Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji,  Profesa Kitila  Mkumbo  amesema Tanzania imejipanga kikamilifu kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia mipango thabiti ya muda mrefu, wa kati na mfupi inayolenga kuijenga nchi yenye uchumi jumuishi, ustawi wa wananchi na uwezo wa kujitegemea.

Prof. Mkumbo aliyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu (2026/27–2050/51), Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31) pamoja na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/27.

Alieleza kuwa kwa kipindi cha takribani miaka miwili, kuanzia Aprili 2023 hadi Julai 2025, Serikali ilitekeleza mchakato mpana wa kuandaa dira mpya ya maendeleo kufuatia kukamilika kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2000–2025. 

Alisema mchakato huo uliongozwa na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kukamilika kwake kulipelekea uzinduzi rasmi wa Dira 2050 tarehe 17 Julai 2025.

Kwa mujibu wa Prof. Mkumbo, Dira 2050 itatekelezwa kwa kipindi cha miaka 25 kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 hadi 2050/51, ikiwa na lengo kuu la kuijenga Tanzania kuwa Taifa jumuishi, lenye ustawi, haki na linalojitegemea. 

Alisema,Dira hiyo ina malengo mahususi manne yakiwemo kujenga uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu ulio shindani, jumuishi na himilivu, kuhakikisha maisha bora na ustawi kwa wote,kulinda na kutumia rasilimali za asili kwa uendelevu huku kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuijenga jamii yenye umahiri wa kutumia teknolojia za kidijitali katika kuchochea ubunifu na ushindani wa kimataifa.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya utekelezaji wa dira hiyo, Waziri Mkumbo alisema Serikali imeandaa nyenzo tatu muhimu zitakazotafsiri dira kuwa vitendo. 

Alisema nyenzo hizo ni Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu wa miaka 25, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano utakaotekelezwa katika awamu ya kwanza ya dira, na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/27 unaobainisha vipaumbele vya muda mfupi.

Katika mwelekeo wa uchumi kwa mwaka 2026/27, Waziri alisema Serikali inalenga kukuza Pato Halisi la Taifa hadi kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026 kutoka asilimia 5.9 mwaka 2025, huku likitarajiwa kufikia wastani wa asilimia 6.9 katika kipindi cha muda wa kati.

 Aidha, Serikali inalenga kudhibiti mfumuko wa bei katika wigo wa asilimia 3.0 hadi 5.0, kuongeza mapato ya ndani hadi asilimia 17.1 ya Pato la Taifa, mapato ya kodi kufikia asilimia 13.7, pamoja na kuhakikisha nakisi ya bajeti haizidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa.

Prof. Mkumbo alibainisha kuwa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/27 utazingatia misingi muhimu ikiwemo kudumisha amani, usalama na utulivu, kuimarisha utawala bora na utawala wa sheria, kuendeleza miundombinu ya nishati na usafiri, kuhimiza ubunifu na matumizi ya teknolojia za kidijitali, pamoja na kuimarisha mazingira ya uwekezaji kupitia ushirikiano wa sekta binafsi na wa kikanda.

Katika hitimisho la hotuba yake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais , Mipango na Uwekezaji, alisema changamoto kubwa iliyopo sasa si kupanga mipango bali ni kutafsiri maono ya Dira 2050 kuwa vitendo vinavyoleta matokeo halisi kwa wananchi. 

Alikumbusha msisitizo wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa utekelezaji wa dira hiyo unahitaji mabadiliko ya mtazamo na kufanya kazi kwa namna isiyo ya kawaida ili kufikia malengo makubwa yaliyowekwa na Serikali.

 Prof. Mkumbo alisema, imejipanga kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, tathmini na uwajibikaji ili kuhakikisha programu na miradi ya maendeleo inayopitishwa na Bunge inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayokusudiwa kwa maendeleo ya Taifa.