Mke asiye wa ndoa, mtoto wa nje hawarithi kisheria

Kumekuwa na utata mkubwa kuhusu urithi wa mali za marehemu hasa inapotokea hayati alikuwa na mke zaidi ya mmoja na hapohapo watoto wanaotokana na mama tofauti.
Tumeshuhudia ugomvi mkubwa misibani, pia tunaendelea kushuhudia utitiri wa mashauri kuhusu mkanganyiko wa mali za marehemu ambaye familia yake ni ya watoto wanaotokana na mama tofauti.
Kutokana na hayo kuna umuhimu mkubwa wa kueleza sheria inasemaje kuhusu mazingira ya namna hiyo, ili anayeamua kuchukua hatua au kulalamika alalamikie kitu ambacho ni haki yake kweli, na anayeamua kuacha aache akiwa ameridhika kuwa hajaonewa isipokuwa hicho alichopata ndiyo haki yake kisheria.
Mke asiye na ndoa harithi
Kwa mujibu wa sheria zetu hapa Tanzania zikiwamo tafsiri mbalimbali za sheria hizo ambazo hutolewa na Mahakama Kuu pamoja na Mahakama ya Rufaa, mke wa wa nje ya ndoa hutambulika kama kimada.
Neno ‘kimada’ si tusi isipokuwa ni neno la kitaalamu linalomwakilisha mwanamke anayeishi na mwanaume bila ndoa na ndiyo maana neno hili limetumiwa na Mahakama katika hukumu zake mbalimbali.
 Kutokana na hilo, ieleweke wazi kuwa mwanamke asiye wa ndoa hata kama anaishi na mwanaume kwa mtindo ambao ukiungalia utadhani ni “mke na mume”, bado ikitokea mwanaume huyo kufa mwanamke wa namna hiyo hawezi kudai  chochote katika mali za yule mwanaume.
 Mke halali ni mke ambaye uhusiano wake na mwanaume umetokana na ndoa halali. Nje ya ndoa halali hakuna urithi. Hii isimfanye mtu yeyote ajisikie vibaya isipokuwa kinachotakiwa ni kuhalalisha uhusiano ili ndoa halali ipatikane.
Kadhalika, ieleweke kuwa wakati ambao siyo wa kifo, kwa mfano, wakati wa kuachana baina ya mke na mume ambao wameishi kama wanandoa, lakini wakiwa hawana ndoa, mwanamke asiye wa ndoa ana haki ya kupata mgawo wa mali.
Na hii ni ikiwa wameishi wote kwa zaidi ya miaka miwili kama mke na mume na ikiwa kuna mali waliyochuma kwa pamoja. Kwa maana hiyo, kwa mazingira ya kuachana ya kawaida mwanamke asiye na ndoa anaweza kudai mali, lakini baada ya kifo hawezi kudai mali.
Mtoto wan je ya ndoa harithi


Hapo juu nimetaja aina za ndoa ambazo hutambuliwa na sheria zetu hapa nchini. Nikasema kwamba watoto waliotoka nje ya ndoa hizo ndiyo watoto wa nje ya ndoa.
Ni watoto hao hao ambao hawaruhusiwi kurithi. Katika kutafsiri sheria hii Mahakama nyingine zimekwenda mbali kwa kusema kuwa mtoto wa nje ya ndoa haingii katika tafsiri ya neno ‘mtoto’ lililo katika sheria ya ndoa.

 

Mtoto wa nje ya ndoa hurithi iwapo kuna wosia
Maelezo niliyotoa hapo juu kuhusu mtoto wa nje ya ndoa kutokurithi yanahusu pale tu marehemu anapokuwa hajaacha wosia.


 Kawaida marehemu anapokuwa  hajaacha wosia, familia ya marehemu au ndugu ndiyo hushughulika na kugawana mali za hayati na ndipo hapo mtoto wa nje ya ndoa hatakuwa na nafasi ya  kurithi.
Lakini iwapo kuna wosia na marehemu amemtaja mtoto wa nje ya ndoa kama mrithi, basi atapewa hiyo mali aliyoamrishwa aipate katika wosia. Hii ndiyo sababu kubwa ya kuhimiza watu kuandika wosia ili kuondoa utata wa vitu kama hivi.

 

Ushauri wa kumsaidia mtoto wa nje ya ndoa
Kama unataka mtoto wako uliyempata nje ya ndoa asipate taabu baada ya kufa kwako, basi andika wosia naye umpe chake. Nje ya wosia mtoto wako hatapata kitu na wewe waweza kuwa sababu ya kumfanya mwanao kuwa mtoto wa mitaani (chokoraa) kwa kukosa msingi wa kipato.
Nimesema hapo juu kuwa sheria haina shida kama mtoto wa nje ya ndoa amepewa mgawo katika wosia. Lakini nje ya wosia sheria inamzuia kupata mali.
Mwandishi wa makala hii ni mwanasheria, pia tembelea: sheriayakub.blogspot.com usome ushauri wa sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa na kadhalika.