Wakati Serikali ikiendelea na kazi ya kuvifunga vituo vya kuuza mafuta nchini, Chama cha Wamiliki wa Vituo vya Mafuta (TAPSOA) kimebainisha sababu za kutoanza kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti kwenye pampu (Electrical Fiscal Petrol Printers-EFPPs).
Katibu Mkuu wa TAPSOA, Tino Mmasi, ameliambia JAMHURI, wanashangazwa na hatua zinazochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Serikali kwa ujumla kuvifunga vituo vya matufa ambavyo havitumii EFPPs.
Amesema wanashangaa kwa sababu Mei 2014, baada ya Serikali kutoa agizo la kutaka wafanyabiashara wote nchini kuanza kutumia mashine hizo, walikutana na uongozi wa TAPSOA na TRA kujadili suala hilo ili kuangalia namna ya kushughulikia changamoto katika sekta ya mafuta kwa manufaa ya pande zote mbili.
Katika mazungumzo hayo ambayo yalimshirikisha pia Kamishna wa TRA, walikubaliana kuunda kamati ya wajumbe watano kutoka TRA na TAPSOA kwenda nchini Uturuki kupata mafunzo na semina juu ya namna ya kuingia katika mfumo wa kutumia mashine za EFPPs.

Katibu huyo amesema baada ya safari hiyo timu hiyo kwa pamoja iliandaa ripoti ya pamoja iliyoainisha changamoto mbalimbali na mapendekezo ya nini kifanyike ili kuweza kukabiliana nazo.
Mmasi amesema katika ripoti hiyo, kamati ilibainisha changamoto zinazotakiwa kutafutiwa ufumbuzi na TRA kabla ya kuendelea na kazi ya kufunga EFPPs kwenye vituo vya mafuta kwa manufaa ya pande zote ambazo hadi leo hazijafanyiwa kazi na mamlaka husika.
Katibu huyo amesema baadhi ya changamoto walizoziainisha katika ripoti yao ni pamoja na kuwapo kwa tatizo la mtandao (network) ambalo limekuwa sugu TRA na hivyo kusababisha mashine za EFPPs kushindwa kufanya kazi kwa usahihi.

“Kwa mfano, kuanzia Jumatatu ya Julai 10, 2017 kulikuwapo na tatizo la network TRA na mafundi walihangaika kwa muda mrefu kushughulikia tatizo hilo.”
Changamoto nyingine zilizoainishwa na wadau wa mafuta ni kuwapo kwa gharama ambapo bei na faida katika biashara ya mafuta kupangwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Amesema kabla ya TRA kuchukua uamuzi wa kuanza kuvifunga vituo ambavyo havitumii mashine hizo, ingeanza kushughulikia changamoto zilizoainishwa na wadau wa mafuta nchini miaka miwili iliyopita.
Anasema biashara ya mafuta ina changamoto nyingi ambapo faida ya mauzo ya mafuta ya rejareja ni takribani asilimia 2 kabla ya kutoa utitiri wa tozo mbalimbali katika vituo vya mafuta.
Tozo hizo ni pamoja na mishahara, umeme, maji, benki (bank charges), kodi za majengo, ushuru wa huduma na  Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA).

Mmasi anasema kimsingi TAPSOA na wanachama wake wapo tayari kufunga mashine za EFPPs lakini wana wasiwasi kama zipo za kutosha kuweza kufunga kwenye vituo vyote 1,600 vilivyopo nchi nzima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo, amesema wakati Serikali inatoa agizo la kuhakikisha vituo vinafunga mashine za EFPP kwenye pampu za mafuta kulikuwa na changamoto za gharama ambapo mashine moja ya EFPP ilikuwa inauzwa kwa dola za Marekani 3,500 na baadaye dola 2,500.
Amesema kwa hali hiyo mtu ambaye alikuwa na mashine nne alitakiwa kulipia dola za Marekani 10,000, jambo ambalo lilikuwa gumu kutekelezwa.
Kayombo alipoulizwa kuhusu makubaliano kati ya TRA na TAPSOA, amesema kwa sasa uamuzi uliofikiwa na Serikali ni kuhakikisha kila mfanyabiashara anakuwa na mashine za EFPP kwa manufaa ya Watanzania.
“Kwa sasa muda wa majadiliano haupo, kinachotakiwa ni kwa kila mfanyabiashara awe na EFPP ili Serikali ipate kodi kwa maendeleo ya nchi,” amesema.

Kayombo amesema tatizo lililopo kwa Watanzania wengi ni kutokuwa na utamaduni wa kulipa kodi na hii imekuwa ni changamoto kubwa tunayohangaika nayo kwa miaka mingi.
Amesema TRA ikiwa miongoni mwa taasisi za umma ilianzisha mkataba wa mlipakodi ili kuweka bayana haki, wajibu na viwango vya huduma vinavyotarajiwa na Mamlaka hiyo.
Amesema dira ya TRA ni kuongeza mapato ya ndani kwa kuimarisha ulipaji wa kodi kwa hiari, kwa lengo la kuongeza mchango wa mapato ya ndani kufikia asilimia 70 ifikapo mwaka 2018.
“Vituo vyote vilivyofungiwa vitafunguliwa iwapo watakidhi vigezo ambavyo ni pamoja na kulipia mashine na kuingia makubaliano na TRA ni muda gani mafundi watakuwa wamefunga mashine hizo,” amesema Kayombo.
Amesema katika utafiti uliofanywa na TRA imebainika kuwa kati ya watu 10 wanaojaza mafuta, ni wawili tu ndiyo waliokuwa wanapewa risiti hizo, tena kwa kuzidai; mwanya uliokuwa ukitumiwa na wamiliki wa vituo vya mafuta kukwepa kodi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango, mwaka jana aliongeza muda kwa wamiliki wa vituo vya mafuta kuanzia Julai 16 hadi Septemba 16, 2016 wawe wamefunga mashine hizo kwenye pampu za mafuta.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wakala wa Serikali wa Uagizaji wa Mafuta nchini (PBPA), Kedron Mbwilo, amesema majukumu ya taasisi yao huishia bandarini pale mafuta yanapokuwa yameshafika nchini bandarini.
“Suala la kufunga EFPPs linaweza kuwa na changamoto zake lakini ni suala lenye faida kubwa kwa mfanyabiashara yeyote anayehitaji kuendesha biashara zake kitaalamu,” amesema Mbwilo.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo, alipoulizwa juu ya malalamiko ya TAPSOA, amesema wao hawahusiki na zoezi hilo linaloendelea nchini la kufungia vituo vya mafuta.
Tamko la Rais

Kwa kuweka msisitizo, Rais John Magufuli ametoa siku 14 kwa wamiliki wa vituo vya mafuta kote nchini kutumia mashine za EFPP na watakaoshindwa wafutiwe leseni zao.
Agizo hilo amelitoa wakati wa ufunguzi wa barabara ya Kigoma-Biharamulo-Lusahunga yenye urefu wa kilometa 154 huku akiwataka mawaziri wenye dhamana kuhakikisha wanafuatilia maagizo hayo kuanzia sasa.

1396 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!