Prof. Ndalichako tumbua jipu NECTA

Joyce NdalichakoNi matumaini yangu mu wazima wa afya na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku katika harakati ya kuijenga nchi yetu. Binafsi  ni buheri wa afya nikijitahidi kuendana na falsafa ya ‘hapa kazi tu’ kukwepa jipu litakalochangia kutumbuliwa.

Nikiwa mdogo, babu yangu alinifundisha kupaka dawa ya mswaki juu ya ngozi yenye uvimbe (ikiwa ni dalili ya kutokea jipu) na uvimbe ule ulipotea kabisa na kuniaminisha ya kwamba dawa ya mswaki ni dawa ya jipu, na ndiyo maana hadi hii leo nimekuwa mwoga kutumbuliwa jipu kwa sababu babu yangu alinifundisha namna ya kuliondoa jipu mapema kabla halijawa kubwa na kuiva ili hatimaye litumbuliwe.

Najiuliza, iwapo wenzangu mmzoea kutumbuliwa, hamuogopi kutumbuliwa na kama hamuijui dawa ya babu. Yamkini kuna watakaosema ndiyo wanaijua dawa ya kuzuia kukua kwa majipu na wapo watakaosema dawa yake ni moja tu – kulitumbua.

Je, ipi ni njia rahisi na yenye athari ndogo kuliko nyingine? Kutumia dawa ya babu au kusubiri hadi jipu liive ndiyo litumbuliwe?

Binafsi naona Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA) ni “jipu”, lakini je, jipu hili tunalitibu vipi? Tutumie dawa ya babu yangu (mzee Namangunga) au tusubiri liive ili litumbuliwe? Kila mtu atatoa jibu lake, na kila njia ina athari zake.

Hata hivyo, kwa hili la NECTA dawa ya babu inafaa zaidi kuliko kusubiri liive kwa sababu muda wote huu wa kusubiri liive, mgonjwa anapata mateso makubwa yanayomfanya kupata joto kali na homa, kisha kidonda  na majeraha yanayotokana na utumbuzi. Mtasema nampendelea babu yangu, lakini la hasha.

Babu alikuwa na utaalamu uliotukuka kwenye kugundua athari za kuliacha jipu live, ndiyo maana akagundua dawa ya kulitibu mapema.

NECTA ilianzishwa rasmi mwaka 1973 baada ya Tanzania kujiengua kutoka Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki; likijumuisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 1971. Baada ya kujiengua ilibaki kama idara ndani ya Wizara ya Elimu huku ikiwa na majukumu ya kusimamia mitihani yote na mitaala nchini.

Muda mfupi baadaye, sheria iliyounda Baraza hilo ilibadilishwa na kugawanya majukumu ya Baraza kwa kuunda idara mbili zinazojitegemea; yaani NECTA kwa ajili ya mitihani na jukumu la kukuza na kusimamia mtaala likabaki chini ya Wizara ingawa baadaye ilihamishiwa Chuo Kikuu cha Elimu cha Dar es Salaam kabla ya kuudwa kwa idara kamili iliyotambulika kama Taasisi ya Kukuza Mitaala (Institute of Curriculum Development -ICD) na kuanzia mwaka  1975 ikabadilishwa na kuitwa Taasisi ya Elimu Tanzania (Tanzania Institute of Education).

Hivyo ndivyo mapacha hao walivyozaliwa, walivyolelewa kwa karibu kabisa na mama yao (Wizara ya Elimu) kwa takribani miaka 35 hivi. Kipindi hicho, babu alikuwa mzima ana uwezo wa kuongea kwa sauti ambayo nina uhakika mama wa mapacha hao (NECTA na TIE) alikuwa anaisikia na kujaribu kuiba mbinu za kitabibu alizokuwa akinipa. Nina uhakika na hilo kwamba ‘Mama Mapacha’ alitumia dawa ya mswaki kutibu majipu ya wanae.

Ni mwaka wa tatu sasa tangu babu afariki. Hakuna wa kunielekeza tena namna ya kutibu jipu kabla halijawa kubwa. Hii imesababisha ‘Mama Mapacha’ kusahau  namna ya kutibu jipu likingali dogo, jambo lililomfanya mwanae Kulwa (NECTA) kuwa jipu hadi leo linakaribia kuiva.

Baraza la Mitihani Tanzania ndiyo chombo kilichopewa majukumu ya msingi ya kutunga mitihani kulingana na Sera ya Elimu kwa kuandaa eneo na mazingira mazuri ya kufanyia mitihani, kupokea nyaraka na taarifa zote zinazoweza kuathiri Sera ya Elimu na kubadili sera kulingana na changamoto zinazojitokeza.

