……..Yaahidi kuendelea kushirikiana na KHEN kuenzi maono ya Kairuki

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe, amezindua mtambo mpya wa kisasa wa teknolojia ya Laser ambao utasaidia kwenye uchambuzi wa viini tete wakati wa upandikizaji mimba ulioko katika Kituo cha kupandikiza mimba cha Kairuki Green IVF.

Katibu Mkuu alipongeza Mtandao wa Afya na Elimu Kairuki (KHEN) kwa kuanzisha kituo cha upandikizaji mimba na mchango wake wa muda mrefu kwenye sekta ya afya hapa nchini.

Alitoa pongezi hizo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua mtambo huo ulioko kwenye kituo ch Kairuki Green IVF (KGIVF) kilichoko Bunju A jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi wa teknolojia hiyo ya kisasa ulifanyika ikiwa ni kilele cha kumbukizi ya mwanzilishi wa Hospitali ya Kairuki, Chuo Kikuu Karuki na Mtandao wa KHEN, Hayati Profesa Kairuki aliyefariki mwaka 1999 na miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa kituo hichomwaka 2023.

Dk Shelikaghe alisema anafurahi kuona urithi alioucha Profesa Kairuki unaendelezwa tena kwa ufanisi wa hali ya juu na kuahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na KHEN katika kuimarisha sekta ya afya nchini.

“Kazi mnayofanya ni ya serikali, mmetoa mchango mkubwa sana serikali lazima tuwapongeze kwa mchango ambao mmeutoa na mnaendelea kuutoa kwenye sekta ya afya nchini na nawapongeza sana kwa kuendeleza maono ya hayati Profesa Kairuki,” alisema.

“Mtambo huu wa kisasa wa Laser utakuwa na manufaa makubwa sana kwa taifa letu kwasababu utasaidia kuongeza idadi ya watoto, Serikali yenyewe haiwezi kufanya kila kitu kwa hiyo tunapoona watu kama nyinyi mnatusaidia inapendeza sana nawaahidi kuwa tutaendelea kushirikiana,” alisema

“Kupitia mtandao wenu wa KHEN mmeanzisha hospitali, mmeanzisha kiwanda cha dawa, mmeanzisha Chuo Kikuu na Kairuki Green IVF nihatua kubwa sana ya kujivunia na kwa dhati kabisa nawapongeza kwa hatua kubwa,” alisema Dk Shekalaghe

Mkurugenzi wa Kituo cha Kairuki Green IVF, Dk Clementina Kairuki alisema mpaka sasa kituo hicho kimefanikisha kupatikana kwa watoto zaidi ya 140 na wengine wameanza chekechea.

Alisema wameamua kufanya maadhimisho kwenye kituo hicho kama sehemu ya kumuenzi Profesa Kairuki kwani maono yake ndiyo yalisababisha kuanzishwa kwa kituo hicho.

“Mwaka 1990 Hayati Profesa Kairuki na mke wake Kokushubira walikwenda kwenye kongamano la afya nchini Denmark, walivutiwa na huduma kama hii iliyokuwa inatolewa huko kwa hiyo waliporudi wakawa na mawazo ya kuanzisha huduma hii ya upandikizaji mimba, lakini kabla ya kuanzisha huduma hii mwaka 1999 alifariki dunia,” alisema

“Alifariki kabla ya kutimzia hii ndoto yake lakini sisi tuliobaki tulisema lazima tutimize ndoto yake ya kuwa na kituo kama hiki na miaka mitatu iliyopita mwezi wa pili tarehe kama ya leo kikazinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi,” alisema

Alisema tangu kianzishwe kituo hicho wameshapokea wenza ,1,205 na kati ya hao wenza 501, walikuwa na sifa ya kufanyiwa huduma ya upandikizaji mimba lakini walioweza kupewa huduma hiyo ni wenza 205.

Alisema kati ya wenza hao 1,205 asilimia 60 walifanikiwa kupata ujauzito na mpaka sasa wameshafanikisha kupatikana watoto 140 na kwamba kuna wengine bado ni wajawazito na wanatarajia kupata watoto wakati wowote.