Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Katika hatua ya Tanzania kuendelea kujiimarisha kama kitovu cha uwekezaji wa kimkakati barani Afrika, Serikali kupitia wizara ya madini imekaribisha uwekezaji wa Kampuni kutoka Korea Kusini kuja kuwekeza nchini na kueleza uwepo wa fursa katika utafiti wa madini, uongezaji thamani pamoja teknolojia za kisasa za uchimbaji na uchakataji madini hususan madini muhimu na mkakati.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, Amesema hayo Januari 28, 2026 Jijini Dodoma wakati akizungumza na ujumbe kutoka Korea Kusini ukijumuisha Shirika la Kukuza Biashara na Uwekezaji la Jamhuri ya Korea (Korea Trade-Investment Promotion Agency – KOTRA) na Kampuni ya HD Construction Equipment kutoka nchini Korea Kusini inayojihusisha na utengenezaji wa vifaa na teknolojia ya uchimbaji na viwanda.
Mbibo alisisitiza kuwa Sera na maboresho ya kisheria yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania katika Sekta ya Madini yamelenga kuvutia mitaji yenye teknolojia, maarifa, na mtazamo wa muda mrefu, hasa katika uchakataji wa madini ndani ya nchi, ujenzi wa viwanda, na uhamishaji wa teknolojia za kisasa.
“Tanzania iko tayari kwa ubia wa kimkakati unaoongeza ajira, mapato ya ndani, na ushindani wa kimataifa. Tunakaribisha wawekezaji wanaoleta suluhisho za kisasa kwenye mnyororo mzima wa thamani wa madini, kuanzia utafiti wa madini hadi uongezaji thamani madini ndani ya nchi, hususan eneo la madini muhimu na mkakati” alieleza Mbibo.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi na Kamishna wa Biashara wa KOTRA Ofisi ya Dar es Salaam Kim Sangwoo, alibainisha kuwa Korea Kusini ina nia ya kuongeza uwekezaji wake Afrika Mashariki kupitia miradi yenye tija na uwajibikaji na Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye mazingira mazuri ya uwekezaji.
Naye, Meneja Mkuu wa Kampuni HD Construction Equipment Soohong Min, alisema kuwa kampuni za Korea zina uzoefu mkubwa katika teknolojia za uchimbaji, vifaa vizito vya kisasa, na mifumo ya uzalishaji yenye ufanisi na uwezo unaoweza kuharakisha ajenda ya Tanzania ya uongezaji thamani wa madini.
Majadiliano hayo yaligusa maeneo muhimu ikiwemo utafiti wa kina wa madini kwa kutumia teknolojia za kisasa, uchakataji na uongezaji thamani, ujenzi wa viwanda na miundombinu ya uzalishaji na uhamishaji wa teknolojia kwa wataalamu wa ndani.
Kwa kuhitimisha, pande zote zilionesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiteknolojia, huku Tanzania ikiweka wazi mlango kwa wawekezaji wanaoendana na dira ya maendeleo jumuishi na endelevu kwa manufaa ya kiuchumi, teknolojia na kijamii.
KOTRA ni Shirika la Serikali ya Korea Kusini, lililoanzishwa mwaka 1962, linalohimiza biashara ya kimataifa na uwekezaji wa kigeni. KOTRA huunganisha kampuni za kimataifa na washirika wa Korea, ikitoa taarifa za soko na usaidizi wa kiutendaji kupitia ofisi zake duniani kote ikiwemo iliyoko Dar es Salaam.






