*Mkutano Mkuu wa Kata Oloipir watoa tamko

*Dk. Mary Nagu aandikiwa waraka maalumu

Migogoro mingi katika vijiji vya Tarafa ya Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha inadaiwa kusababishwa na mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na raia wa Kenya. Diwani wa Kata ya Oloipir, William Alais, amemwandikia barua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk. Dk. Mary Nagu, akieleza chanzo cha migogoro katika Tarafa hiyo, hususan vijiji katika Kata ya Oloipiri, na suluhisho la kuwapo amani ya kudumu.

 

Mpendwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji  na Uwezeshaji

Salaam,

Kama wawakilishi wa jamii tunafahamu majukumu mengi uliyonayo mbele yako, lakini ulichukua dhamana ya kukubali na kutaka kufahamu undani wa changamoto ambazo tunakabiliana nazo katika Kata yetu ya Oloipir.

Tunachukua nafasi hii kuwakilisha maoni na mapendekezo yetu kwa Serikali kwa njia ya maandishi kama rejea ya mazungumzo tuliyofanya katika mkutano maalum wa kata yetu ya Oloipiri. Na lengo la mkutano huo lilikuwa na madhumuni ya kubainisha hali halisi ya changamoto zilizopo na jinsi ya kukabilina na changamoto hizo ili kuweza kufanya kazi za kimaendeleo na  wadau mbalimbali katika Wilaya ya Ngorongoro.

Kama wawakilishi wa jamii hii husika, tuliona ni vyema kuwatuma baadhi ya viongozi wetu wa kimila na kata kusafiri hadi Dodoma, kuja kutoa msimamo wa Kata juu ya masuala mbalimbali yaliyoletwa kwako na watu waliojitokeza kwa madai ya kuwa ni wawakilishi wa kata.

Ili kufahamu ukweli juu ya kata yetu, basi ni wajibu wetu kukupa histroia fupi ya kuundwa kwa Kata yetu ya Oloipiri. Kabla ya kufanya hivyo, ni lazima tuweke bayana kuwa, ujumbe uliotangulia kukuona hawakuwa wawakilishi rasmi wa jamii na haswa Kata ya Oloipiri. Kwa kuwa Diwani aliyeongozana na hao wajumbe ni Diwani wa Kata ya Soitsambu akiongozana na wenyeviti wa Mondorosi na Soitsambu. Kwa kukusaidia kuona ni jinsi gani wahusika hao si wawakilishi wa Kata yetu, basi rejea historia fupi hapa chini ya uundwaji wa Kata ya Oloipiri.

Historia ya Kata ya Oloipiri

Kata Oloipiri ni kata changa iliyozaliwa na Kata ya Soitsambu, baada ya kata hiyo ya Soitsambu kugawanywa na kuwa kata zifuatazo; Soitsambu, Oloipiri, na Ololosokwan. Mwanzoni Kata ya Soitsambu ilikuwa na vijiji vya Soitsambu, Oloipiri na Ololosokwan na baadaye vijiji hivi kupandishwa hadhi na kuwa kata zinazojitegemea.

Baada ya Kata ya Oloipiri kupewa hadhi ya kuwa kata, iliunda vijiji vya Oloipiri, Orkuyene na Sukenya. Hapo zamani Kijiji cha Sukenya kilichokuwa ni kitongoji katika kijiji mama cha Soitsambu, kilipewa hadhi ya kuwa kijiji kamili na kuwekwa ndani ya Kata ya Oloipiri, na hivyo kufanya Kata ya Oloipiri kuwa na vijiji vitatu- Oloipir, Orkuyene na Sukenya. Baada ya maelezo ya historia fupi ya Kata ya Oloipir, basi ni vyema tukakupa historia fupi ya shamba namba 373 la Sukenya, lililopo ndani ya Kijiji cha Sukenya.

Historia Fupi ya Shamba la Sukenya

Shamba la Sukenya lipo katika Kijiji cha Sukenya ndani ya Kata ya Oloipir. Shamba la Sukenya ambalo lipo katika Kijiji cha Sukenya ni shamba lenye ukubwa wa ekari 12,600. Mwaka 1984, wakati Kijiji cha Sukenya kikiwa ni kitongoji chini ya Kijiji cha Soitsambu, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro iliombwa kutoa eneo lolote katika Tarafa ya Loliondo kwa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa ajili ya kilimo cha shairi. Hivyo basi, Kijiji cha Soitsambu kilitoa mapendekezo kuwa eneo la Sukenya ndilo eneo stahili katika kilimo cha shairi.

