📌Wakandarasi watakiwa kuacha maneno, ahadi na michakato wamalize mradi kwa wakati
📌Bilioni 57.3 kupeleka umeme vitongoji 358 mkoani Katavi
📌Ajira kupewa kipaumbele
📍Katavi
Imeelezwa kuwa mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Awamu ya Pili B (HEP 2B) unakwenda kuongeza na kuchocchea uchakataji wa mazao ambayo kwa kiasi kikubwa wananchi wa mkoa wa Katavi wanazalisha mazao katika mkoa huo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko leo tarehe 6 Februari, 2026 mara baada ya kutambulishwa kwake mkandarasi Kampuni ya M/s ETDCO Ltd atakayetekeleza mradi wa HEP 2B wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 358 kwa wakazi zaidi ya 11,536 mkoani Katavi.

“Kwa sasa badala ya kuuza mazao ghafi tutaiza bidhaa, suala hili la kupatikana kwa umeme litakwenda kuipandisha bei za mazao kwa sababu yatachakatwa katika hali nzuri na zitauzwa bidhaa badala ya kuuza malighafi,” Amesema RC. Mrindoko.
Vilevile, ameongeza kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika kupitia mradi wa HEP 2B utakwenda kukuza uchumi, kukuza uwekezaji na kuleta ajira kwa vijana, wanawake, wazee na makundi mbalimbali katika mkoa huo.
“Nimsisitize mkandarasi kujipanga sawasawa uingie kazini kwa miguu yote miwili ukiwa na kasi kubwa kwa sababu wanachohitaji wananchi ni umeme wala sio maneno au ahadi, sio ratiba, sio michakato,” Amesema RC Mrindoko.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Bw. Mussa Muze amesema lengo kuu la utekelezaji wa mradi wa HEP 2B ni kuongeza upatikanaji wa umeme kwa wananchi katika vitongoji vya mkoa wa Katavi na kusaidia maendeleo jumuishi ya kijamii na kiuchumi.

Naye, Msimamizi wa Miradi ya REA mkoa wa Katavi, Mha. Gilbert Furia amesema, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Katavi kushiriki vema katika utekelezaji wa mradi, na kutumia fursa ya kuletewa umeme kuweza kujiinua kiuchumi.
Pia, Mkandarasi kutoka Kampuni ya M/s ETDCO Ltd, Mha. Abdalah Mitenda amemueleza RC Mrindoto kuwa katika mradi huo wakandarasi watapewa kipaumbele kufanya shughuli mbalimbali zitakazokuwa zinafanyika katika mradi huo na kuwataka kuchangamkia fursa.





