Niliposikia malalamiko ya watu kuwa Mheshimiwa Magufuli anachelewa kutaja baraza la mawaziri nilikuwa najiuliza kwani mawaziri ni lazima akurupuke kuwachagua ili serikali iwepo au hao wanaoitwa makatibu wakuu kazi zao ni zipi kama siyo kusimamia wizara zao kiutendaji, na ukweli ni kwamba walifanya kazi sana kiasi cha baadhi kuanza kukataa kuwa na mawaziri.

Wakati wa kampeni zake Mheshimiwa Rais Magufuli alisema bayana kuwa kinachomkera ni umaskini na utumishi mbovu serikalini uliosababisha ananchi kukata tamaa na serikali yao na aliahidi kuwa akiapishwa atashughulika nao ipasavyo ili kuhakikisha kuwa heshima ya serikali inarudi mahali pake na utumishi utatukuka na kuleta maendeleo.

Leo nimeamua kuandika waraka huu baada ya kuona kila uchao una mabadiliko yake katika uongozi, wapo wanaosema nafuu ya jana na wapo wanaosema sasa anazidi kutuumiza, ukweli ni kuaminishana na baadhi ya watu wachache ili tuliowengi tujenge taswira ya ubaya wa uongozi wa uliopo na kwamba tuone mambo yanayofanyika ni kwa Watanzania wote na siyo mtu anayehusika.

Baada ya uteuzi majipu yamezidi kukamuliwa, mengine yamewagusa watu ambao walikuwa wanawafadhili na tumeaminishwa ni roho mbaya ya kiongozi aliyemtumbua, kimsingi nchi yetu ilioza katika dhana nzima ya utumishi wa umma, wapo waliodhani wao ndio wenye serikali na wakasahau kuwa wao ni waajiriwa wa Watanzania.

 

Hivi sasa Mawaziri nao wameanza kutumbua majipu kidogokidogo, watu wengi wanasema eti mawaziri hao wanaiga mtindo wa  kiongozi wao, mimi nilidhani kwa sasa kiongozi wao alipaswa kupumzika na kuangalia mambo mengine ambayo bado ni kero kubwa kwa wananchi na Mawaziri wakafanya kazi ya kutumbua majipu na sisi wananchi tukawasimamia na kuwapongeza kwa kazi hiyo.

Baadhi ya Mawaziri wanafanya hivyo, mimi kama Mtanzania nawapongeza kwa kazi hiyo ambayo kimsingi hawafanyi ili waonekane lakini wanafanya kwa mujibu wa sheria, na unapoona taarifa kwa umma kwa kupitia taarifa za waandishi siyo kwa sababu ya kujitangaza kuwa waonekane wanafanya kazi, ni kwa sababu Watanzania wanatakiwa kujua nini kimetokea, na haki ya kupata habari kwa Watanzania kwa mujibu wa sheria yetu ya habari.

Nimewasikia Mawaziri kama Mwigulu akifanya kazi ya kutumbua, nimemsikia Profesa Ndalichako anatumbua, Maghembe anakamua majipu huko utalii, Simbachawene alianza na kuna baadhi ya mabadiliko ya  kauli ni majipu tosha kwa wanaohusika, wote nawapongeza, mkubwa akikamuliwa na mdogo anaanza kufikiria kukamua wadogo zaidi na kwa mtindo huo nchi itanyooka baada ya muda mfupi.

Wapo walianza kusema siku nyingi kwamba nchi hii imeoza kwa rushwa na mimi nakubali kuwa kweli ilioza kwa rushwa, nilidhani ni tatizo kubwa sana ambalo haliwezi kudhibitika kwa muda mrefu, kumbe suala la rushwa linaweza kwisha hata kwa siku moja, mfano ni huu dhahiri ambapo mkubwa amesema basi suala la utegaji kazi na kukwepa kodi matokeo yake tumeyaona dhahiri bila shayiri kuwa yametimia ya Musa.

Hivi sasa pongezi zinashuka kila uchao kwa kiongozi mkuu ambaye anajaribu kutupeleka katika barabara anayotaka twende, nchi za nje wamekuwa mstari wa mbele tangu alipoapishwa kumpongeza hatua anazozichukua kiasi cha sisi Watanzania kuwashangaa wageni hao wa mataifa hayo kwanini wanatupongeza na kumpongeza kiongozi wetu.

Siku za hivi karibuni viongozi mbalimbali wa madhehebu wamekuwa wakitoa pongezi na kufanya ibada maalumu za kumwombea ulinzi wa kiroho zaidi, wapo viongozi waliofika kwake na kumpa Baraka na wapo viongozi wa serikali za nje waliofika Ikulu kumpa pongezi, hili ni jambo jema linalotia moyo.

Viongozi wakuu wastaafu tumewashuhudia wakifika kwa nyakati tofauti kumpa pongezi, mioyoni wanajua ugumu wa kazi anayofanya, wao wanafarijika kwa kuwa anaendeleza pale walipoachia wao, jukumu letu kama Watanzania ni kumuombea aendelee kukamua majipu lakini tusifikirie ataweza kufanya mwenyewe bila kumsaidia, hiki ni kitimutimu cha Magufuli na Mawaziri wake wa awamu ya tano

Sisi tulioko mitaani mijini na tulioko vijijini tufanye kazi ya kukamua vipele na vijipu uchungu ambavyo vikiachwa yatageuka kuwa majipu makubwa, naamini Mawaziri nao wataendelea kupambana na majipu kila siku, rai yangu ni Watanzania kuwaombea pia viongozi hawa mawaziri kwa kuwa wao tuko nao jirani zaidi kuliko rais kiusalama.

 

Wasaalamu

Mzee ZUZU 

Kipatimo.

By Jamhuri