Wanangu, ningependa mpokee mawazo yangu muone,  je, kuna tija yoyote ya kuwa mbele katika mambo ambayo mimi niko nyuma kama wazee wengine wa zamani; na kwamba uzembe huo wa kutokwenda na wakati ninyi mwendao na wakati mmefanikiwa kwa kiwango gani!

Hoja si kubishana bali hoja ijibiwe kwa hoja ya haja na si haja bora hoja. Nasema hivi kwa sababu kwanza nataka nipate fursa ya kutoa maoni yangu katika mabadiliko ya Katiba, nataka nipate muda wa kupitia faili langu la miaka mingi kidogo ya nyuma kama waasisi wa taifa hili kiutamaduni, kiujamaa, kujitegemea, kiushirika, kisiasa, na kadhalika.


Nitaangalia Katiba mpya katika mtazamo wa ukale zaidi, uliotufikisha mahala tukawa na heshima katika bara hili la Afrika na nje ya Afrika. Nitaangalia vitabu na nyaraka mbalimbali zilizotufikisha hapa tulipo na tukawa na historia napo kwa kizazi chenu.


Wanangu, najua kuwa kuna mambo mengi yenye matatizo katika Katiba, lakini kwa mtazamo wangu kuna makubwa mawili yamechangia kuonekana Katiba ina matatizo yasiyoweza kuvumilika. La kwanza ni kuliacha Azimio la Arusha na la pili ni mfumo wa vyama vingi vya siasa.


Wachambuzi wa mambo na wenye upeo mkubwa kuliko wangu, watapinga hoja hii kwa sababu wao wanatumia zaidi usomi na usasa ambao ndiyo uliofifisha ukale tulioishi maisha bora kwa kila Mtanzania.


Muhimu zaidi nitakalolipinga ni wazo la rais kupunguziwa madaraka aliyonayo, kwa sababu ikitokea nimechaguliwa haitanisaidia katika utendaji kazi wangu. Nitakuwa kama kiranja mwenye viranja ambao siwezi kuwashughulikia wakarofi.


Ikitimia ndoto yangu nikachaguliwa kuwa rais nitafanya yafuatayo:

Kwanza, nitawafukuza kazi viongozi watendaji ambao wamekuwa wanasiasa, viongozi ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao na muda mwingi wanafanya vikao na waandishi wa habari kujitakasa. Hao fagio la chuma nitalishika mwenyewe sitakasimisha madaraka kwa msaidizi wangu yeyote hata Waziri Mkuu.


Pili, nitavunja mikataba yote mizuri na mibaya tuanze upya, nitatumia falsafa muhimu sana ya “usipochafuka utajifunzaje”. Baadhi ya Watanzania wataumia kwa muda mfupi lakini watafurahi kwa muda mrefu.


Nitapiga marufuku safari zote za viongozi ndani na nje ya nchi, kwa kuwa sasa dunia ni kijiji kwa hiyo naamini kwa dhati kabisa kuwa safari za mafaili haziko tena baada ya kuingia katika kizazi cha dot.com, kwamba kazi hizo zinaweza kufanywa pale ulipo na pale alipo, hapa nahisi kutokana na tabia ya kupenda fedha za umma watu hujitoa katika kundi la dot.com.


Nitaunda kikosi kazi maalumu kitakachochunguza mali za viongozi walioondoka madarakani na uhalali wake, kukiwa na shuku yoyote na kwa kuwa sijapunguziwa madaraka ya urais basi mimi si malaika nisiyefanya kosa, nitataifisha mali zote kwa manufaa ya Watanzania.


Nitatunga sheria zangu mpya kama kanuni ndogondogo kwa manufaa ya Watanzania. Ndani ya kanuni hizo nitaonesha uwezekano wa rais kuamua jambo ghafla kwa manufaa ya Taifa na si manufaa ya mtu binafsi.


Nikiwa rais nitapendekeza kuwa rais awapo madarakani hatakiwi awe na uhusiano na mawasiliano ya ndugu, jamaa na marafiki, ili kumpa nafasi ya kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Sitakuwa na mialiko isiyo na sababu za msingi, muda wote nitakaa Ikulu nikifanya tathmini kujua Watanzania wanataka nini.


Msahafu wangu wa utendaji utatumika katika hali ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na kwamba chetu ni cha Watanzania na si cha viongozi. Kwamba matunda ya Uhuru yaliwe na wote na joto la Uhuru liotwe na wote.


Mwisho sitafanya sherehe yoyote ya kuchaguliwa kuwa rais, kwani ni sawasawa na kukabidhiwa mgonjwa mahututi atibiwe nawe ukaanza kuonesha furaha yako badala ya kumtibu. Lengo halitaeleweka kama unataka afe ama apone.


Wakatabahu, naomba mniunge mkono kama mgombea binafsi, naomba mnikubali niwe rais wenu katika kipindi kijacho, naomba myakubali mabadiliko ya kisiasa kutoka mbele kwenda nyuma, kutoka tulipo kurudi tulikokuwa.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri