Watanzania sasa tukatae kutawaliwa

Minyukano ya kutafuta uongozi nchini tayari imeshaanza. Tumeshuhudia ya kushuhudiwa, mitandao nayo ipo kazini usiku na mchana. Inashangaza kuona harakati za kutaka kuwatawala Watanzania ambao dalili zinaonesha kuanza kupevuka uelewa, zimeanza kujidhihirisha.

Wanaotaka utawala wamejisahaulisha ahadi zao na matatizo ya wapiga kura, badala yake wameanza kuelekeza nguvu kubwa kwenye sakata la udanganyifu kwa wadanganyika, kwa kutumia vijisenti na vijizawadi visivyo na tija kwa mustakabali wa maisha ya Watanzania.

Harakati hizi za kusaka utawala kwa watawaliwa zimegawanyika katika kila aina ya utawala. Hii ni kutokana na aina ya watawala waliojitanabahisha kwa watawaliwa.

Jambo kubwa linalochefua ubongo ni kiu yao kubwa ya kutaka na wala si kuongoza. Nia yao kubwa ni kujitengenezea ulaji kama tulivyoona. Katu hawana kiu ya kumkomboa Mtanzania, bali wao na familia-koo.

Kutokana na ufikiri wao kuwa mdogo, hawana nia ya kuongoza zaidi ya kutawala, wamekuwa wakitoa matamshi yasiyo na mashiko kwa jamii.

Kutokana na kuishi maisha ya kuvuta milungula kila uchao kutokana na kodi zetu, fikra zao zote wamezielekeza kwenye kuhongana tu. Hizi ni fikra na bongo za watawala wetu. Wamelewa madaraka, wameamua kujitanabahisha kuwa wao ndiyo bora zaidi yetu kutokana na kulewa madaraka.

Wamejiaminisha ya kuwa wao ndiyo wenye hatimiliki ya kututawala kutokana na utumwa tuliojitengenezea. Watakapoona kuwa sasa wamechoka hututafutia watu wa kuwarithi ili utawala wao uweze kuendelea.

Kutokana na uwendawazimu wa utawala, wamewaaminisha maswahiba zao kuwa wataendelea kututawala, hivyo maswahiba hao wanawasaidia kuhakikisha wanawaingiza madarakani ilivyozoeleka. Watawala wengi waliojitokeza hivi karibuni bila hata kuangalia uwezo wao, wameelezwa kuwa wanafaa kututawala huku watawaliwa wakipuuzwa na kukejeliwa.

Kutokana na historia, miongo kadhaa iliyopita ilikuwa vigumu na halikuwa jambo rahisi kuona mtu akipewa fursa ya kuongoza, lakini nyakati hizi hao ndiyo wenye nafasi kubwa ya kutuongoza. Kila nikifikiria nini kimetufikisha hapa nakosa majibu.

Ajabu, nyakati hizi kila mtu akilala na kuamka anajiona ni mtawala, hata kama ameshindwa kuiongoza kaya yake binafsi, bila kujipima anakurupuka kutoka huko alikokurupushwa hata kama ni usingizini anaanza kutaka kutuongoza.

Haikuwahi kuwa rahisi kwa mtu kuchaguliwa kuwaongoza watu kutokana na uwezo wa fedha, kuimba, kuigiza, kucheza ngoma au hata uhodari wa kuongea. Hivi havikutosha kuwa sifa ya kuwa kiongozi hata kama ni mjumbe wa nyumba kumi.

Bila kuwa makini, uamuzi wa kuwapatia watu madaraka utatulazimu kuishi maisha ya majuto maana tutalazimika kusubiri miaka mingine mitano. Tutaishi kwa majuto na kuweweseka kusikokoma katika kipindi chote hicho.

Kukosekana kwa miiko na sifa za uongozi ndiko kulikotufikisha hapa tulipo. Wale tunaowatarajia kutusemea ndiyo waliokengeuka, wanatutusi na kujivuna huku wakitukebehi kila siku. Kutokana na kukosa miiko na sifa za uongozi basi tumekuwa tukiishia kuwapata watawala na si viongozi.

Kiongozi yeyote wa kweli anazo sifa za uongozi ambazo zipo kuanzia kwenye mtiririko wa damu yake tangu utotoni kama ilivyo kwa baadhi ya watu hapa nchini. Kamwe uongozi hauji tu kama mate kinywani, ukiamua kutema unatema tu na ukiamua kumeza unameza bila hata kufikiri.

Ni lazima kutambua kuwa hamu ya mtawala siku zote ni kutaka kujinufaisha. Kwa kuwa wameshagundua kuwa kwenye utawala kuna masurufu ya kutosha yenye uwezo wa kuwanufaisha kwa haraka.

Kutokana na kupenda kutawala wanasaka mianya inayowawezesha kupenya kwenye maeneo ya kuteuliwa bila hata kujali weledi. Wepesi wa kuchochea mambo yasiyo na maana ambayo siku zote huamsha hasira na chuki kwa umma.

Kama wamepata hamu ya kutuongoza ni vyema kuhakikisha tunalitambua hilo mapema ili kuepuka makosa. Tukumbuke ya kuwa hawatakuwa na msaada kwetu zaidi ya kuwa wepesi wa kuanzisha mambo yasiyo na maana katika maeneo yetu.

Kipindi kilichosalia kuelekea Uchaguzi Mkuu ni kifupi mno, iwapo hatutakuwa makini na halmashauri zetu za kichwa tutajikuta tumepigwa kumbo na kubakia kuishi kwa kulalama, kulialia huku tukitupiana lawama na majuto kwa miaka mitano.

Ni wakati sasa wa kutofautisha watawala na viongozi kwa mustakabali wa Taifa letu. Tunatakiwa kutafakari upya iwapo tunataka kutawaliwa au kuongozwa kama mataifa mengine.

Mungu ibariki Tanzania.