Na Veronica Mrema, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Umri wa miezi minane alipofikia, aligundulika ana ugonjwa wa siko seli (selimundu) na ameishi nao kwa miaka 39, miaka yake imebeba mengi yasiyoweza kuonekana kwa majibu ya kipimo cha damu pekee.
Ni maisha ya mtu aliyekua akiufahamu ugonjwa huu kwa karibu, kabla baadaye uzoefu wake haujageuka kuwa sehemu ya kupambana na siko seli hapa nchini Tanzania.
Ni miaka 18 sasa tangu alipoanza harakati hizo, Arafa Said, bado anamtazama kwa ‘jicho la tatu’ mtoto anayezaliwa leo akiwa na siko seli huku pia kukiwa na kundi kubwa la watu wasiojua hali zao.
Je, mtoto huyo atalazimika kukua akikabili vikwazo vilevile kwa mfano unyanyapaa, gharama za matibabu na changamoto nyingine, kwa sababu anaishi na siko seli?
Je, Tanzania inaweza kuweka mfumo bora zaidi kwa mtoto mwenye siko seli kupata huduma bora na stahiki bila kikwazo chochote, ikiwamo cha kifedha au umbali wa kufuata huduma?
Arafa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Siko Seli Tanzania (SCDPCT).
Anasema anatamani kuona mtoto aliyezaliwa na siko seli anapata huduma bora na anaishi vema hadi kuzifikia ndoto zake.
Kwa mwaka huu pekee, SCDPCT kwa kushirikiana na wadau wengine imewakatia bima ya afya zaidi ya watoto 30.
Idadi hiyo si suluhisho la changamoto yote, lakini kwake inaonyesha jambo moja kwamba mtoto anayeishi na siko seli hawezi kupewa nafasi ya kuishi vizuri kwa kumtambua tu kuwa ana ugonjwa.
“Mtoto asipate shida au asishindwe kupata huduma kwa kukosa fedha. Kwa familia yenye kipato duni, gharama haianzi hospitalini. Kuna nauli ya kufika kituoni na gharama za vipimo.
“Kulazwa inapohitajika na mahitaji mengine yanayoweza kujitokeza katika maisha ya mtoto anayehitaji huduma mara kwa mara. Kwa familia ambazo kipato kipo chini au duni, gharama za usafiri, vipimo na kulazwa ni mzigo,” anasema Arafa.
Kutokana na hali hiyo, SCDPCT inataka huduma zisogezwe karibu na watu lakini pia mfumo wa bima uangalie kwa namna ya pekee mahitaji ya wanaoishi na siko seli.
Kwa mtoto, changamoto hiyo inaweza kuwa na madhara yanayokwenda mbali zaidi ya siku akikosa huduma.
Anaweza kukosa shule, familia kutumia kipato chake katika matibabu badala ya mahitaji mengine au mzazi kushindwa kumudu gharama zinazohitajika ili mtoto aendelee kupata huduma.
Katika sehemu zilizopita za safari hii, watoto na familia zao wameeleza namna siko seli inavyogusa maisha yao.
Kwa Arafa, mtoto hatakiwi kuachwa nyuma kwa sababu tu amezaliwa katika familia yenye kipato kidogo. Ndiyo maana anasisitiza umuhimu wa watoto kutambuliwa mapema.
“Ushauri wangu kwa ujumla, tukianza na serikali, umefika muda sasa tuweze kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa Tanzania anapima siko seli na kuanza matibabu,” anasema.
Mratibu wa Siko Seli wa Wizara ya Afya, Dk. Asteria Mpoto, anasema serikali nayo inaangalia suala hilo katika muktadha mpana wa upatikanaji wa huduma na bima.
Anasema baada ya kuzinduliwa kwa Bima ya Afya kwa Wote, serikali inaamini kila Mtanzania anayehitaji huduma ataipata kwa usawa.
Anataja upandikizaji wa uloto kuwa mfano wa huduma ambayo bado ni ghali, kwa sababu ni mpya nchini na inahitaji wataalamu wenye utaalamu maalumu.
