*Lissu akiwa gerezani, misimamo kuhusu haki, ushiriki wake yapima juhudi za wadau
*Tume yataka mazungumzo yenye kujenga, kuheshimiana na njia za kikatiba
*Uingereza yahimiza kurejesha kuaminiana, Serikali yatetea mahakama, CHADEMA yaweka madai
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
NA MWANDISHI WETU
Milango ya mazungumzo inatajwa, lakini funguo zake zinabishaniwa. Lissu akiwa gerezani huku mawakili wake wakiandaa rufaa, juhudi za kurejesha kuaminiana nchini zinaendelea; JAMHURI linaripoti.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameanza kutumikia kifungo cha miaka minne jela baada ya kukutwa na hatia ya kosa la uchochezi; nyuma yake kumetolewa mwito wa kukaa pamoja kutafuta suluhu inayoheshimu haki, sheria na umoja wa kitaifa.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imezitaka taasisi za umma, vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia na wananchi kuendeleza mazungumzo yenye kujenga, huku tofauti kuhusu hukumu ya Lissu zikiongeza mjadala ndani na nje ya nchi.
Katika tamko la Novemba 13, mwaka huu, Tume imeweka sakata hilo katika mazingira mapana ya haki, usawa mbele ya sheria, ushiriki wa kidemokrasia na kuishi pamoja kwa amani.
Mwelekeo huo unatoa msingi wa kuendeleza juhudi za maridhiano bila kuziondolea mahakama mamlaka yake au kuyafunika malalamiko yanayohitaji majibu.
“Tofauti za maoni kuhusu uamuzi wa mahakama na masuala yenye maslahi kwa umma zinapaswa kushughulikiwa kupitia njia halali, za kikatiba na kidemokrasia,” inasomeka sehemu ya ripoti ya Tume iliyosainiwa na Mwenyekiti wa THBUB, Dunford Mpelumbe.
Mwito huo umekuja baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, Novemba 6 mwaka huu, kumwachia huru Lissu katika shtaka la uhaini, lakini ikamtia hatiani kwa kosa la uchochezi na kumhukumu kifungo cha miaka minne.
KWA HABARI ZAIDI ZA KINA SOMA JAMHURI LA NOVEMBA 17 -23, 20206



