Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mipango inayoandaliwa na Serikali inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, viwanda na biashara katika ukanda wa Afrika.

Amesema Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027 – 2030/2031 una dhima ya mageuzi kwa ajili ya ukuaji wa uchumi jumuishi na uzalishaji wa ajira na kwamba unatarajiwa kuweka msukumo wa kipekee na kuleta mageuzi yatakayobadilisha mifumo, mitazamo na mwenendo katika utendaji.

“Hatua hii itachochea tija katika uzalishaji, kuongeza uwezo wa nchi katika kushindana kikanda na kimataifa, na kuchochea muunganiko wa sekta mbalimbali. Lengo ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, viwanda na biashara katika ukanda wa Afrika,” amesema.

Ametoa kauli hiyo bungeni leo (Ijumaa, Februari 6, 2026) katika hotuba ya kuhitimisha mkutano wa pili wa Bunge wakati akielezea Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali katika muda wa Kati wa 2026/2027 – 2028/2029 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2026/2027. Bunge limeahirishwa hadi Machi 31, 2026.

Akielezea mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango huo, Waziri Mkuu amesema Serikali itatekeleza vipaumbele katika miradi inayoendelea, iliyosainiwa pamoja na vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

“Maeneo mahsusi ya kipaumbele katika matumizi ni kugharimia miradi ya kielelezo na kimkakati inayoendelea, deni la taifa, mishahara ya watumishi wa umma na huduma za jamii,” amesema.

Akitoa maelekezo katika maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2026/2027, Waziri Mkuu amewataka Maafisa Masuuli waweke msukumo kwenye maeneo sita yakiwemo ya kusimamia kusimamia nyongeza ya asilimia tano kwenye mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

“Ninaelekeza Ofisi za Wakuu wa Mikoa zisimamie Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia kwa pamoja asilimia tano kati ya asilimia 15 ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa ajili ya uwekezaji kwenye miradi ya kuboresha mazingira ya biashara na ujasiriamali ili kuvutia na kuongeza fursa za ajira kwa makundi haya,” amesema.

Amewataka Maafisa Masuuli wazingatie mkakati wa kulinda wawekezaji wa ndani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika zabuni, masharti ya mikataba na malipo ya hati za madai. Aidha amewataka waandae mikakati ya kuzalisha, kulea na kukuza wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa kupitia dhana ya ushirikishaji wa wananchi katika utekelezaji, uwezeshaji na upatikanaji wa mikopo ya gharama nafuu ili kuwezesha uibuaji wa fursa za ajira kwa vijana.

Pia amezitaka taasisi na mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara yaweke mikakati ya kuondokana na utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu ifikapo Juni, 2029 ili kutoa fursa kwa serikali kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayowahusu wananchi.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa ziongeze uwazi katika utekelezaji wa miradi kwenye halmashauri nchini. “Mapato yote yajulikane kwa Waheshimiwa Wabunge na Madiwani. Kila wakati, Katibu Tawala Mkoa anapotuma fedha kwenye halmashauri atoe nakala kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mbunge, ofisi ya Meya, kwa Wenyeviti wa Halmashauri na Madiwani na aainishe aina ya miradi inayoenda kutekelezwa,” amesisitiza.

Amesisitiza kuwa ratiba za vikao vya Baraza la Madiwani zizingatie ratiba za vikao vya Bunge ili kutoa fursa kwa wabunge kushiriki vikao kwani vikao vya Bunge si vya dharura na ratiba yake inajulikana mapema. “Miradi yote ambayo ipo kwenye hatua za utekelezaji gharama zake zisiwe siri, taarifa zake zijulikane kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Wabunge, Meya, Wenyeviti wa Halmashauri na Madiwani. Lengo la kuweka uwazi ni kuwarahisishia Waheshimiwa Wabunge kufuatilia miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao,” amesema

Ili kufanikisha utekelezaji wa maelekezo hayo, Waziri Mkuu amewaomba wabunge wanaporejea majimboni kwao, wafuatilie kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, waweke mawe ya msingi na kuzindua miradi ambayo imekamilika. Vilevile, hakikisheni mnapata taarifa za utekelezaji wa kila mradi na maeneo ambayo mna ushauri, tumieni fursa zote zikiwemo vikao vya halmashauri, vikao vya baraza la ushauri la wilaya (DCC), vikao vya Baraza la Ushauri la Mkoa (RCC), wizara za kisekta au hata Ofisi ya Waziri Mkuu,” amesema.

Amewataka viongozi na watendaji wote wa serikali waithamini na kuishirikisha sekta binafsi katika hatua mbalimbali za kupanga na kutekeleza miradi yote ya maendeleo kwa kuwa mchango wa sekta binafsi katika utekelezaji Dira ya Taifa ni mkubwa. “Sekta binafsi ipewe heshima ili kuhakikisha mchango wao unaonekana.