Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Mkuu wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameipongeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani kwa kuiwezesha Serikali kufidiwa kiasi cha sh milioni 707 baada ya kumalizika kwa mashauri nane (8) ya uhujumu uchumi yaliyohusisha uharibifu wa miundombinu ya umeme na reli ya SGR mwaka 2025.
Alitoa pongezi hizo Februari 2, 2026, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kwa Mkoa wa Pwani, yaliyofanyika katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kibaha mkoani humo.
Aidha, aliipongeza Mahakama kwa mchango wake katika kukuza uchumi na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwemo kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kupitia kupunguza migogoro ya ardhi.
Katika hatua nyingine, Kunenge alisisitiza umuhimu wa wananchi pamoja na wadau wa sekta ya sheria kupatiwa elimu kuhusu mabadiliko ya sheria ili waweze kufuatilia na kutatua masuala yao ya kisheria kwa uelewa, “Katika hilo, ametolea mfano marekebisho ya sheria 15 yaliyofanywa na Mahakama.
Aliwataka watendaji wa umma kuzingatia kikamilifu taratibu za kisheria, huku akisisitiza kuwa sheria ndogondogo zinapaswa kuendana na sheria mama.
Kunenge aliongeza kuwa ,Mahakama ihakikishe ushiriki wa wananchi katika matukio mbalimbali yanayoandaliwa ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu mabadiliko ya sheria.
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Pwani, Joyce Mkhoi, alifafanua mashauri yaliyofidiwa ni ya kimkakati yanayohusu masuala ya biashara na uchumi, yaliyohusisha fedha nyingi, na yamefanikiwa kumalizika baada ya Mahakama kuanzisha vikao maalumu vya kuyasikiliza na kuyahitimisha.
Alieleza, kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Mahakama ya Mkoa wa Pwani imesikiliza kesi 152 kwa njia ya runinga (video conference), hatua iliyosaidia kupunguza gharama za uendeshaji na usafirishaji wa mahabusu na wafungwa.
Vilevile, alisema katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, mkakati mmoja muhimu ni kusogeza huduma za kimahakama na wananchi kwa kufungua mahakama katika maeneo yenye msongamano wa watu .







