Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi wa Wasafi Media, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, ameipongeza Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kwa utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, huku akiahidi kuwa tayari kufuata matakwa yote ya kisheria yanayohusu sekta ya habari na watumishi wake.

Akizungumza baada ya kufika katika ofisi za Bodi hiyo kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria, Diamond amesema Wasafi Media haina nia ya kukwepa utekelezaji wa Sheria, bali iko tayari kushirikiana kikamilifu na wasimamizi wa taaluma hiyo.

Amesema licha ya Sheria ya Huduma za Habari kuathiri vyombo vya habari kwa namna moja au nyingine, haiwezi kupingwa kwani ilitoa muda wa kutosha kwa wadau kujipanga na kutimiza vigezo vilivyowekwa ikiwemo Waandishi wake kuwa na kiwango cha Elimu cha Diploma na kuendelea.

Diamond amekiri kuwa ujio wa Bodi ya Ithibati umeleta nidhamu kubwa katika taaluma ya habari, akisisitiza kuwa Wasafi Media inaunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha weledi, maadili na uwajibikaji vinazingatiwa.

“Sisi hatutaki kukwepa utekelezaji wa Sheria. Hakuna namna unaweza kuvunja Sheria na ukabaki salama, tumehakikisha uzingatiaji wa Sheria kwa watumishi wetu wote na katika hilo sina utani” amesema Diamond.

Aidha, amesema awali alipata taarifa na maelezo tofauti kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, lakini baada ya kufika Bodi na kupewa ufafanuzi wa kina, ameelewa vyema dhamira ya Serikali ya kuimarisha taaluma hiyo na kwamba imeonesha uvumilivu mkubwa kwa kutoa kipindi cha mpito cha kutosha kwa waandishi na taasisi husika.

Amepongeza msimamo wa Waziri mwenye dhamana aliyebainisha kuwa Bodi ni mlezi wa waandishi, akisema amejiridhisha yeye mwenyewe baada ya kufika katika ofisi hizo kuwa ni kweli Bodi ipo kwa ajili ya kulinda taaluma, si kuibana.

“Nakiri wazi kuwa Bodi ni mlezi kwa waandishi. Baada ya kuielewa vizuri Sheria, hakuna sababu ya kupingana nayo. Watu wangu tayari wamechukua hatua na wamerejea vyuoni,” amesema Diamond, akisisitiza umuhimu wa mawasiliano mazuri kati ya wadau wa habari na wasimamizi wa Sheria.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati, Wakili Patrick Kipangula, amesema Sheria ya Huduma za Habari ilitungwa mwaka 2016 na ilitolewa kipindi cha mpito cha miaka mitano, kikaongezwa miaka miwili na baadaye kupita miaka mingine mitatu, hivyo kufikisha jumla ya miaka kumi.

Amesema Serikali inaamini kuwa muda huo ulikuwa wa kutosha kwa waandishi na wadau wote wa sekta ya habari kutimiza vigezo vya kisheria, hatua inayolenga kujenga taaluma yenye weledi, maadili na heshima.