua gari, na matokeo yake ni kuwa wamiliki wa gari wanabanana kwenye jiji ambalo miundombinu yake ya barabara haikidhi ongezeko la magari.


  Kijijini mtu akikualika nyumbani kwake unashukuru. Dar es Salaam ukimtembelea mtu nyumbani kwake yeye ndiyo anapaswa kukushukuru, kwa sababu unalazimika kutumia muda mwingi kukamilisha jambo hilo. Athari za ongezeko la watu Dar siyo wingi wa magari tu. Athari mojawapo kubwa ambayo haikumbukwi na wengi ni kuwa vijana wanaohamia mijini huwaacha wazazi vijijini ambao hawana nguvu kazi ambayo zamani iliwasaidia kumudu gharama za maisha. Matokeo yake ni kuwa utakuta baadhi ya wazee ambao wanahangaika na shughuli ambazo zingefanywa na watoto wao. Athari nyingine kubwa ya kasi kubwa ya uhamiaji kuja Dar es Salaam ni ongezeko la makazi holela katika maeneo ambayo ni hatarishi kama vile mabonde ya mito. Mvua kubwa au za mfululizo zinaponyesha zinasababisha mafuriko yanayoleta pia hasara ya mali na hata kupoteza maisha, kama ambavyo imetokea tena hivi karibuni kwenye msimu wa mvua ulioanza hivi karibuni.


 Tatizo jingine ni kuwa upatikanaji wa ajira mijini haulingani na kasi ya ongezeko la watu na matokeo yake ni kuwa kuna umati mkubwa wa watu ambao hawana ajira na ni lazima watafute namna ya kuishi mijini. Wengi wao wanakuwa ni tegemezi kwa wale wachache wenye ajira na hiyo pekee inafanya hata wale walioajiriwa kuwa siku zote wanatafuta mbinu  nyingine halali, nyingine siyo halali, za kuongeza kipato ili kugharamia watu wanaowategemea. Bila shaka mfanyakazi mmoja kutegemewa na watu wengi inaweza kuwa kichocheo cha rushwa na utovu wa uaminifu katika maeneo mengi ya ajira.


 Suluhisho linajulikana tangu tumepata uhuru. Ni pale maendeleo ya kweli yatakapofika vijijini ndiyo watu wataacha kuhamia mijini. Tangu tumepata uhuru imetamkwa na viongozi wengi kuwa kilimo ndiyo kazi ya msingi ya Watanzania walio wengi, na ni kwa kuendeleza kilimo kwa dhati ndiyo itawezekana kuongeza pato la Watanzania wengi na kupunguza kasi ya kuhamia mijini.


 Lakini changamoto za kuleta mabadiliko chanya vijijini yatakayofanya watu wabaki huko ni kubwa, kama nilivyoainisha awali kwenye makala hii. Ni changamoto ambazo Serikali inapaswa kuzitafutia ufumbuzi.
 Lakini kuna mtazamo wa fikra ambao yapaswa kuutafakari. Wapo wasomi wengi ambao wameng’ang’ania mijini lakini wana taaluma na kazi ambazo zinawaruhusu kuishi vijijini na kuweza kuendelea kufaidika na elimu yao, pamoja na kuleta mawazo chanya kwa wale ambao wamebaki vijijini na hawakupata fursa za kupata elimu nzuri.


 Mimi naamini kuwa kuna baadhi ya maendeleo yanaletwa na kuwapo kwa mawazo mapya ya mtu mmoja mmoja, pamoja na kuwapo kwa mipango ambayo Serikali inaweka. Kama wale wenye elimu na uwezo wa kuchambua changamoto za wanaoishi vijijini watabaki mijini, mikakati ya maendeleo siku zote itasisitiza barabara za juu, treni za mijini, na boti za Bagamoyo mpaka bandarini ya Dar.
 Matokeo yake wale wa vijijini watakuwa wanatembelea Dar na kubaki kushangaa tu.

By Jamhuri