Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Unguja

Majengo yaliyowapa makazi Wazanzibari kwa miongo kadhaa, sasa yamewekwa kwenye mpango wa kubomolewa na kujengwa upya; JAMHURI linaripoti.

Ni majengo ya eneo maarufu la Michenzani yaliyochukuliwa na wengi kama ‘alama’ miongoni mwa nembo za Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mapinduzi Zanzibar, chini ya Sheikh Abeid Amani Karume.

Uamuzi wa kuyavunja na kuyajenga upya unakutanisha hoja za usalama wa maisha, haki za wakazi na uhifadhi wa historia ya visiwa hivyo.

Kwa upande mmoja Serikali ya Zanzibar inasema nyumba hizo zimechakaa na zinahatarisha maisha; wakati Balozi Ali Abeid Karume anaonya akisema kuzibomoa kunapaswa kutanguliwa na uchunguzi wa kitaalamu, mipango inayoeleweka na uhakika wa wenye haki kupata stahiki zao.

Balozi Karume ni mtoto wa Sheikh Karume.

Mbali na Michenzani, makazi mengine ya Wazanzibari yaliyojengwa baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, yapo Kilimani na Kikwajuni; maeneo ambayo ni sehemu ya historia ya maendeleo ya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, ametangaza mpango wa kujenga upya makazi hayo, akisema serikali haitasubiri majengo yaporomoke na kusababisha vifo ndipo ichukue hatua.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mauzo ya nyumba za mradi wa Saateni, Unguja, Rais Mwinyi amesema makazi bora ni sehemu ya ustawi wa wananchi na maendeleo ya uchumi.

“Nyumba hizi zilijengwa miaka 60 iliyopita. Muda wake wa matumizi umekwisha, hazifai tena kwa makazi na zinahatarisha maisha ya watu. Serikali imeamua kuzijenga upya zote,” amesema.

Mradi wa Saateni unatarajiwa kuwa na nyumba 209, pamoja na maeneo ya biashara, huduma za kijamii na maegesho ya magari.

Mpango wa serikali unakwenda mbali zaidi ya eneo moja. Rais Mwinyi amesema:

“Tulianza Kikwajuni, sasa tupo Saateni, na tutaendelea Michenzani, Kilimani na maeneo ya vijijini. Hakuna eneo la makazi ya serikali litakaloachwa nyuma.”

Hata hivyo, tamko la kujenga upya linaibua suala la namna ya kushughulikia wakazi wenye hadhi tofauti; wapangaji wa nyumba za serikali, wenye nyumba binafsi na familia zilizopata makazi kutokana na mipango ya fidia ya zamani.

KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA JAMHURI NOVEMBA 17 – 23, 2026