….Yahamasisha wananchi wawahi kupima

Na Mwandishi Wetu

WATANZANIA wametakiwa kuondokana na dhana kwamba saratani haitibiki na badala yake wawahi hospitalini kupima kila wanapoona dalili mbaya kwani saratani inatibika kama mgonjwa atawahi kupima mapema na kuibaini.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salam na Daktari bingwa wa saratani wa hospitali ya Shifaa iliyoko Kinondoni, Barabara ya Msese, Magreth Moshi, wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya saratani duniani.

Alisema saratani inaweza kutibiwa kama mgonjwa atakuwa na kawaida ya kupima na kugundulika ikiwa katika hatua ya awali badala ya kusubiri mpaka hali inapokuwa mbaya ndipo waende hospitalini.

Alisema kila tarehe 4 ya mwezi wa pili dunia huadhimisha siku ya saratani duniani ambapo elimu hutolewa kwa wananchi kuwahi hospitalini mapema wanapoona dalili mbaya mwilini kama uvimbe usiokuwa wa kawaida.

Alisema utambuzi wa mapema wa ugonjwa wa saratani unatoa ahueni kwa mgonjwa kwani uwezekano wa kupona unakuwa mkubwa zaidi kuliko akichelewa kwenda kufanya vipimo.

“Ukipimwa ukaonekana unadalili za saratani ambayo iko katika hatua za awali nawahakishia watanzania kwamba inatibika tuwahi kupima mapema,” alisema

Alisema mwaka 2024 Hospitali ya Shifaa ilianzisha kitengo cha saratani ambacho kinatoa tiba kemia, chemotherapia na uchunguzi wa sarani kwa ujumla.

Alisema tamwimu zilizoko zinaonyesha kuwa hapa nchini kunakuwa na wagonjwa 40,000 kila mwaka wanaougua ugonjwa huo.

“Tunachowashauri watanzania ni kwamba waishi maisha yenye afya kwa maana kwamba kuacha tabia hatarishi kama kuvuta tumbaku na wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara,” alisema.

Victoria Tarimo ambaye ni Meneja Masoko wa Hospitali hiyo alitoa wito kwa wananchi kufika Shifaa kwaajili ya kufanya uchunguzi wa awali wa saratani.

Alisema hospitali hiyo ilianzisha kitengo maalum cha saratani ambacho kimewekeza kwenye utaalamu na teknolojia ya hali ya juu ya kuchunguza na kutibu maradhi ya saratani.

“Huduma za hapa Shifaa ni za kimataifa, ukija hapa ni kama uko India kwasababu tumesaini ushirikiano na hospitali ya Mumbai kwaajili ya kufanya matibabu ya saratani,” alisema