Katika makala mbili zilizopita nilikuwa nikichambua kuhusaina na ulimwengu mpya wa biashara. Nilieleza kwa kina namna uchumi ulivyohama kutoka viwanda kwenda taarifa na huduma, na hivyo kuathiri namna biashara zinavyofanyika.
Katika makala zile mbili nilieleza kwa sehemu kubwa kuhusu taarifa zinavyoathiri mienendo ya biashara. Katika makala hii leo ninamalizia kwa kuangalia uchumi wa huduma lakini mahususi tunaangalia kizazi cha wateja katika zama hizi za taarifa na huduma
Ni vema kutambua kwamba ile misukumo mitatu inayowaongoza wateja katika ulimwengu mpya wa biashara, ipo katika mfuatano usiobadilishika. Mteja wa sasa hivi anahitaji uharaka, urahisi na unafuu. Hii ina mana kwamba bidhaa ama huduma yako kama  haina urahisi wala uharaka; hata kama ukiiuza kwa bei ndogo kiasi gani huwezi kupata wateja.


Mambo hayo matatu hapo juu yamekuja kutokana na mwingiliano wa tamaduni za kimataifa, mibinyo ya maisha, migogoro katika jamii, kiu ya kuthaminiwa pamoja na mbadiliko wa mitazamo kuhusu maisha na mipaka ya mahusiano katika jamii. Kwa mambo hayo unaweza kuielezea jamii ya wateja wetu kwa sasa kuwa ni jamii inayopenda "ukisasa wa kiwango cha juu sana".


Kutokana na mabadiliko, changamoto na matamanio yote niliyoyataja hapo juu; wateja wa ulimwengu mpya wanatazamia kupata majawabu kutoka katika bidhaa na huduma zilizopo sokoni. Nitakupa mifano michache.
Siku hizi biashara ya saluni za kiume imeshika kasi kubwa katika miji na maeneo mengi. Zamani kidogo huduma kubwa katika saluni hizi ilikuwa kunyoa nywele basi. Lakini miaka ya karibuni uwanja wa huduma umepanuliwa kutoka kunyoa pekee kwenda katika kuosha uso, kukandwa mwili na manjonjo mengine mengi.
Kazi kubwa zinafanywa na mabinti. Kabla ya ulimwengu wa sasa kulikuwa na mipaka ya kimahusiano na mwingiliano; kwamba haikuwa jambo rahisi mwanaume aliyeoa ama asiyeoa kwenda mahala akashikwashikwa kidevu (mtanisamehe ikiwa nimetumia neno kali) kwa sababu tu eti ya kunyolewa.
Pointi ninayotaka uione hapa ni hii: wanaume wengi (waliooa na wasiooa) wanafurahia huduma za namna hii. Hili linamaanisha jambo moja kubwa; kuwa ipo faraja ama burudani ambayo wanaume hawa wanaipata saluni (kutokana na huduma hizi) ambazo wanaamini hazipatikani nyumbani mwao.


Nimekupa mfano wa saluni za kiume, lakini ni kawaida pia kwa sasa wanawake kumiminika masaluni na kuhudumiwa kucha zao na sehemu nyingine za mwili na wanaume.
Hapa utagundua kuwa kuna hitaji la kihisia limeibuka miongoni mwa wateja wa zama mpya na wajasiriamali wamesoma gepu hilo na wanalitumia kuzalisha fedha. Siyo lengo langu kubatilisha ama kuhalalisha huduma yoyote katika mifano yangu, lakini ninataka utambue kuwa kuzalisha fedha katika ulimwengu mpya wa biashara ni lazima utambue mabadiliko yanayotokea.


Wateja wa sasa wapo tayari kukulipa kiasi chochote cha fedha unachotaka maadamu tu huduma ama bidhaa yako iwe inajibu hisia ama hitaji lake halisi. Wewe kama una saluni na huna huduma ya wadada wanaoosha, usishangae kuona wateja hawaji kwako hata kama unanyoa kwa elfu mbili na wanaenda saluni yenye wadada inayonyoa kwa elfu tano.


Mwanamke uliye na ujuzi wa kuosha kucha kwa ustadi usishangae kuona wanawake wenzio wakikukwepa hata kama una bei chee na wanaenda kuwasaka vijana wa kiume. Ukiwa mjasiriamali siyo jukumu lako kuhangaika kujiuliza ni kwa nini watu wako namna hii siku hizi? Mengine waachie wanaharakati wa maadili na wanasaikolojia ila wewe angalia namna unavyoweza kutumia mabadiliko hayo kama fursa.
Wateja wa ulimwengu mpya wanataka kuthaminiwa na kukubalika. Biashara yoyote ni lazima ihakikishe kwamba inatoa huduma zake kwa kuangalia upande huu. Ikiwa una duka la nguo ni lazima uhakikishe kuwa mteja anapokuja si tu unamuuzia nguo bali pia unamuuzia kuthaminiwa na kukubalika. Mambo madogo madogo yaliyokuwa yakipuuzwa siku hizi ndiyo msingi wa kuhimili kwenye biashara.