Kipindi hicho Kampuni ya TBL ilikuwa ni shirika la umma, na hivyo basi kijiji kilitoa shamba hilo kwa nia ya kuendeleza shirika hilo la kiserikali. Wakati kijiji kikitoa dhamana hiyo, shamba lilikisiwa kuwa na ekari 10,000 na ndizo ambazo kijiji kiliridhia kutoa, lakini baada ya shamba hilo kupimwa ilibainika lilikuwa na ekari 2,600 zaidi na hivyo kufanya shamba kuwa na ekari 12,600.

Katika kipindi cha mwaka 1987 Kitongoji cha Sukenya kilitoa malalamiko kwa uongozi wa Kijiji cha Soitsambu, kwa kutoa ardhi  yake kwa  halmashauri na hatimaye kwa TBL bila ridhaa yao. Jamii ya Laitayok ambao kwa kipindi hicho chote walikuwa ni wachache ikilinganishwa na koo za Purko na Loita katika uwakilishi wa uongozi wa Kijiji cha Soitsambu, waliona kuwa ilikuwa ni njama ya Purko kumilikisha shamba hilo la jamii yao bila ridhaa yao.

Wanajamii hao waliona ni uonevu mtupu na Purko walitumia ubabe wa kuwa wengi katika uwakilishi wa uongozi na ujumbe katika kijiji hicho cha Soitsambu. Hivyo basi, wanajamii hiyo ya Laitayok, kama Kitongoji, waliamua kuchukua uamuzi wa kufungua kesi  dhidi ya TBL mwaka 1987, lakini kesi hiyo ilitupiliwa mbali, na hivyo wanajamii hao kwa kushauriwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daniel ole Njoolay, walikubaliana na ushauri huo wa kufanya majadiliano na Serikali badala ya kukata rufaa ya kesi.

Tangu kipindi hicho jamii ya Laitayok haijawahi kurudi mahakamani kufungua kesi kwa kukata rufaa.  Sisi hatuamini katika ubaguzi wa kikoo, nia ni kutaka tu kufahamu historia ya maeneo yetu ili kusaidia Serikali kufanya uamuzi wake kwa umakini bila kupotoshwa.

Mwaka 2006, TBL ilichukua uamuzi wa kuuza mashamba yake yote yaliyo pembezoni mwa maeneo ya hifadhi za wanyamapori, kwa kuwa walikuwa wakiendesha mashamba hayo kwa hasara.  Shamba la Sukenya lilikuwa miongoni mwa mashamba ambayo TBL ilionelea kuwa ni vyema kuyauza, na hivyo basi mnamo mwaka 2006 TBL ilitangaza rasmi zabuni ya uuzwaji shamba hili kwa njia ya uwazi kupitia vyombo vya habari vya magazeti. Kampuni ya Tanzania Conservation Limited (TCL) ilishinda zabuni na kuwa mmiliki halali wa shamba namba 373.

Baada ya ushindi huo wa umiliki, kampuni ya TCL ilijitambulisha rasmi kwa  wanajamii wa eneo la Sukenya na kuahidi kushirikiana nasi kama wanajamii katika shughuli za uhifadhi na maendeleo ya jamii, na TCL imekuwa ikitimiza ahadi zake za maendeleo kwa jamii, kwa kusaidia miradi mbalimbali ya jamii ikiwemo Elimu, Afya na Maji.

Kwa bahati mbaya, kumekuwapo na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yamekuwa yakifanya uchochezi kati ya TCL na wanajamii kwa maslahi binafsi. Mashirika hayo kwa kutumia nafasi zao za kujulikana kimataifa, wamekuwa wakiwatumia jamii ya Kimasai kwa kuonyesha kuwa wananyanyaswa na kuporwa ardhi yao, ili mradi tu kutetea maslahi yao binafsi na kupotosha ukweli wa hali halisi iliyopo katika jamii zetu. Kwa mfano, mashirika haya bila kushirikisha Kata yetu ya Oloipir, walitumia nafasi yao ya kifedha, na kuwarubuni baadhi ya wenyeviti wa vijiji na madiwani ili kufungua kesi dhidi ya TCL bila ridhaa ya viongozi na wananchi  wa Oloipir wala wanavijiji wa Sukenya.

