Na Mwandishi Wetu, Songea

MAHAKAMA kuu kanda ya Songea,imefanikiwa kumaliza kusikiliza mashauri 19 ya kimkakati sawa na asilimia 86 yanayohusu kodi,biashara,benki na ardhi kati ya 22 yaliyofikishwa mahakamani mwaka 2025.

Hayo yamesemwa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Songea James Karayemaha,wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini ambayo mkoani Ruvuma yamefanyika katika viwanja vya Mahakama kuu mjini Songea.

Alisema,kumalizika kwa mashauri hayo imesaidia kufungua shughuli za kiuchumi zilizokuwa zimesimama kutokana na uwepo wa mashauri hayo mahakamani,hivyo kuchangia ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa.

Alisema,maendeleo ya Taifa ni mchakato wa kuboresha hali ya maisha ya wananchi wote kwa njia endelevu yanayohusu maendeleo katika Nyanja mbalimbali ili kuleta ustawi wa Taifa.

Alisema,maendeleo hayo yanaweza kuonekana kutokana na ongezeko la kipato,ajira,uzalishaji na kuimarika kwa uchumi wan chi,elimu bora,afya,usawa,haki,utawala bora,amani na usalama na ushiriki wa wananchi kwenye kazi za maendeleo.

Jaji Karayemaha alisema,mahakama kanda ya Songea inaendelea kuboresha upatikanaji wa haki kwa kuongeza huduma za mahakama za mwanzo kupitia uanzishwaji wa mahakama za mwanzo karibu na wananchi.

Alisema,lengo la mkakati huo ni kupunguza umbali kufuata huduma za haki na kuhakikisha upatikanaji wa huduma hizo kwa gharama nafuu na kwa wakati na katika kanda ya Songea mahakama ipo hatua ya mwisho za ujenzi
wa mahakama mpya katika eneo la Msamala na Lilondo Wilaya ya Songea.

Kwa mujibu wa Jaji Karayemaha, awali wananchi wa maeneo hayo walipaswa kusafiri umbali mrefu ili kupata huduma za mahakama na ujenzi wa mahakama hizo utasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi.

“vituo kama Namasakata,Lukumbule,Magazini na Ligera ambavyo vilisimama kwa muda mrefu bila kufanya kazi vyote vimefunguliwa na wananchi wa maeneo hayo hawasafiri umbali mrefu kutafuta haki kama ilivyokuwa zamani”alisema.

Aidha alisema,matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wajibu wa utoaji haki umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuboresha huduma za mahakama na kuongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri katika kanda ya Songea.

Jaji Karayemaha,amewataka wadau wa mahakama kushauri kwa hekima na kutoa ushirikiano kwa kuwa kufanya vizuri kwa mahakama ni kufanya vizuri kwa wadau wote na dola zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas amewapongeza mahakimu na majaji wa mahakama kuu kanda ya Songea kwa kazi nzuri wanayofanya katika kusimamia na kutoa haki kwa jamii bila kuangalia sura ya mtu.

Alisema,mahakama ina jukumu kubwa la kusimamia suala la utoaji haki kwa wananchi bila kubagua na kuwataka kuendelea kutoa na kusimamia haki bila upendeleo kwani hatua hiyo itasaidia sana watu wengi hasa wanyonge kutumia mahakama kwa ajili ya kutafuta haki.

Wakili wa serikali mfawidhi Mkoa wa Ruvuma Egidy Mkolwe,amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua Madhubuti anazoendelea kuchukua katika kushughulikia changamoto zilizojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa Mwezi Oktoba 29 mwaka 2025.

Alisema,kuundwa kwa tume ya uchunguzi itaweka msingi wa maridhiano ya Kitaifa na hatua hiyo ni msingi muhimu katika kujenga na kudumisha umoja na mshikamo wa kitaifa,kurejea kwa amani ya wananchi kwa taasisi za dol ana kuimarisha mazingira ya haki,amani na utulivu.

Naye mwenyekiti wa Chama cha wanasheria Tanganyika(TLS)Mkoa wa Ruvuma Elisius Ndunguru alisema,Taifa linapokuwa kwenye mfumo wa utaoji haki bila upendeleo au ukandamizaji usaidia kuharakisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na nchi.