Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuhimiza urasimishaji wa vikundi vya huduma ndogo za fedha (VICOBA) kama njia ya kuhakikisha usalama wa fedha na uwazi wa shughuli za vikundi.
Wataalamu wa benki hiyo wameeleza kuwa urasimishaji unaweza kuongeza imani ya wanachama na kutoa ulinzi wa kisheria pale panapojitokeza changamoto au migogoro ndani ya vikundi.
Meneja Usimamizi wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa BoT, Dickson Gama, ameeleza kuwa licha ya VICOBA kuwa chanzo kikubwa cha mitaji kwa wananchi wa kipato cha chini, bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto za usimamizi na ukosefu wa uwazi.

Akizungumza leo November 20,2025 Jijini Dodoma amesema baadhi ya vikundi vimekuwa vikikosa kurasimishwa kwa muda mrefu, jambo ambalo limeathiri uaminifu wa wanachama na kupelekea malalamiko kuhusu matumizi yasiyoeleweka ya fedha na upendeleo katika utoaji mikopo.
Aidha, Gama amebainisha kuwa ukosefu wa uwazi wa baadhi ya viongozi umechangiwa na hali ambapo maamuzi mengi hufanywa bila kushirikisha wanachama, jambo linalosababisha migogoro na kudhoofisha misingi ya kisheria na kijamii ndani ya vikundi.
Amesema hali hii imekuwa kikwazo kwa wananchi wanaotegemea VICOBA kama njia ya kujikwamua kiuchumi.
Pia, ameeleza kuwa ukosefu wa takwimu sahihi na uhaba wa taarifa unazidisha changamoto za usimamizi, huku ukizuia wadhibiti na serikali za mitaa kufanya tathmini sahihi kuhusu maendeleo ya vikundi.
Gama amesema kuwa hali hii inaweza kudhoofisha usalama wa fedha zinazotegemewa na kaya nyingi nchini.
Licha ya hayo amefafanua kuwa Serikali kupitia TAMISEMI imepewa jukumu la kusimamia mchakato wa urasimishaji, ikiwa ni pamoja na kupokea maombi kupitia mfumo wa WEZESHA PORTAL, kutunza rejista ya vikundi vilivyosajiliwa na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
Amesema hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha uwajibikaji, uwazi na ulinzi wa wanachama.
Amesema kanuni zinazoongoza sekta hiyo zinataka vikundi vipya kuwa na wanachama kati ya 10 hadi 50, kufanya mkutano wa awali wa kuchagua kamati ya muda, na kuendesha mkutano wa uanzishaji chini ya afisa aliyeidhinishwa.
Amebainisha kuwa taratibu hizi zinalenga kuhakikisha vikundi vinajengwa kwa msingi imara wa uongozi na weledi kabla ya kuanza kufanya shughuli rasmi.

Kulingana na hayo amesema BoT imeweka sharti kwamba maombi ya usajili yanapaswa kuambatana na nyaraka muhimu ikiwemo katiba, orodha ya wanachama, mihtasari ya mikutano, majina ya viongozi na barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa.
Amesema maombi huchakatwa ndani ya siku 14 na vikundi vinavyokosa kufuata masharti hayo vinaweza kukataliwa hadi kitakapokidhi vigezo vyote.
“Baada ya kusajiliwa, vikundi vinatakiwa kuanza shughuli ndani ya miezi mitatu, kuwa na ofisi rasmi, kufungua akaunti ya benki, kutunza rekodi sahihi za fedha na kuwasilisha taarifa za robo mwaka, ” amesema.
Gama amebainisha kuwa BoT na TAMISEMI pia wana mamlaka ya kufanya ukaguzi wa ghafla ili kulinda maslahi ya wanachama na kuzuia matumizi mabaya ya fedha na kwamba lengo la hatua hizo ni kuhakikisha sekta ya VICOBA inakuwa imara, salama na yenye manufaa kwa wananchi wanaotegemea mfumo huo.


