SERIKALI imetangaza hatua kali za kudhibiti vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanafunzi wanaotumia usafiri wa mabasi ya mijini maarufu kama daladala, huku ikisisitiza kuwa haki ya mwanafunzi kupata elimu kwa usalama haiwezi kuvunjwa na maslahi ya kibiashara.

‎Hayo yamesemwa leo Februari 4,2026 jijini Dodoma na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia video iliyoenea mitandaoni ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Mariana Eric Mirindima wa Shule ya Sekondari Jangwani, aliyewasilisha barua ya kueleza changamoto wanazokumbana nazo wanafunzi wanapotumia daladala.

‎Katika barua hiyo, mwanafunzi huyo alieleza kuwa baadhi ya makondakta wamekuwa wakigoma kuwabeba wanafunzi kwa madai kuwa hawalipi nauli kamili, hali inayowasababisha wanafunzi kusimama vituoni kwa muda mrefu, kuchelewa kufika shuleni au kushindwa kabisa kuhudhuria masomo. Alieleza kuwa hali hiyo inahatarisha usalama wao na kuathiri maendeleo yao ya kitaaluma.

‎ Prof. Mbarawa amempongeza mwanafunzi huyo pamoja na mzazi wake kwa ujasiri wa kutoa taarifa, akieleza kuwa Serikali imeisikiliza sauti ya wanafunzi na itachukua hatua stahiki.

‎“Kwa kufanya hivyo, mwanafunzi huyu ametimiza wajibu wake wa msingi wa kuipa Serikali mrejesho unaopaswa kufanyiwa kazi. Napenda kuwahakikishia kuwa sauti ya wanafunzi imesikilizwa,” amesema Prof. Mbarawa.

‎Waziri huyo amesema Serikali imetoa fursa kwa sekta binafsi kutoa huduma za usafiri wa umma, lakini haitasita kuchukua hatua dhidi ya watoa huduma watakaokiuka Sheria, Kanuni na staha ya utoaji huduma kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla.

‎Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Prof. Mbarawa amesema Serikali imeweka mikakati ya kuboresha usafiri wa wanafunzi mijini ikiwemo kuanzisha mabasi maalumu yaendayo haraka kwa ajili ya wanafunzi nyakati za asubuhi na jioni, pamoja na kutenga mabehewa maalumu ya wanafunzi kwenye treni za mijini hususan jijini Dar es Salaam.

‎Aidha, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa nauli maalumu ya Shilingi 200 kwa wanafunzi katika daladala na mabasi yaendayo haraka, pamoja na kuthibitisha madereva na kusajili makondakta ili kuimarisha nidhamu na uwajibikaji katika sekta ya usafiri wa umma.

‎Prof.Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuharakisha zoezi la usajili wa wahudumu wa usafiri, kuimarisha udhibiti wa nauli za wanafunzi, kutoa elimu kwa watoa huduma na watumia huduma, pamoja na kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya daladala.