Naanza na salamu. Salamu ni uungwana wa kawaida kwa muungwana yeyote ili aweze kuwasiliana na mwenzake, maisha ya kuishi kila mtu akimuona mwenzake ni adui si maisha mazuri na kupishana kwa itikadi hakutufanyi tuwe maadui na kukubali matokeo ya walio wengi ni jambo la busara katika ulimwengu wa siasa za ushindani.

Nimeamua leo kumaliza barua yangu mapema sana kabla ya kuongea mambo mengine kwa sababu Waswahili wanasema “…mwazima baiskeli huazima baiskeli hali chakula.” Kwa hoja hiyo, nimemaliza waraka wangu mapema na kwa wale ambao hawajanielewa naweza kuanza kueleza kwa kina na kinagaubaga.

Katika maisha ya kawaida ni lazima siasa iingie mahali popote, ni lazima tuishi kwa sababu kuna siasa, bila siasa hakuna maisha kwa sababu tutaishi bila kuwa na mwongozo, mataifa yaliyovuruga utaratibu wa siasa yamejikuta katika ugomvi mkubwa na kusababisha vifo vingi na uhamaji wa wananchi wa taifa hilo na kuwa wakimbizi, siasa ni muhimu kwa taifa lolote lenye kutaka kuwa na amani na maendeleo.

Taifa letu lilianza siasa miaka ile ya vyama vya wafanyakazi wa kikoloni, vyama vile ndivyo vilivyotia chachandu ya kuanza kufikiria juu ya kutafuta uhuru na kujitegemea kama taifa, wafanyakazi wale walilelewa katika misingi ya kuunda umoja ambao unawafanya wawe na sauti ya pamoja katika jambo fulani.

Umoja ule uliongozwa na makubaliano ya mambo mengi, ambayo kimsingi mambo yale ndiyo yaliyozaa kitu kilichoitwa katiba, katiba ile ndiyo iliyofanya kazi ya kuwaunganisha wapigania uhuru na kuwa na mwongozo wa pamoja katika mambo mengi ya kudai uhuru, moja kati ya mambo hayo ni kuchaguana kuwa viongozi na muda wa uongozi ikiwa ni pamoja na maadili ya uongozi.

Taifa letu likapata uhuru bila ya kumwaga damu, ni jambo la heri ambalo tunapaswa kulienzi hata kama kuna watu wengine wanadhani ni jambo la kubeza. Uhuru ule tuliutaka ili tuweze kuwa na maamuzi yetu wenyewe na tujenge taifa letu wenyewe. Kwa ufupi tumiliki amani yetu na rasilimali zetu.

Taifa lilifanya mabadiliko mengi sana baada ya kupata uhuru, yapo yanayofananishwa na kumwaga damu lakini ukweli ni kwamba ulikuwa ni uamuzi wa wengi na kama tulivyokubaliana kabla ya uhuru ni mambo gani tutayafanya kwa mustakabali wa taifa, lilipita Azimio la Arusha na Operesheni Sogeza kama mambo muhimu kwa taifa ili kujiletea maendeleo.

Haya mambo makubwa mawili yalifanyika ili kuleta maendeleo, lakini wapo ambao walikataa kwa manufaa yao wenyewe kwa nia ya kulinda masilahi yao, lakini kwa kuwa walikuwa wachache, basi wengi walinufaika na kurudisha mali za umma uliokuwa umetawaliwa kwa maana ya Azimio la Arusha. Pili, kuleta maendeleo kwa wananchi waliokuwa pamoja, huduma za msingi zilitufanya tukae pamoja hata kama nguvu ilitumika ili kukamilisha azima ya serikali yetu iliyokuwa ikitumia ilani ya chama kilichotupa uhuru.

Leo tupo kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa, kuna vitu vingi tumejifunza ndani ya taifa letu na kutoka nje ya taifa letu. Kimoja na kikubwa zaidi ni demokrasia ya kuongea sera mbadala kutoka kwa wengine ili uweze kupewa fursa na kuongoza pamoja na kuwa na wanachama.

Kabla ya ukoloni na kabla taifa halijajaliwa wasomi wengi, tuliweza kuweka misingi imara ya chama chetu, kwamba chama kinatakiwa kisiwe kinatenga watu na itikadi zao za dini, kabila, rika na maeneo, ndiyo maana chama kilikuwa kipo Kusini hadi Kaskazini, chama cha mfumo wa kizamani kilikuwa na wanachama Mashariki hadi Magharibi mwa nchi yetu.

Leo tupo katika mfumo huu ambao kila mtu anaona na kusoma sera za vyama mbalimbali, tupo katika mfumo wa kuwa na wasomi wengi wenye kuweza kufikiria na kuona sera mbadala za vyama mbalimbali, tupo kwenye hatua ambayo tunaweza kuiangalia dunia kiganjani na kuona wengine wamefikia wapi kwa kuwa na vyama vingi.

Naamini siasa ni mfumo unaokubalika kuongoza watu kwa ridhaa yao, ni mfumo unaochaguliwa na wengi, kwa hiyo dhana ya kueleza sera zako ni dhana ya kutaka kukubalika. Ni vema wanachama ambao ndio wapiga kura tukajipa muda wa kuchagua sera badala ya matusi, tukachagua chama cha nchi badala ya vile vinavyopinga baadhi ya itikadi.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

303 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!