Kwenye kitabu chake What is not sacred? (Kipi siyo kitakatifu?) mwandishi na mwanazuoni Padri Laurenti Magesa anajenga hoja kuwa mila na tamaduni za Waafrika wanaoishi chini ya Jangwa la Sahara hazikupewa uzito unaostahili pale jamii hizi zilipofikiwa na dini kutoka maeneo mengine ya dunia.

Yote yaliyokutwa kwenye mila na tamaduni zetu yalionekana hayafai na jitihada kubwa ilifanyika kupandikiza mila na tamaduni, ikiwa ni katika utamaduni wenyewe, dini, na falsafa, zilizoonekana kuwa ndiyo sahihi kwa mtazamo wa wakati huo. Jitihada hiyo ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa na hadi hii leo imeacha athari nyingi. Na siyo ni zote ni nzuri.

Anajenga hoja kuwa ipo hazina kubwa katika mila na tamaduni zetu ambayo inaweza kuwa somo jadidi kwa zile tamaduni ambazo ndiyo zilipazwa na kuonekana za maana kuliko tamaduni zetu.

Yapo mengi ya kujifunza juu ya elimu yetu ya jadi, uhusiano wa kifamilia, mifumo ya uwajibikaji, na kuhusu rika na mamlaka za rika mbalimbali katika jamii zetu. 

Elimu zetu za zamani zilifundisha kuwa mkubwa akiongea mdogo husikiliza na kufuata maelekezo; leo tunaambiwa kuwa mkubwa anapaswa kukaa na mtoto na kumsikiliza. Kwa kifupi, hata watoto wana maoni yao ambayo yanapaswa kusikilizwa na wakubwa. 

Ukweli ni kuwa hakuna jibu rahisi kwa sababu yapo mazingira ambayo wakubwa hawana budi kusikiliza maoni ya watoto. Lakini elimu hiyo hiyo ilitufundisha kuwa ipo mipaka ya kuzingatia. 

Kwenye utangulizi wa kitabu cha Padri Magese, mwana theologia Benezet Bujo anasema kuwa mitazamo ya tamaduni inapokinzana iwekwe jitihada ya kila upande kujifunza kutoka upande mwingine, badala ya kuweka jitihada ya kubadilisha mawazo ya upande mwingine. 

Lakini kukubali sana tamaduni za nje pia kumedhoofisha nidhamu ya wadogo kwa wakubwa. Na hakuna msingi mkubwa zaidi wa mila zetu kama wadogo kutii wakubwa.

Elimu yetu ya jadi iliwaandaa vijana kuishi maisha ya watu wazima na kubeba dhima zinazoambatana na maisha hayo, ikiwa ni pamoja na kuishi ndani ya maisha ya ndoa. Tulifundishwa kuwa ndoa ni kati ya mwanaume na mwanamke, siyo kati ya mwanamke na mwanamke; au kati ya mwanaume na mwanaume kama ambavyo baadhi ya jamii sasa zinakubali. 

Kwenye baadhi ya jamii za Mkoa wa Mara ambako mwanamke mzee alimuoa binti au mwanamke wa umri mdogo, uhusiano ule ulikuwa unafanana zaidi na wa mzee yeyote aliyefika umri mkubwa kutafuta msaidizi nyumbani wa kufanya kazi, lakini siyo mwenza wa kuishi naye kama ilivyo kwenye ndoa hizi za jinsi moja ambazo zimeanza kuhalalishwa kwenye baadhi ya nchi.

 

Msingi wa kuhalalishwa kwa ndoa hizi ni kufikia uamuzi kwenye nchi hizi kuwa uwepo wa ndoa za jinsi moja, kama ambavyo ni haki ya raia wenye ndoa za jinsi tofauti, ni haki ya msingi ambayo kila raia ana haki nayo kama haki nyingine za binadamu. 

Hata hivyo, pamoja na kuwa ajenda hii tunaisikia sana siku hizi, ni nchi chache sana duniani ambazo zimehalalisha utaratibu huu. Kati ya zaidi ya nchi 200 duniani; ni 18 tu ndizo zilizoidhinisha ndoa hizi.

Na hizi ni nchi zenye sauti kwenye masuala ya kimataifa na ndiyo maana viongozi wake wanapozungumza hutegewa sikio. Hatukubaliani nao, lakini tunawategea masikio. Kwenye ziara yake ya nchini Kenya mwaka huu, Rais Barack Obama wa Marekani, alimhimiza Rais Uhuru Kenyatta kuweka taratibu ambazo zinatoa haki chini ya sheria kwa wale ambao wanapigania haki hizi.

Tatizo ninaloliona mimi si la kisheria tu, ila ni juu ya makubaliano kuhusu nini hasa kipewe haki chini ya sheria. 

Sheria za jamii yeyote zinatokana na makubaliano ndani ya hiyo jamii kuhusu maudhui ya mkusanyiko wa miongozo inayounda maadili ya jamii hiyo. Nchi zote haziwezi kuwa na msimamo mmoja juu ya maadili ya msingi ambayo yatakubalika kwa binadamu wote. 

Kwa hiyo linaloonekana la kawaida sehemu moja litaonekana kufuru sehemu nyingine. Linaloonekana zuri upande huu, litaonekana dhambi upande ule.

Na kama alivyojibiwa na Rais Uhuru Kenyatta, si rahisi kwa serikali kulazimisha raia kukubali tamaduni ambazo wananchi wenyewe wanaamini zinakiuka maadili ndani ya jamii yao. 

Jitihada za kushurutisha upande mmoja ukubali mtazamo wa upande wa pili bila kuzingatia misingi ya mila na utamaduni wa upande wa pili ni jambo ambalo halitaleta maridhiano ya aina yoyote. 

Ni kweli kuwa mila na tamaduni hubadilika na hatimaye hubadilisha hata sheria zilizopo, lakini ni mchakato ambao unaenda kwa kasi yake bila ya upande mmoja kuulazimisha upande mwingine. 

Kuna nchi nyingi za magharibi ambazo zilianza michakato ya uchaguzi ambayo haikuruhusu wanawake kupiga kura. Lakini baadaye nchi hizi zilibadili sheria kuruhusu wanawake kupiga kura. 

Kupiga kura kwa wanawake si suala ambalo linaleta malumbano makali kama suala la kuhalalisha ndoa za jinsi moja; kwa hiyo upo uwezekano pia kuwa zipo nchi zitaendelea kukataa kulazimishwa kukubali mabadiliko ya aina hii.

1336 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!