Baraza linaongozwa na Mwenyekiti na Katibu Mtendaji ambaye ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku za Baraza hilo.

Tangu kuanzishwa kwake, Baraza limeongozwa na wenyeviti wanane na makatibu saba wakiwamo hawa waliopo madarakani; yaani Profesa Rwekaza Mukandala ambaye ni Mwenyekiti, na Dk. Charles Msonde, ambaye ni Katibu Mtendaji.

Dk. MSonde aliingia madarakani mwaka 2014 baada ya sintofahamu ndani ya Baraza, hali iliyomlazimu aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza wakati huo, Prof. Joyce Ndalichako, kwenda likizo ya kitaaluma.

Kuondoka kwa Prof. Ndalichako kumeleta mabadiliko mengi katika taasisi hiyo ikiwamo kuanzishwa kwa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). BRN ilitajwa kuwa na lengo la kuleta mtaala wenye tija, ufanisi na unaokidhi mahitaji ya soko la ajira katika kuleta maendeleo ya Taifa na kuhimili ushindani.

Kubadilika kwa sera ya elimu, na kuwapo kwa mpango wa matokeo makubwa sasa, kumechangia mabadiliko katika upangaji wa madaraja kwa kisingizio cha kubadilika kwa sera ya elimu, huku zikitolewa sababu hafifu za kuwa na mfumo mmoja wa matokeo katika ngazi zote za elimu.

Mpangilio wa zamani wa madaraja wa kuwa na darala la I-IV ukafutwa. Mfumo ulioainisha kwamba daraja la kwanza linaanzia kwa mwanafunzi mwenye kiwango cha ufaulu cha alama 7-17, daraja la pili alama 18-22, la tatu alama 23-25, la nne alama 26- 33 na atakayepata alama chini ya hapo atakuwa ameshindwa atawekwa kapuni.

 Badala yake wametengeneza madaraja ya ufaulu kufikia matano, ikiwa na maana kwamba, mtu aliyekuwa amefeli kwa mfumo wa zamani, kwa mfumo mpya atakuwa amefaulu kwa daraja la tano. Hapa babu alikuwa ameshafariki na Mama Mapacha akasahau namna ya kutibu majipu bila kuyatumbua nilivyoelekezwa.

Mama Mapacha akaendelea kusubiri jipu liive kwa kuendelea kubadili mfumo wa matokeo, na safari hii wakaenda mbali zaidi na kuleta mfumo mpya unaotumiwa na taasisi za elimu ya juu.

Binafsi naona ulikuwa na lengo la kutafuta suluhu ya muda mfupi na kuficha uhalisia wa kushuka kwa kiwango cha elimu yetu. Mfumo wa wastani wa alama ambao kwa lugha ya kigeni unaitwa grade point average (GPA), ni mfumo mgumu kueleweka.

Mfumo huu wa matokeo huonesha wastani wa alama alizopata mtahiniwa. Kwa mfumo huu, mwanafunzi anayepata alama D katika masomo mawili au ‘gredi’ C, B, B+, au A katika masomo pungufu ya saba atakuwa amefaulu. Mwanafunzi huyu ambaye masomo yake hayakutimia 7, kwenye mfumo wa awali matokeo yake yangekuwa hayajakamilika, hivyo yasingelitoka.

Si hivyo tu, mfumo huu pia unaongeza uzito wa gredi. Mfumo wa awali gredi A ni 100-81, B ni 80-61, C ni 60-41, D ni  40 – 30 na chini ya 30 ni sifuri, lakini kwa mfumo wa  sasa, idadi ya makundi ya gredi yameongezeka kutoka gredi tano hadi sita ambapo sasa A imekuwa 100- 75, kitu ambacho kimerahisisha upatikanaji wa gredi A tofauti na mfumo wa awali.

B+  ni 74-61, ambayo kwa mfumo wa awali ilikua ni gredi B, B ni 60- 55 ambayo kwa mfumo wa awali ilikuwa gredi C, C ni 54-50, D ni 49-30 na  E inayoanzia 30- 25 ambao kwa mfumo wa awali ilikuwa sifuri, na F inaanzia 24 hadi 0. Kwa mantiki hiyo, leo wanafunzi wanaopata chini ya 30 wamefaulu, lakini kwa mfumo wa awali ilikuwa wamefeli.

