*Lajipanga kuwatafutia eneo maalumu huku likiwaonya wanasiasa

ARUSHA

Na Zulfa Mfinanga

Jiji la Arusha ni maarufu nchini na duniani kote kutokana na kuwa kitovu cha utalii pamoja na mkoa mzima kuhodhi vivutio vingi vya utalii.

Sambamba na hayo, Arusha pia ndio Makao Makuu ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, Mahakama ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na Mahakama Maalumu ya Kimataifa ya Kuhitimisha Masalia ya Makosa ya Jinai (ya Rwanda).

Kuwapo kwa taasisi hizo kumesababisha mji huu kupokea wageni wengi kutoka nchi mbalimbali duniani wanaofika kufanya kazi, biashara, utalii na hata uwekezaji.

Lakini licha ya kuwa na hadhi hii, Jiji la Arusha linakosa mvuto machoni mwa wageni na hata wenyeji kutokana na uchafu wa mazingira ambao kwa kiasi kikubwa umesababishwa na uvamizi wa wafanyabiashara wadogowadogo (wamachinga) kando ya barabara na sehemu zisizo rasmi.

Uvamizi huu unatokana na kauli ya Serikali Kuu kuwaruhusu wamachinga kufanya shughuli zao bila kubughudhiwa, hivyo kusababisha kuwapo biashara holela sehemu mbalimbali za mji.

Maeneo mengi ya katikati ya Arusha yameathiriwa na wafanyabiashara wadogo, yakiwamo maegesho ya magari na barabara za watembea kwa miguu, hivyo kuwapa wakati mgumu watumiaji wengine wa barabara wakiwa katika shughuli zao.

Hali hii pia imekuwa ikihatarisha maisha ya watembea kwa miguu wanaopata taabu kupishana na vyombo vya moto; huku vyombo hivyo, hasa bodaboda zikiwa katika hatari ya kugonga au kugongana kutokana na msongamano uliopo barabarani.

Wafanyabiashara wenye maduka maeneo la Kariakoo jirani na Stendi Kuu ya mabasi yaendayo mikoani, Soko Kuu na barabara za katikati ya jiji wanasema wamachinga wamevamia maeneo mengi ya mji hadi milangoni mwa maduka yao na kupunguza idadi ya wateja wanaoingia madukani.

“Unakuta bidhaa za wamachinga zimepangwa nje ya duka lako. Mteja akitaka kuingia dukani anaona kero au pengine hakuna njia kabisa! Hata kama ni kutafuta riziki, si kwa mpangalio mbovu namna hii,” anasema Anna Mushi, mfanyabiashara wa Soko Kuu.

Lakini ipo kauli (au dhana) inayoleta mkanganyiko kwa kiasi fulani, ikidaiwa kuwa ni wafanyabiashara hao wenye maduka makubwa ndio chanzo cha kuwapo wamachinga.

Kwamba wafanyabiashara wakubwa huwapa bidhaa waziuze barabarani nje ya maduka yao ili maeneo hayo yasivamiwe na wamachinga ‘orijino’.

“Hao unaowaona mbele ya maduka usidhani ni wamachinga, wenye mali hizo ni wenye maduka ya nyuma, wanafanya hivi kulinda biashara zao kwani wakiacha tu nafasi, watu wengine watakuja kuweka bidhaa mbele ya maduka na wao kukosa wateja,” anasema Madii Hussein, mfanyabiashara mdogo na kuongeza:

“Kwa hiyo kusema ukweli hawa si wamachinga, machinga halisi ni sisi tunaotembeza bidhaa mitaani. Na kwa mtindo huu serikali inakosa kodi kubwa sana kwa sababu hao vijana wanatumia vitambulisho vya wamachinga wakati si wamachinga. Wao wanalipwa na wenye maduka.”

Wenye maduka ya bidhaa za watalii nao wanalalamikia utaratibu uliopo.

“Nina duka la bidhaa za watalii, lakini kwa msongamano uliopo, watalii wanashindwa kuingia kwa kuhofia kukosa maegesho ya magari yao. Inabidi kuwatumia bidhaa zetu kwa njia ya simu, wakishachagua ninawapelekea waliko. Hili linanikosesha uhuru wa kufanya biashara,” anasema Jacob Bazil, mfanyabiashara wa Barabara ya Uhuru.

Malalamiko mengine yanatoka kwa watembea kwa miguu wakidai kadhia iliyopo mjini Arusha inawapa wakati mgumu, kwani hata barabara maalumu za watembea kwa miguu nazo zinatumiwa na wamachinga!

“Sasa tunalazimika kutumia barabara za magari kwa sababu za watembea kwa miguu zimejaa bidhaa za wamachinga. Huu utaratibu wa kuwaruhusu wafanye biashara kiholela umeleta shida sana. Mtu ukiwaza kuja mjini, unaanza kufikiria kupishana na pikipiki, magari na watu! Unakata tamaa,” anasema mzee Sajilu.

Wamachinga wenyewe wanasemaje?