Jambo la kutambua ni kuwa wateja wa zama mpya wanapima huduma zao kwa kutegemea maoni ya jinsia tofauti. Mwanaume anapovaa suti anataka kuona akikubalika mbele ya wanawake. Mwanamke akivaa nguo anajisikia vema ikiwa nguo hiyo inakuwa ikivuta usikivu mbele ya macho ya wanaume. Kwa hiyo, unapouza nguo ni lazima uhakikishe unajitahidi kuwa na huduma ambatanishi ikiwamo kumuelekeza mteja nguo sahihi, kumuhakikishia kuwa itampendeza na hata kumsifia ajaribupo hapo dukani kwako.
Tunaishi kwenye jamii ambazo hazithamini utu, jamii ambazo zinapita kwenye majanga makubwa ya kuraruliwa kihisia. Mke anatoka nyumbani kanuna, mume anatoka nyumbani kafura hasira, mtoto anakwenda shuleni akiwa na huzuni moyoni kwa sababu baba yuko bize kazini, mama yuko bize kazini; wanatoka alfajiri wanarudi usiku hawana muda wa kukaa na kuzungumza naye.


Mwananchi kila anapotembea anaugua moyoni kwa sababu anahisi serikali yake haimjali. Watu wote hawa ndiyo wateja wetu katika magari yetu, kwenye maduka yetu, kwenye saluni zetu, kwenye bucha zetu, hotelini na kila sehemu kunakofanyika biashara. Biashara yoyote yenye nafasi ya kusonga mbele katika nyakati hizi ni ile itakayokuwa na uwezo wa kujibu maumivu ya kihisia kwa wateja wa namna hii.
Ndiyo maana wateja wa sasa wanathamini huduma kuliko hata bidhaa inayouzwa. Mtu akienda kununua nyama buchani kipaumbele chake si tu kupata nyama (bidhaa) bali ni pamoja na anavyopokelewa, anavyojibiwa na anavyoagwa. Huduma unazotoa katika biashara yako zinaamua sana ikiwa mteja husika atarudi kesho ama ataenda moja kwa moja.
Hapa utagundua kitu kingine: Zamani tulizoea kusema mteja ni mfalme, lakini katika zama za ulimwengu mpya wa biashara mteja amepanda cheo kutoka mfalme na sasa mteja ni "bebi" (baby). Bila shaka umesikia msemo wa vijana wa kisasa wakisema, "Uzee mwisho Chalinze, mjini kila mtu ni bebi". Basi ubebi huu ndiyo uliopo vichwani mwa wateja wa zama mpya, hivyo lazima uwahudumie wateja kwa mtindo wa kudeka na kubembeleza.
Kama nilivyobainisha hapo juu ni kwamba ukiiangalia jamii ya wateja wa ulimwengu mpya utagundua kuwa "wanadeka sana", "na wana uvivu fulani". Uvivu na kudeka huku ni fursa nzuri sana kwa wajasiriamali. Ukianzisha huduma ambayo inabembeleza na kuwafanya wadeke basi uwe na uhakika kwamba watakuwa tayari kukulipa bei yoyote unayotaka.


Kwa mfano, kama unafanya biashara ya kusafirisha  abiria, magari yako yakiwa ya kisasa, viti vya kunesanesa na vyenye kubembeleza una nafasi ya kuwapata wateja wengi kuliko kuwa na magari ambayo hayabembelezi wala kudekeza wateja.
Katika eneo la wateja kuwa na uvivu fulani napo utabaini kwamba kuna mambo ama kazi ambazo wateja wa kisasa hawataki kuzifanya. Hivyo, ukiweza kutoa huduma kwa kazi ama mambo hayo ni rahisi sana kuzalisha fedha. Mathalani, si watu wengi wapo tayari kubeba taka na kuzipeleka dampo hasa maeneo ya mjini. Ukijipanga na kuanzisha biashara ya kukusanya taka unaweza kuzalisha faida.


Nafahamu sehemu za mijini kama Dar es Salaam na maeneo mengine tayari kuna wajasiriamali waliochangamkia fursa hii. Kikubwa ninachotaka ukione hapa ni kuwa katika zama mpya za uchumi na biashara; faida kubwa zipo katika kuziba pengo la uvivu wa wanajamii.
Siutaji uvivu kwa nia mbaya, la hasha! Ukae ukijua kwamba hata waliogundua lifti za maghorofa ilikuwa ni kutokana na uvivu wa kupandisha kwa miguu kwenye maghorofa. Uvivu ninaoumaanisha katika dhana ya wateja wa ulimwengu mpya wa biashara ni ule unaolilia kurahisishiwa mambo.
Katika hayo yote tunarudi katika msingi wa uchumi wa zama mpya ambao ni kufikiri kwa kina. Ukiwa mzembe katika kufikiri huwezi kuibuka na ugunduzi, huwezi kuibuka na ubunifu, huwezi kutambua namna za kuwateka wateja na huwezi kudumu katika biashara. Mtaji mkubwa katika biashara za ulimwengu mpya ni kufikiri kwa bidii ukiwa ndani ya ubongo wa wateja unaotazamia kuwahudumia.
Unahitaji kujipanga kwa ajili ya ulimwengu mpya wa biashara!
stepwiseexpert@gmail.com, 0719127901

4301 Total Views 4 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!