Wapinzani wachekelea Pinda kugwaya

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeeleza kufarijika na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba kampuni ya Agrisol haijapewa ardhi ya Katumba na Mishamo mkoani Katavi.

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, alitoa msimamo huo wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi hiyo ya makadirio ya matumizi ya mwaka wa fedha wa 2012/2013, bungeni jana. Wakati wa Hotuba ya Waziri Mkuu, Mdee alimtaja kuwa ni mmoja wa washiriki wakuu wa kutoa ekari zaidi ya laki saba kwa wawekezaji wageni kinyume cha sheria.

“Wakati akihitimisha hotuba yake ya bajeti, pamoja na mambo mengine, (Waziri Mkuu) alitamka kwamba mchakato wa Agrisol haujaanza, hawajaingia makubaliano/mkataba  ‘wowote’ na kwamba mchakato ukianza ndipo wataingia kwenye mambo ya msingi waone wanapangiana vipi, uwiano utakuwaje na kwamba halmashauri imiliki kiasi gani cha hisa!

“Rai ya Kambi ya Upinzani ni kwa serikali kusitisha mpango wake wa kuligawa eneo la Mishamo na Katumba lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 325,000 au ekari 760,728 kwa Agrisol. Kuna taarifa kwamba tayari serikali ilishaligawa eneo la Lugufu lenye ukubwa wa hekta 10,000 kwa Agrisol (kwa kuwa mikataba  inaendeshwa kwa usiri mkubwa.) Ni imani yangu  Serikali itatupa jibu juu ya mustakabali wa Lugufu.

“Wakati serikali ikitafakari, ni muhimu Bunge hili tukufu likaelewa kwamba aliyekuwa mshirika muhimu wa Agrisol, Iowa State University College of Agriculture aliyekuwa mhimili muhimu wa mwekezaji huyu hasa katika kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kama ilivyoainishwa katika kipengele cha  4.7 cha MoU  baina Halmashauri ya  Wilaya ya Mpanda  na Agrisol  Energy Tanzania Limited, alijitoa baada ya kugundua kwamba mwekezaji huyu hana dhamira ya kuisaidia nchi na wakulima wadogo zaidi ya kujinufaisha kibiashara.

“Kwa maelezo ya Iowa State University College of Agriculture, ilijitoa baada ya kugundua ilitumiwa na mmiliki wa Agrisol, Bruce Rastetter ili aweze kupata uhalali wa kukubalika kirahisi kama mwekezaji mahiri! Ukweli ni kwamba nia ya mwekezaji huyu haikuwa kuisaidia nchi, bali kuendeleza mashamba makubwa ya zao mojamoja, matumizi ya viwango vikubwa vya kemikali na pia kuomba mabadiliko katika kanuni za kitaifa za usalama wa kibaiolojia ili mazao yenye viinitete (GMO) yaweze kupandwa.

“Madhara ya GMO ni makubwa sana , moja kubwa ni kufifisha kabisa matumizi ya mbegu za asili. Mwekezaji akizitumia kwenye eneo lake, madhara yanasambaa pia kwa mashamba ya jirani, inajenga utegemezi wa wakulima kununua mbegu kutoka kwa wakulima wakubwa.

Mbali na utegemezi wa mbegu, GMO zina madhara makubwa sana kiafya. Tafiti zimeonyesha kwamba nchi zilizoendelea ziko katika vita kali sana za kuzuia matumizi ya GMO, lakini sisi tunapokea kampuni kubwa kwa misamaha lukuki ya kodi, tukiamini tunaalika wawekezaji waje kuijenga nchi, kumbe wanakuja kutengeneza taifa la utegemezi na lenye maradhi lukuki.

“Ni muhimu ikaeleweka kwamba katika Wilaya ya Mpanda ardhi ambayo iko wazi kwa matumizi ya binadamu ni asilimia 19 tu ya eneo lote. Nyingine iliyobaki ni hifadhi za taifa; asilimia 18 hifadhi ya wanyama; asilimia 59 hifadhi ya misitu  na asilimia nne ni hifadhi ya maji.

“Badala ya kila kitu kuwategemea mabeberu, inawezekana kabisa serikali ikawekeza katika eneo husika. Taarifa zinaonyesha kwamba Agrisol walitarajia kuwekeza dola milioni 100 (Sh bilioni 150) katika kipindi cha miaka 10, kwa matarajio ya kupata faida ya dola milioni 272 (Sh bilioni 408) ndani ya mwaka mmoja baada ya uwekezaji huo kwa kulima hekta 200,000 tu za mahindi, kiasi ambacho  kinalingana kama sio kuzidi bajeti ya Wizara ya Kilimo!

“Kama Agrisol wangepata/watapata hadhi  ya mwekezaji wa kimkakati (stratergic investor), wangepata/watapata pia msamaha wa kodi ya shirika (corporate tax)  ambayo ni asilimia 30 ya Sh bilioni 408 (ambayo ni Sh bilioni 122)!

Hivi kweli serikali makini, mbali ya kuwa na vivutio vya utalii vilivyosheheni, na hivyo kuwa nchi ya nne ya uzalishaji wa dhahabu Afrika, nchi pekee yenye madini tofauti tofauti zaidi ya 15 na kwa upekee ni madini ya Tanzanite, tuna urani ya kutosha, hivi karibuni tumegundua gesi yenye thamani ya Sh trilioni 626.7, tuna tani milioni 86 za makaa ya mawe, tuna kila dalili ya kupata mafuta n.k, inashindwa kuwekeza kwa faida ya nchi na wananchi wake? Tunawezaje kuokoa kizazi cha vijana waliogeuka wazururaji kwa sababu serikali yao haijawapa fursa?”