Yah: Magufuli; kama uchaguzi ukiamriwa urudiwe TZ, kubali

Mwanangu Magufuli kutoka Chato, uliyekuja mjini kwa gea ya ubunge, umeleta kizaazaa mjini hata watoto wa mjini sasa wanahaha na sampuli ya Msukuma wewe, eti “hapa kazi tu” asiyeweza aanze mwenyewe kuondoka. Nasikia misemo mingi sana – kuna kugufulika, tingatinga, matumaini, angaza na kadhalika.

Ulipokuwa motto, tena huko Chato, hukujua hata siku moja kwamba utakuja kupata nafasi ya kuja mjini na ukafikia katika nyumba kuu kuliko zote na ukawa baba mwenye nyumba. Hukuwahi kufikiria kwamba kuna siku utapewa dhamana ya kuongoza nchi hii ikiwamo mashamba ya kwenu kule Chato, ulikuwa ukilima huku ukiwaza mambo mengine kabisa, yawezekana uliwaza kumiliki mbuzi na ng’ombe kidogo ukiwa na utu uzima.

Si wazazi wala yeyote katika ukoo wenu ambaye alibashiri au kutarajia kuwa ungekuwa rais wa Tanzania, hata ukiwauliza kama walikuwa na ndoto hizo miezi michache iliyopita. Ni kudra za Mwenyezi Mungu ambazo zimewaelekeza Watanzania rais anayewafaa katika kipindi hiki. 

Mwanangu Magufuli wa kugufulika, ni mipango ya Mungu iliyokufanya ukaota ndoto na kuamua kuchukua fomu ya kugombea urais Tanzania, mizengwe na misukosuko ya kukupitisha ndani ya chama chako ilitosha kukuonesha kuwa kuna upinzani mkubwa katika ngazi hiyo, na kisha baada ya hapo ulipoingia katika ngazi za Taifa katika mfumo wa vyama vingi.

Uliona mwenyewe jinsi ulivyokutana na upinzani mkali, hukukata tamaa ulisonga mbele. Uliona jinsi mashabiki wa vyama walivyokuwa wakijaa katika mikutano yako na mikutano ya wenzako, ilitosha kukata tamaa hasa ulipokuwa ukisikia katika mikutano mingine ya wenzako kuna mashabiki walioamua kuzimia na wengine kumpigia deki mpinzani wako.

Ni ujasiri uliokuwa nao ukaweza kusema ‘hapa kazi tu naomba mnipe ridhaa ili niwaongoze katika awamu hii’. Wapo wengi tu waliokukataa na wapo waliokupigia kura kwa sababu zao lakini si kwa kukupenda, wapo waliokupenda na wapo waliokuchagua kwa maana ya kujua dhamira yako ni ipi.

Inatosha nikisema siku chache ambazo umeweza kukaa Ikulu kila mtu anaelewa ulikuwa unasema nini, kila mwananchi wa hali ya chini anaweza kusema Magufuli ni nani, na wale wote wapigaji wamekubatiza jina la nguvu ya soda, wapiganaji wa chini wanakuombea usipatwe na pepo la nguvu ya soda lakini pia eti wanasema zipo eti eti kwamba unaweza kununuliwa muda ukifika.

Magufuli, kama uchaguzi ukiamriwa leo urudiwe kubali, nakuhakikishia utashinda kwa asilimia tisini kwa kazi ambayo umeifanya siku hizi chache tu ulizokaa katika mjengo huo, wamekubali uamuzi wako wa ghafla, wamekubali utendaji kazi wa dharura kama ilivyokuwa katika mabarabara. Watanzania hawa watakumbuka maneno ya rais wa Awamu ya Nne kwamba yeye alikuwa mpole, sasa muziki umefungwa wacheze wao.

Magufuli umebadilisha ghafla mifumo ya maisha ya watu, jinsi ya watu kulala, jinsi ya watu kuamka, jinsi ya watu kula, jinsi ya watu kufanya kazi, jinsi ya watu kutembea, na jinsi ya watu kuongea. Magufuli ni neno la kumshtua mtu aliyelala, Magufuli ni nguzo ya wanyonge ambao siku zote haki zao zilipotea, Magufuli ni kama mwokozi wao wale wanyonge lakini adui mkubwa kwa wale  walioamini kwamba nchi hii ni mali yao na hakuna kuhojiwa.

Najua ni siku chache sana ulizokaa Ikulu, najua una maadui wengi kabla ya kuingia Ikulu na baada ya kuingia Ikulu, mzee wa figure unaogopwa. Kuna watu wamejipanga kufanya kila linalowezekana kuiweka mfukoni Serikali yako kama ilivyokuwa kwa Nyerere, yaelekea unafahamu, jipange vizuri.

Watanzania hawahitaji ufanye makubwa sana, wanahitaji utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Magufuli. Watanzania walichoshwa na undugunaizesheni, posho za vikao, safari za nje, ufalme wa madaraka, sheria kutofuata mkondo, ufisadi, kufumbia macho mambo mazito, kucheka na vibaka na panyarodi,  kuponda utamaduni wetu, kuporomoka kwa maadili, kukosa uzalendo, kupanda kwa bei ya mafuta, mishahara midogo kwa watumishi wa umma. Watanzania walichoshwa na kukosa huduma muhimu za jamii kama afya na elimu sahihi, riba za mikopo, na kadhalika.

Najua safari uliyopo ni miaka mitano na huwezi kukamilisha yote kabla ya uchaguzi ujao, lakini ukiweza haya machache nakuhakikishia uchaguzi ujao utaomba kura siku ya mwisho tena kwenye TV na hutahangaika na hayo makilometa 17,000 uliyokimbia kuutafuta urais mwaka huu. 

Hutapata mpinzani katika kinyang’anyiro hicho kwa kuwa nao utakuwa umewakosha. Baada ya miaka kumi atakayegombea urais atajipima kwa viwango vyako.

 

Wasaalam, 

Mzee Zuzu,

Kipatimo.