Nia yetu ni kubainisha na kuweka bayana ukweli wa hali iliyopo katika tarafa yetu, ili kuwasaidia ninyi viongozi wetu kuwa na historia itakayowapa muongozo katika kufanya uamuzi yakinifu na bila upendeleo wa upande wowote.

Mheshimiwa Waziri, sisi kama Kata, tuna nia ya kuleta amani na utulivu katika eneo la Tarafa ya Loliondo, na ndiyo maana tumeonelea ni vyema kutoa historia hii kwako na mawaziri wengine husika. Kwa kipindi kirefu, mashirika haya yasiyo ya Kiserikali yamekuwa ni kikwazo cha maendeleo ya kata za Loliondo kwa kupindisha ukweli. Lakini sisi kama Kata, tunatambua kuwa wawekezaji wote wameletwa kwa ridhaa ya Serikali, hivyo basi ni vyema kwa serikali yetu kufahamu ukweli kuwa sisi kama kata tuko tayari kusimamia ukweli na kutoa taarifa za ukweli juu ya kampuni zote zilizopo katika eneo letu. Kwa mfano, sisi kama Kata tunashirikiana vyema na kampuni ya uwindaji ya Ortello Business Company (OBC) ambayo pia imekuwa ikipigwa vita na mashirika makubwa yasiyo ya kiserikali  katika ngazi ya wilaya na mkoa.

 

Changamoto zinazoikabili Kata ya Oloipir

Mheshimiwa Waziri ni dhahiri unatambua changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiikabili Wilaya yetu ya Ngorongoro hasa Tarafa ya Loliondo, ambazo pia mkutano wetu ulibainisha rasmi na kutambua umuhimu wa kuziweka bayana kwa Wizara yako ya Uwekezaji na Uwezeshaji. Tungependa kuziroodhesha baadhi ya changamoto hizo, ambazo zimekuwa ni kikwazo kikubwa, si tu kwa maendeleo ya jamii, bali hata kusababisha hali ya ukosefu wa amani na utulivu katika Kata ya Oloipir.

1. Mgongano wa kimaslahi baina ya mashirika yasiyo ya kiserikali na wawekezaji. Katika migongano hii baadhi ya mashirika na kampuni za uwekezaji, husababisha wananchi wa kata husika kuwa katika mazingira duni. Imekuwa kawaida kwa baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali kuwarubuni baadhi ya viongozi wa vijiji na wajumbe wa vijiji ili kuchochea vurugu dhidi ya wawekezaji. Na hii imekuwa ni changamoto kuu katika Kata ya Oloipir.  Hali hii imesababisha  kubadili muonekano mzima wa Tarafa ya Loliondo na kuonekana ni tarafa yenye kupenda migogoro tu na kuwafanya wawekezaji kutokuwa na uhakika wa uwekezaji na hata kutowapa fursa ya kuwekeza kikamilifu na hatimaye vijiji vyetu kukosa fursa ya ajira na maendeleo ya jamii (Social Services).

2. Kuwapo kwa mashirika mengi yasiyo ya kiserikali na kutokuwa na msaada wowote katika kuleta maendeleo ya jamii. Kwa mfano, mashirika mengi yamekuwa yakipokea pesa nyingi kwa kutumia kigezo cha kusaidia wananchi wa jamii ya Kimasai kutetea ardhi yao, lakini ukweli wenyewe kwa kipindi cha miaka mingi idadi ya fedha wanayoipata kutoka kwa wafadhili hailingani na maendeleo katika kata zetu.

Na kwa bahati mbaya fedha hizi zinabagua katika kuleta maendeleo. Kwa mfano, shirika moja wapo liliomba kuchangishiwa pesa kwa ajili ya moja ya shule zake, ingawa katika mpango wa kazi zake kwa wafadhili waliomba na kupata Sh milioni 500 (mwaka 2011) kwa ajili ya shule hiyo. Basi sisi tunajiuliza ni kwanini Serikali kupitia vyombo vyake inashindwa kufuatilia mtiririko wa fedha hizi ambazo zimeombwa kwa ajili ya jamii zetu, lakini hazifanyi kazi iliyolengwa?

