Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Taifa na Mlezi wa Mkoa wa Pwani, Lailah Burhan Ngozi, amewataka Watanzania kuilinda kwa nguvu zote amani ya Tanzania waliyoachiwa na waasisi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Zanzibar.
Ngozi alitoa wito huo wakati akizindua rasmi maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi za CCM Wilaya ya Kibaha Vijijini, mkoani Pwani.
“Tangu CCM ilipoanzishwa mwaka 1977 baada ya kuunganishwa kwa TANU na ASP, imeendelea kuwa chama tawala kwa kuwa karibu na wananchi kwa vitendo katika kuwaletea maendeleo, kuimarisha umoja, mshikamano na kudumisha amani nchini” alielezea Ngozi.
Kabla ya uzinduzi huo, Ngozi alitembelea wodi ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya cha Mlandizi, ambako amegawa boksi za sabuni za kufulia na zawadi mbalimbali kwa akina mama waliojifungua .
Alitoa rai kwa wahudumu wa kituo hicho cha afya kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa mama na mtoto bila kuweka mbele maslahi binafsi.
Vilevile Ngozi ,alishiriki zoezi la upandaji miti ikiwa ni sehemu ya juhudi za utunzaji wa mazingira.
Uzinduzi wa maadhimisho hayo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama, wanachama pamoja na baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kibaha Vijijini.







