Rais Samia atunukiwa Tuzo Maalum ya Kiongozi Mwenye Maono

● Watalii wa kimataifa wafikia zaidi ya milioni 2.09 mwaka 2026

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameibuka kinara wa Tuzo za Kitaifa za Uhifadhi na Utalii (Serengeti Awards) kutokana na uongozi wake bora na wa kimkakati katika kukuza sekta ya Maliasili na Utalii kupitia jitihada zake za kutangaza vivutio vya Tanzania kimataifa.

Katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Kitaifa za Uhifadhi na Utalii (Serengeti Awards) iliyofanyika leo Januari 31, 2026 katika Ukumbi wa Mount Meru Hotel jijini Arusha, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitunukiwa Tuzo Maalum ya Kiongozi Mwenye Maono (Visionary Leadership Award) kwa mchango wake mkubwa katika kukuza utalii na uhifadhi wa maliasili, hususan kupitia filamu za Tanzania The Royal Tour na Amazing Tanzania, pamoja na juhudi zake za kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utalii na kuimarisha uhifadhi. Tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba yake na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba alisema jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita zimezaa matunda ambapo idadi ya watalii wa kimataifa imefikia 2,097,823 kati ya Januari hadi Novemba 2025, sawa na ongezeko la takribani asilimia 9.02 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa sekta ya Maliasili na Utalii inachangia takribani asilimia 21 ya Pato la Taifa, ikiwemo asilimia 17 kutoka utalii na asilimia 4 kutoka misitu na nyuki, sambamba na kutoa ajira kwa takribani watu milioni 3.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti uliowezesha kuimarika kwa uhifadhi, ujenzi wa barabara na viwanja vya ndege katika maeneo ya hifadhi, hatua ambazo zimerahisisha shughuli za utalii na kuongeza mvuto wa Tanzania kimataifa.

Aidha, hafla hiyo ilihudhuriwa na shabiki wa klabu ya Manchester City ya Uingereza, Braydon Bent, ambaye alieleza kuvutiwa na uzuri wa vivutio vya Tanzania ikiwemo Serengeti na Ngorongoro pamoja na ukarimu wa wananchi, akisema safari hiyo itabaki kuwa kumbukumbu isiyosahaulika maishani mwake.

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, kulinda mazingira, kuhakikisha wananchi wanaozunguka hifadhi wananufaika kiuchumi, pamoja na kuendeleza ubunifu na matumizi ya teknolojia ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa la utalii. 

Waziri Mkuu, alimalizia kwa kuwakumbusha Watanzania kuwa amani ni tunu kuu ya Taifa na ni wajibu wa kila mmoja kulinda rasilimali zilizopo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.