3. Mashirika yamekuwa yakitumia mitandao ya kijamii kupotosha ukweli kuhusu matatizo ya ardhi katika maeneo ya Tarafa ya Loliondo, badala ya kuzungumzia ni jinsi gani tunaweza kutumia ardhi kwa manufaa ya kiuchumi, mashirika yameamua kuonyesha dunia Wamasai wananyanyaswa ili mradi waendelee kupata ufadhili wa kufungua kesi zisizo na ukweli kama vile ile ya mwaka 2009 dhidi ya Mkuu Wilaya na OBC; na hata hii ya sasa dhidi ya TCL. Na pia wamekuwa wakipotosha Serikali na jamii ya kimataifa kuwa wawekezaji si tu wamepora ardhi ya wananchi, pia huwanyanyasa wananchi hao kwa kuwapiga, na kwa kushirikiana na Serikali kwa maana ya Polisi, wamekuwa wakiwapiga risasi wananchi bila sababu, jambo ambalo ni upotoshaji mkubwa.

4. Mashirika yamekuwa yakitumia baadhi ya viongozi wa vijiji kushawishi kufungua kesi dhidi ya kampuni. Kwa mfano, baadhi ya wenyeviti walirubuniwa na moja ya mashirika kufungua kesi dhidi ya TCL bila kupata idhini ya Mkutano Mkuu wa Kijiji husika. Walitumia ubabe kwa kuleta viongozi wa mila kama kigezo cha kumtisha Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Sukenya na baadhi ya wazee mashuhuri, kuwa wasipokubali kufungua kesi watalaaniwa. Katika kufanya hivyo, inasemekana kuwa shirika hilo liliwapa pesa viongozi hao wa mila ili kuja kufanya mkutano huu ingawa wengi wa viongozi hao wa mila hawakutoka katika maeneo ya kata.

5. Mhehimiwa Waziri, ni muhimu kufahamu kuwa sisi kama wanajamii wa Laitayok, tunaona kuwa mashirika haya yanatumia nafasi yao ya wingi kutuletea vurugu katika maeneo yetu. Kwa mfano, maeneo yote ambayo mashirika haya yanadai kuwa Wamasai wananyanyaswa, ni maeneo ambayo kuna idadi kubwa ya Laitayok na ndiyo sehemu ambazo kuna wawekezaji kama OBC na TCL. Tunaomba uchunguze kuona ukweli huu kwa kuwa mbona maeneo ya Pinini, Nguserosambu, Malambo na Ololosokwan ambao ndiyo kuna Purko wengi, wawekezaji hawapati changamoto hizi ambazo wawekezaji wengine wanazipata?

6. Ongezeko kubwa la mifugo kupita uwezo wa ardhi iliyopo. Ongezeko hili pia limechangiwa na koo mbili kubwa za Loita na Purko kuwakaribisha wenzao kutoka Kenya kuhamia katika hifadhi zetu za malisho. Hii imesababisha kuwa na uhusiano hasi na wawekezaji ambao kutokana na shughuli zao za kibiashara, hali hii ya mifugo husababisha shughuli hizo kutofanyika kwa umahiri.

7. Vijiji kutokuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi.  Hii huchangiwa na mgongano wa sheria mbili ambazo ni Sheria Na. 5 ya Vijiji ya Mwaka 1999, na Sheria ya Wanyamapori ya Mwaka 1974 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009. Sheria hizi mbili zinaleta migongano kuhusu Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1982 iliyoipa vijiji vyote vilivyoko Pori Tengefu la Loliondo vyeti vya vijiji na Sheria ya Mwaka 1974 inayotuelekeza tena kuwa ardhi yote ni Pori Tengefu.

8. Mabadiliko ya tabianchi ambayo imesababisha kuwa na ukame wa muda mrefu katika maeneo ya malisho

9. Kuongezeka kwa uwingi wa watu na kusababisha kutokuwa na mipango endelevu ya makazi na hivyo kulazimu  wanajamii kujihusisha na shughuli za kilimo na katika baadhi ya maeneo kuna uharibifu mkubwa wa misitu na vyanzo vya maji.