Anasema Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC sasa nayo ipo katika hatua za kuanzisha huduma hiyo, huku akieleza kuwa huenda vituo vingine kama Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) vikapanua huduma hiyo kadiri uwezo unavyoongezeka.
Kwa mtazamo wake, upanuzi wa huduma unaweza pia kusaidia kushusha gharama.
Anatoa mfano wa hydroxyurea, anasema awali ilikuwa na gharama kubwa lakini sasa inapatikana katika vituo vya kutolea huduma na gharama yake imepungua kwa kiasi.

Pia anasema serikali imeanza kuangalia makundi yenye ushawishi mkubwa katika jamii, wakiwamo vijana, viongozi wa dini, waandishi wa habari na walimu.
Kwa vijana, anasema lengo ni kuwafanya wafahamu hali zao kabla ya kuanzisha familia. Kwa viongozi wa dini, anasema ni kuwapa nafasi ya kusaidia kuondoa imani potofu na kutoa elimu wakati wa maandalizi ya ndoa.
Vilevile anasema waandishi wa habari wamefikiwa katika mikoa 17, huku walimu hasa wanaofundisha afya katika shule za msingi, wakitazamwa kama sehemu muhimu ya kuwafikia watoto wakiwa shuleni.
Hata vijana wanaopita katika mafunzo ya kijeshi, anasema wameanza kufikiwa kwa kushirikiano na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Mwaka 2025, vijana 30,000 walifikiwa na mwaka huu zaidi ya 34,000 wamefikiwa huku idadi inayofikiwa kwa mwaka ikiwa kati ya 30,000 na 50,000.
Katika hatua nyingine, anasema serikali imeendelea kuongeza uwezo wa kutambua siko seli na mwaka 2019 kulikuwa na hospitali nane zenye uwezo wa kutambua ugonjwa huo.
Kwa sasa, anasema hospitali zaidi ya 100 zinaweza kutambua na kutoa huduma zikiwamo 28 za mikoa, hospitali zote sita za kanda, MNH pamoja na baadhi ya hospitali za halmashauri na vituo vya afya.
Anasema Tanzania imeona makadirio ya watoto wanaozaliwa na siko seli yakifika 14,000 kwa mwaka kutoka 8,000 huku sehemu ya ongezeko hilo inahusiana na kuongezeka kwa upimaji na kuwafikia watu ambao awali hawakujitambua huku asilimia 15 hadi 20 ya watu bado hawajitambui hali zao za vinasaba.
Kigoma anasema imetoa mfano wa namna picha ya ugonjwa inaweza kubadilika pale upimaji unapoongezeka kwa kuwa serikali ilifanya upimaji katika hospitali nane za halmashauri za mkoa huo.
Baada ya upimaji, anasema Kigoma ilifika nafasi ya kwanza kwa idadi ya watu waliotambuliwa kuwa na siko seli kutoka nafasi ya tatu.
“Tunamini hata maeneo mengine tunasema hayana wagonjwa wengi, labda ni kwa sababu hatujaweka nguvu ya upimaji. Labda tukiweka tutapata wengi,” anasema.
Anakiri bado kuna makundi hayajafikiwa kikamilifu likiwamo la wataalamu wa tiba asili.
Anasema kitengo cha siko seli bado hakijafanya mazungumzo ya moja kwa moja na wataalamu hao ingawa wizara ina kitengo kinachohusika na tiba asili.
“Siko Seli ni wa kurithi, si kurogwa kama sehemu kubwa ya jamii inavyoamini na kukimbilia kwa waganga wa tiba asili kutafuta matibabu. Hapa tunaona kuna umuhimu wa kukutana nao waganga wa tiba asili kwa sababu watu wanakwenda huko,” anasema.
Pamoja na hatua hii ambayo Tanzania imepanua uwezo wa upimaji, kuongeza vituo
vinavyotambua siko seli na kuingiza huduma katika mfumo mpana wa afya, lakini bado kuna pengo kati ya mtoto anayehitaji huduma na uwezo wa familia yake kuifikia huduma hiyo.