Kwa upande mwingine, wamachinga wamesema wataendelea kufanya biashara katika maeneo hayo kama serikali ilivyotamka kuwa wasibughudhiwe.

“Kinachotakiwa siyo sisi kuondolewa, kwani waliotuleta waliziona changamoto zote hizi. Cha msingi ni serikali ione jinsi gani kila kundi litafanya shughuli zake kwa amani na si kuwaondoa wengine na wengine wabaki. Haya maeneo (mjini) ndiyo yenye wateja wengi, kwa hiyo kila mtu anayatamani,” anasema Abuu Kachonjo, mfanyabiashara wa eneo la Idara ya Maji.

Majuzi, Baraza Maalumu la Madiwani Jiji la Arusha limejadili changamoto za biashara holela katika jiji hilo na kusema wimbi la wamachinga linatokana na sababu kadhaa, ikiwamo baadhi yao kuacha meza (vizimba) kwenye masoko na kuhamia barabarani.

Pia wengine wameyauza maeneo waliyokuwa wakiyatumia na kuhamia barabarani kisha kudai hawana maeneo ya kufanyia biashara.

Sababu nyingine ni baadhi yao kufunga maduka/vyumba na kujiondoa kwenye mfumo rasmi wa ulipaji kodi, kisha kupanga bidhaa barabarani, hali inayopunguza mapato ya halmashauri.

Ili kutatua changamoto hii, menejimenti ya Halmashauri ya Jiji katika kikao chake cha Mei 24, 2021 pamoja na kile cha Kamati ya Fedha na Mipango cha Mei 26, 2021, wameandaa mikakati kabambe.

Akisoma mapendekezo ya kamati hiyo kwa wajumbe wa Baraza Maalumu la Madiwani, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk. John Pima, anasema kuna ya muda mrefu na ya muda mfupi.

“Hadi Julai mosi mwaka huu, yale ya muda mfupi yatakuwa yameshafikiwa. Mikakati ya muda mfupi ni kuwasajili wamachinga. Usajili huo utazingatia sifa, kutafuta maeneo kwa ajili yao kufanyia biashara, kuwapanga wamachinga katika maeneo yaliyobainishwa pamoja na kuwaondoa wafanyabiashara wote ambao si wamachinga, lakini wanapanga biashara barabarani,” anasema Dk. Pima.

Amesema wajumbe wameainisha mikakati ya muda mrefu katika kutatua changamoto hiyo kuwa ni kujenga jengo la ‘Machinga Complex’ katika eneo la Bondeni City, kusanifu na kujenga soko la NMC kwa ajili ya wamachinga, kujenga jengo la wamachinga eneo la CCM (Azimio) Kata ya Elerai, kupanua na kuboresha masoko katika kata zote.

Pia Dk. Pima amewaambia wajumbe wa baraza hilo kuwa kikao kimekuja na mpango kazi wa utekelezaji ambapo wataalamu watatoa elimu kwa wamachinga na elimu hiyo itajikita katika kuelezea mmachinga ni nani, utaratibu wa utoaji wa vitambulisho vya wamachinga na kuwafahamisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao.

Mpango kazi mwingine ni kuwatoa wafanyabiashara barabarani na maeneo ya watembea kwa miguu wale ambao si wamachinga na kuwarudisha kwenye masoko na meza; kuwapanga wamachinga katika maeneo yaliyoainishwa pamoja na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara huku kila hatua ikiwa na ukomo wa muda wa utekelezaji.

Jiji la Arusha likiongozwa na Meya wake, Maximilian Iranghe, linaendelea kufanya usafi wa mazingira kila Jumamosi ambapo watu zaidi ya 1,000 hujitokeza. 

“Tunapaswa kuibadilisha Arusha bila kuathiri mazingira, wafanyabiashara na wamachinga. Na sisi wanasiasa tuwaonee huruma wapiga kura wetu wakiwamo wamachinga, kwa sababu hata ukiangalia maeneo wanayofanyia biashara zao, ni hatarishi! Bila kuwaambia ukweli, hatuwasaidii,” anasema meya.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Idd Kimanta, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, amewahakikishia wakazi wa Arusha kuwa suala la usafi wa mazingira na mwonekano mzuri wa mji ni kipaumbele chake cha kwanza.

Amesema atafuata utaratibu wa mazungumzo ili kujua wafanyabiashara hao wanataka nini na upande wa serikali utawaambia unataka nini ili kwa pamoja wafikie muafaka wenye tija hata kama kuna upande mmoja kati yao utapoteza au kupata kitu.

“Hata wakati nikiwa mkuu wa wilaya hapa, hali ilikuwa mbaya zaidi ya ilivyo sasa. Tulikaa nao kujadiliana na tukaelewana, tukawapeleka kule Samunge. Ikumbukwe kule Samunge lilikuwa eneo la wazi, na hata sasa hatutatumia nguvu, tutatumia njia ya majadiliano na tutaelewana tu,” anasema Mongella.

By Jamhuri