Mapendekezo ya Kata ya Oloipir kwa Serikali

Kutokana na malalamiko ambayo yamekuwa yakiletwa kwa Serikali na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali na hata kufikia kupotosha ukweli halisia wa changamoto zilizopo katika tarafa yetu kupitia mitandao ya kijamii, sisi kama wananchi wa Kata ya Oloipir, tungependa Serikali kutambua kuwa pamoja na changamoto zilizopo katika Kata yetu ya Oloipri, Mkutano huu maalumu unaazimia na kutambua kuwa, ili kuleta maendeleo katika jamii zetu ni wajibu wa Kata kufanya shughuli na wadau watakaowezesha kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika kata yetu. Wadau hao ni; Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wawekezaji (Responsible Investors). Hii ni kwa kutambua umuhimu wa dhana nzima ya Public-Private Partnership (PPT).  Hivyo basi sisi tunatoa mapendekezo yafuatayo:

1. Serikali ichukue jukumu la kutoa onyo na hata adhabu kali pale inapostahili kwa viongozi wa mashirika haya yasiyo ya kiserikali ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha hakuna uhusiano chanya kati ya jamii na wawekezaji. Mkutano Mkuu vilevile umeazimia Kata na vijiji vyetu kufanya kazi na wawekezaji waliopo katika kata yetu na hata wale watakaojitokeza kutaka kuwekeza katika maeneo yetu yenye rasilimali zinazoweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi. Tunaomba Serikali itusaidie kuwadhibiti wale wote watakaokuwa na madhumuni ya kuchafua kata yetu kupitia vyombo vya mitandao, maana wamekuwa wakituharibia uhusiano wetu na wawekezaji. Kwa ufupi, Kata ya Oloipir inakubali na kutambua uwepo wawekezaji na inaomba Serikali iwalinde katika kuwatetea wawekezaji wazuri waliopo.

2: Tunaishauri Serikali kupitia vyombo vyake vya dola, kufanya uchunguzi wa kina kuchunguza (audit) haya mashirika kwa kufuatilia miradi waliyoombea pesa na kulinganisha kama miradi hiyo inaendana na thamani ya pesa walizopata kutoka kwa wafadhili kama njia mojawapo  ya kuwadhibiti na kuhakikisha fedha hizo wazipatazo kutoka kwa wafadhili zinatumika kwa malengo waliyokusudia.

3: Kwa kuwa mwaka 2009, Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu iliunda kamati maalaumu kwa ajili ya kufuatilia ukweli halisi juu ya shamba la Sukenya na pia migogoro kati ya jamii za loliondo na OBC; ni vyema Serikali ingetoa tamko ya yale waliyoyabaini walipofanya uchunguzi huo ili kupata ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza kila leo.

4: Katika Ziara ambayo itahusisha mawaziri wa wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Maliasili na Utalii; Maemdeleo ya Mifugo na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, sisi kama Kata tunapendekeza na tunaona ingekuwa ni jambo la busara tena sana kwa mawaziri hao kufanya ziara ya siku tatu ili kujiridhisha juu ya ukweli wa migogoro iliyopo katika Tarafa ya Loliondo na hasa ile inayohusisha wawekezaji wa TCL (kampuni dada ya Thomson Safari) na OBC. Hivyo basi, sisi tunapendekeza kwamba mawaziri hawa wakutane na kata za Oloipir na Soitsambu kwa nyakati  tofauti, maana endapo mtaamua kukutana na kata zote kwa wakati mmoja, hamtaweza kuchanganua ukweli wa migogoro hii na italeta mabishano na kutofikiwa kwa muafaka.

5: Ili kukabiliana na tatizo la mifugo mingi kuzidi uwezo wa ardhi (Carrying Capacity), vijiji vya Kata ya Oloipir tunaiomba Serikali ichukue jukumu la kuhakiki mipaka ya vijiji ili tuweze kutengeneza mipango ya matumizi bora ya ardhi na pia kupata vyeti vya vijiji na hatimaye kudhibiti uhamiaji haramu kutoka mipaka ya nchi jirani ya Kenya na vijiji vya kata zinazotuzunguka.

6: Ipo haja kwa Serikali kuangalia migongano ya Sheria kuhusu ardhi na kurejea sheria ya wanyamapori, lakini vijiji vilazimishwe kufanya mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kulinda na kuendeleza uhifadhi wa mazingira na kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

7: Kwa muda mrefu Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikizuia wafugaji kupeleleka mifugo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Ingawa tunakubaliana na uzuizi huo kwa madhumuni ya kulinda mazingira, ila tunashauri Wizara husika, kujaribu kuruhusu wafugaji kuchunga katika eneo hilo katika kile kipindi ambacho hakuna watalii wengi wanaotembelea hifadhi na wanyama wakiwa wamehamia Masai Mara, Kenya. Badala ya kutumia utaratibu wa kuchoma nyasi mbugani (Controlled Burning), wawaruhusu wafugaji wa vijiji vilivyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kufanya malisho katika Hifadhi hiyo kuliko mifugo ife kwa kukosa malisho. Pia Mheshimiwa Waziri, utaratibu huo hufanyika kwa miezi mitatu tu ya kiangazi.  Kufanya hivi kutapunguza sana malalamiko kutoka kwa wawekezaji na pia mifugo inaweza kabisa kuchangia pato la Taifa kwa kiwango kikubwa.