Leo ufaulu wa mtahiniwa unatafutwa kwa kuangalia idadi ya masomo aliyofaulu pekee na yale aliyofeli yanawekwa kando wakati mfumo wa awali ulimlazimu mtahiniwa afanye masomo yasiyopungua saba na kufaulu kwa sababu kila somo lilikuwa na uzito wake.

Hakuna anayejua tena kama dawa ya meno pekee ingefaa kupunguza athari na madhara ya maumivu ya jipu. ‘Mama Doto’ kasahau maneno ya babu na sasa tumeanza kuziona athari za hili jipu.

Wiki iliyopita nilimtembelea rafiki yangu mmoja anayeishi Tabata Kifuru, Dar es Salaam. Nilipofika tu, aliona fahari kunitambulisha kwa mdogo wake ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa uhandishi kwenye moja ya vyuo vikuu nchini kwa kusema “huyu ndiye yule dogo genius” akiwa na maana ya kwamba huyu ndiye mdogo wake mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri.

Sikusita kumpongeza kwa kumpa mkono na nikamwambia kuna kazi nahitaji anisaidie kuifanya nikiwa nazungumza na kaka yake. Nikatoa karatasi tupu na kalamu ya wino kutoka kwenye begi langu na nikamwandikia kwa lugha ya kigeni” use not less than 50 words to introduce yourself” nikimaanisha “tumia maneno yasiyopungua 50 kujitambulisha”.

Hapo ndipo nilipojua tofauti kati ya ‘genius’ wa sasa na wa zamani. Acha yabaki moyoni yote niliyoyaona kutoka kwa ‘genius’ wa siku hizi ila ninachoweza kusema ni  kwamba yatosha kumlinganisha mwanafunzi mwenye ufaulu wa daraja la juu kabisa wa siku hizi na yule wa daraja la tatu kwa mfumo wa awali wa matokeo.

Je, tunaelekea wapi? Kama nilivyosema, yule ‘genius’ anasoma uhandisi na yamkini si matusi, ‘ugenius’ wake anauendeleza kwenye shule kuu ya uhandisi. Kwa nilichokiona kutoka kwa ‘genius’ wa kisasa nina uhakika hata akimaliza chuo atakuwa na vyeti tu, lakini hataweza kulisaidia Taifa kama lengo mahususi.

Nyakati za nyuma kidogo niliwahi kumuuliza profesa mmoja (jina nimelihifadhi), kwa nini siku hizi muda mwingi nakuona mtandaoni na kwenye magrupu ya ‘WhatSapp’ tofauti na kipindi cha nyuma? Mwalimu wangu akanijibu “sina kazi ya kufanya”.

Nilipohitaji ufafanuzi wa kwa nini anasema hana kazi ya kufanya ilhali angali mwajiriwa wa taasisi ya elimu ya juu, akasema “watoto wa siku hizi hawana shida. Hawaulizi maswali, hawahoji kitu chochote, na hata tafiti wanafanyiwa. Sihitaji muda wa kujiandaa kwenda darasani, hakuna mwanafunzi anayenisumbua nikiwa nasimamia tafiti, na hakuna anayeuliza swali baada ya kipindi”.

Nikajiuliza hao wanafunzi ni wa aina gani, nikakosa jibu. Japokuwa nilipokwenda Tabata Kifuru ndiyo nikapata jibu la kwamba; yawezekana ‘genius’ ni mmoja wa mwanafunzi wa profesa wangu!

Lakini huyu ‘genius’ wa leo asingekuwa chuo kikuu kwa mfumo wa awali wa matokeo. Mfumo huu wa sasa umetengeneza bomu linalohitaji kuteguliwa kupunguza athari zaidi. Ni matokeo ya kudharau dawa ya babu mzee Namangunga.

Tukubali kutumbua majipu kwa muda ya wasomi wasio na tija, lakini utumbuaji uende sambamba na kutumia dawa ya babu kupunguza kujitokeza majipu mengine. Ni muda mwafaka sasa kwa wadau wa elimu kuliangalia hili kwa macho mawili kama lilivyotanabahishwa kwenye kona tatu za jamvi letu tukisubiri mtumbuaji kutufikia.

Mimi ni mwoga kutumbuliwa na ndiyo maana napaka dawa ya mswaki kwenye kila sehemu inayoonesha dalili ya kutokea jipu kama nilivyoelekezwa na babu Namangunga.

Nawashauri wakati mnasubiri mtumbuaji awafikie, tumieni dawa ya babu kwa kurudisha mfumo wa awali.

 

Mwandishi wa makala hii amejitanabahisha kuwa msomaji wa Gazeti JAMHURI na anapatikana kwa simu 0658 032008 au [email protected].