Nakumbuka niliwahi kuwaandikia barua ya kuwataka muwe makini na hayo yanayoitwa maendeleo. Baadhi yenu mlionesha kuipinga kwamba hakuna maendeleo yasiyokuja na mabadiliko ya tabia.

Leo nimeamua kuwakumbusha juu ya utunzaji wa maliasili tulizorithi kutoka kwa wakoloni ambao, pamoja na kututawala, lakini waliogopa kuzitumia ovyo kwani walikuwa na moyo na sura ya haya katika kuzitapanya.


Naandika barua hii nikijaribu kufanya tathmini ninayoiona baada ya miaka michache ya kupata Uhuru – miaka 50 na ushei ya kujitawala, ambayo tulipigania Uhuru wa kuzishika mali zetu na kuzitumia kwa faida ya Watanzania wenyewe badala ya mkoloni.

 

Napata kigugumizi kusema kuwa huenda tukawa tuna wakoloni wenye rangi nyeusi, ambao ni wabaya zaidi kuliko wale wenye rangi nyeupe tuliowafukuza wakaondoka bila mali zetu kuzitapanya. Wakoloni hawa wa mamboleo wanaweza wakawa wanawatumia wazalendo katika kulitaifisha Taifa, wazalendo wasio na moyo wa huruma wala mtazamo wa kesho juu ya kizazi kijacho. Wakoloni wasio waadilifu na dhamana tunayowapatia ya kushika kilicho chetu.

 

Nimeamua kuandika barua hii nikijaribu kujiuliza maswali machache ya kipumbavu kama kawaida yangu. Najiuliza juu ya uhifadhi wa mbuga zetu za wanyama na miti ya asili, hivi ni kweli kwamba bado tunazimiliki kama Watanzania ama zinamilikiwa na watu, au kampuni nyingine kwa niaba ya Watanzania?

 

Taifa limeshindwa nini kushika hatamu ya vivutio hivyo kwa faida ya wote, najiuliza viwanda vilivyokuwa vikiitwa ni vya umma leo hii viko mikononi mwa nani kama si hao wanaoitwa wawekezaji? Je, utendaji wake umeimarika kwa kiasi gani tangu tulipovitoa kwao kwa kigezo hicho? Hawa wawekezaji wamekuwa bora zaidi kuliko Watanzania walioamua kuvianzisha na kutoa ajira kwa wazalendo wenzao?

 

Tufike mbali zaidi. Tujiulize kuhusu mambo mengine kama ya elimu. Hivi leo elimu inayotolewa ni bora zaidi ya ile ya kikoloni ambayo ilikuwa ikiitwa elimu ya Cambridge? Na ni bora zaidi kuliko ile tuliyoamua baada ya Uhuru ambayo mtaala wake ulikuwa na elimu ya kujitegemea?

 

Tuangalie katika vitu vidogovidogo kama umiliki wa hoteli zetu zilizokuwa za umma, kama ambavyo mnaweza kukumbuka zile zilizokuwa zinamilikiwa na usafiri wa reli kila mkoa, leo ziko wapi katika maendeleo ya kidotcom?

 

Sitaki kuzungumzia maeneo ambayo leo hii yamepandishwa bendera za mataifa ya nje ndani ya ardhi ya nchi huru ya Tanzania, uanzishwaji wa kampuni zinazovuna mali ya Tanzania kwa kigezo cha sisi kushindwa kuzisimamia kama madini na kadhalika.

 

Nahisi kushindwa kuwa na wazalendo wenye mamlaka ya kusema “sasa hapana hatuutaki umaskini baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania yetu”, kuwa na watu wenye msimamo kama wa Julius wa kusema kitu kwa dhati ya moyo wake kwamba hilo haliwezekani.

 

Naomba leo niwe mganga wa kienyeji ambaye naitabiria vizuri Tanzania kuwa nchi maskini zaidi katika miaka michache ijayo, Tanzania ambayo sisi tutakuwa wote tumekufa lakini tukiwa na dhambi ya kukitesa kizazi chenu kwa uamuzi wetu wa kushirikishwa na wakoloni mamboleo.

Wasaalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.


By Jamhuri