Faida  kutoka wawekezaji

Mheshimiwa Waziri, ni dhahiri kwamba picha ambayo dunia imekuwa nayo juu ya Loliondo ni ile ambayo imewekwa na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, ambayo kwa kweli huweka sura hasi juu ya Tarafa na Kata yetu, lakini pia nchi kwa jumla.

Pia huu upotoshaji huenda kinyume cha jitihada za Mheshimiwa Rais za kukaribisha wawekezaji kutoka pande mbalimbali za dunia. Pia inaonyesha dunia kuwa Loliondo ni eneo hatari kwa wawekezaji. Kwa sababu hii, wawekezaji wengi wameamua kutoka katika maeneo yetu. Mfano wawekezaji waliotoka ni Nomads, Hoopoe, Buffalo n.k.

Pia kwa kuwa mashirika haya yamekuwa na nguvu sana, yamesababisha kutujengea jina baya kwa tarafa yetu.  Kwa mfano, mwaka 2010, Balozi wa Marekani alifanya ziara kwa mwekezaji wa kimarekani wa TCL, na alikuwa ametoa ahadi ya kujaribu  kuangalia ni jinsi gani kwa kushirikiana na wawekezaji wanaweza kusaidia kwenye ufugaji.

Lakini kwa kuwa mashirika haya nia yao ni kuendeleza maslahi binafsi, walimwandika vibaya Balozi wa Marekani katika mitandao ya kijamii na kusababisha balozi huyo kujitoa katika mchakato huo.

Mheshimiwa Waziri, sisi kama Kata tungependa kutoa taarifa za kimaendeleo ambazo zinafanywa na wawekezaji na si rahisi kuzipata kupitia mashirika haya yasiyo ya kiserikali. Tunaambatanisha taarifa za miradi ya maendeleo iliyofanywa na wawekezaji katika kata yetu na sehemu nyingine za wilaya ya Ngorongoro kwamba ni za kweli na tunakubali na kuthibitisha kwamba miradi hiyo imefanyika. (Tafadhali rejea Viambatanisho vya miradi kutoka kampuni ya Thomson Safaris Ltd/TCL na kutoka kampuni ya OBC)

Hivyo basi, Mkutano Mkuu Maalumu wa Kata ya Oloipir uliofanyika Novemba 10, 2014 umekubaliana kwa sauti moja kushirikiana na Serikali, wawekezaji waliopo katika ardhi ya vijiji yakiwapo OBC, TCL na wawekezaji wengine wanaohitaji kufanya uwekezaji wa kitalii, na uwekezaji mwingine wenye manufaa kwa jamii zikiwamo taasisi za kiraia na kidini; alimradi uwekezaji huo ni kwa manufaa ya jamii (vijiji) na Watanzania kwa jumla.

Mkutano Mkuu Maalumu umekubaliana kuwa matatizo yatakapojitokeza ni sharti yatatuliwe na wananchi kwenye vijiji na Kata husika na siyo watu au vikundi vingine kuyasemea au kujaribu kuyatatua kwa maslahi yao binafsi, na kama ni lazima vikundi hivyo kufanya utatuzi, basi njia shirikishi zitumike.

Mkutano Mkuu Maalumu wa Kata umekubaliana kwa sauti moja kuwa hawako tayari kutengenezewa  migogoro isiyo na tija kwa Serikali kwa ngazi zote, kwa wawekezaji na kwa wadau wote wa maendeleo kwenye jamii husika. Hivyo tunawaomba viongozi wetu wa Serikali kuhakikisha tunalindwa katika jitihada zetu za kutafuta maendeleo endelevu.

Kwa niaba ya Kata ya Oloipir, tunakushukru sana.

Wako katika kujenga Taifa,

 

William Alais

Diwani wa Kata ya Oloipiri

Wilaya ya Ngorongoro

1672 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!