Upo wakati kwenye ndoa ambako mmoja wa wanandoa anaweza akawa anataka kuuza au kubadili jina la nyumba/kiwanja bila ridhaa ya mwenzake ilhali nyumba hiyo ni ya familia.

Lakini pia nje ya hilo kuna mazingira ambayo mtu anaweza kuwa si mwanandoa, lakini ana maslahi katika nyumba au kiwanja cha mtu fulani na anataka kuzuia nyumba/kiwanja hicho kisibadilishwe jina au kisiuzwe. Kisheria jambo hilo linaruhusiwa na huitwa zuio (Caveat). 

Hili si zuio la kwenda mahakamani kama mazuio tuliyoyazoea. Hili ni zuio jingine kama nitakavyolieleza. Aidha, kuzuia hati isibadilishwe kimsingi ni sawa na kuzuia nyumba isiuzwe. Hii ni kwa kuwa hakuna namna ambavyo mnunuzi anaweza kununua kitu ambacho hakiwezi kubadilika na kuingia katika jina lake.

Ikiwa mke ana wasiwasi kuwa mume anaweza kumzunguka na kuuza mali ya familia au mume ana wasi wasi juu ya uwezekano wa mke kuuza, basi wanayo ruhusa ya kuweka zuio ili hati ya nyumba isibadilishwe. Yapo mambo mengi kuhusu hili; nitaeleza baadhi.

 

1.  Nini maana ya zuio?

Zuio ni usitishwaji wa muda ambao huwekwa ili kuzuia mabadiliko yoyote katika hati. Kama maana yenyewe inavyojieleza, huu unakuwa ni usitishwaji wa muda ambao unalenga kulinda maslahi ya mtu aliyeomba zuio. Kuitwa zuio la muda haimaanishi kuwa mtu akizuia itakuwa ni mwezi mmoja au miwili basi, hapana. Ni zuio la muda kwa kuwa haliwezi kukaa milele lakini mtu akishaliweka linaweza kukaa hata miaka mingi kutegemea na sababu za zuio hilo.

 

2. Mwanandoa kuzuia hati isibadilishwe

Lazima ieleweke wazi kuwa si kila mtu anaweza kuamua na akazuia hati ya mtu isibadilishwe. Wapo watu ambao kwa mujibu wa sheria wanayo haki ya kuomba hati isibadilishwe. Kwanza mke au mume; mmoja  kati yao anaweza kuweka kizuizi katika nyumba ya ndoa (matrimonial home) iwapo kuna dalili kuwa mmiliki aliyeandikishwa anaweza kuiuza au kuiweka rehani bila ya ridhaa ya mwingine.

Mara nyingi migongano katika familia inapoanza mmoja kati ya wanandoa hukimbilia kuuza baadhi ya mali kwa aidha kumkomoa mwenzake au sababu nyingine yoyote. Kwa hiyo ili kuliepuka hilo unapogundua kuwa kuna uwezekano huo basi sheria imekuruhusu mwanandoa kuweka zuio ili hati isibadilishwe na hivyo kuepuka kuuzwa kwa mali.

 

3. Hata mkopeshaji anaweza 

kuweka zuio kwenye hati yako

Nimezungumzia zaidi wanandoa kuzuia lakini pia ieleweke wazi kuwa suala la kuzuia si tu la wanandoa. Kampuni, shirika, mtu  binafsi au taasisi ya fedha iwapo imemkopesha mtu na akaweka  nyumba/kiwanja kama dhamana ambacho kina hati, basi wanayo ruhusa ya kisheria ya kuomba zuio liwekwe kwenye hati ile ili dhamana isije kutumiwa kukopea pesa katika taasisi nyingine au kuuzwa wakati ipo kulinda deni. Kwa hiyo iwapo mtu ana maslahi ya namna hii kwenye ardhi inayomilikiwa na mwingine basi ni haki  kwake kuweka zuio hili ili kulinda maslahi yake.

 

4. Wapi upeleke maombi ya kuzuia hati isibadilishwe?

Mamlaka za ardhi ni mamlaka ambazo hutakiwa kupelekewa maombi haya ya zuio. Mara nyingi mamlaka za ardhi huwa zipo katika ofisi za wilaya au manispaa katika mkoa wako isipokuwa kwa walio Dar es Salaam maombi hupelekwa makao makuu pale wizara ya ardhi kama ni hati. 

 

5. Maombi ya kuzuia hati isibadilishwe huandaliwaje?

Maombi haya si maombi kama maombi mengine yalivyo. Maombi haya ni maombi ya kisheria na huandaliwa katika ofisi za wanasheria na hupelekwa yakiwa na muhuri wa mwanasheria. Karika maombi hayo mwombaji hueleza jina lake kwa urefu, anuani yake, uhusiano wake na yule ambaye jina lake ndilo liliko kwenye hati yaani anayemwekea zuio huku akieleza sababu za msingi kwanini anataka kuzuia hati isibadilishwe.

 

6. Lazima maombi yaambatane na nyaraka hizi

Kwanza, picha 2 za mwombaji huku kila picha moja ikibandikwa kwenye nyaraka moja. Pili, risiti za malipo ya ada ya usajili. Maombi haya hulipiwa kiasi cha fedha lakini si kikubwa sana kwa hiyo lazima uambatanishe na risiti za malipo.

Tatu, mwombaji aambatanishe vielelezo vinavyompa haki juu ya kiwanja husika, kwa mfano, cheti  cha  ndoa, mkataba  wa mkopo n.k. kwa  leo  ni hayo.

By Jamhuri