-Bilioni 200 zatua kwa Waziri wa Vijana kwa utekelezaji

Na Byarugaba Innocent, OR-MV

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana Mhe.Joel Arthur Nanauka Februari 5, 2026 amepokea hundi yenye thamani ya Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha Wanawake na Vijana kimitaji kutoka kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, 2025

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu Mlimwa Jijini Dodoma pamoja na kurushwa Mubashara kupitia Redio na Runinga ya Taifa ikishuhudiwa na Wahe.Mawaziri na Wahe.

Wabunge wanaowawakilisha Vijana ikiwa ni utekelezaji kwa vitendo wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100 tangu achaguliwe kuliongoza Taifa Oktoba 29,2025

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa uwezeshaji huo unapaswa kuonesha tija kwa wanufaikaji kwa kuwa chombo cha mageuzi kiuchumi huku akitoa rai kwa waratibu kuendesha zoezi kwa uwazi na uwajibikaji.

“taarifa za Maendeleo zitolewe mara kwa mara na hatua zichukuliwe dhidi ya matumizi mabaya ya fedha hizi”..amesema Waziri Mkuu

Aidha,Waziri Mkuu ametoa rai kwa taasisi na mamlaka zote zinazoshiriki katika utekelezaji wa uwezeshaji kiuchumi kubadili mtazamo kutoka kwenye kutoa fedha kwenda kwenye kusimamia matokeo kwa kujiwekea malengo yanayopimika,kuwa na viashiria vya utendaji kazi na ratiba kamili za utekelezaji kwa lengo la kuhakikisha mitaji hiyo inazalisha ajira,kukuza kipato kwa wanufaikaji na kuwa na biashara endelevu.

Daudi Lister Richard (24) mkazi wa Ihumwa Jijini Dodoma anayejishughulisha na kazi ya upambaji amesema kitendo alichokifanya Rais Samia kutoa kiasi hicho cha fedha ni ukombozi kwa Vijana kwani wengi wamekuwa na mawazo ya kibiashara lakini mitaji imekuwa kikwazo kufikia ndoto zao za kujinasua na umasikini wa kipato

Bahati Jonas (27) Mkazi wa Ilazo Jijini Dodoma anayejishughulisha na usafirishaji wa bodaboda amempongeza Rais Samia kwa kutoa kiwango hicho kikubwa kwa Vijana kwani lengo ni kuwainua kiuchumi na kuwaondoa kwenye minyororo ya kutumikishwa na matajiri.


“…nimekuwa nikiendesha pikipiki ya tajiri kwa mkataba wa Shilingi Milioni 4,500,000.00 wakati Pikipiki ilinunuliwa kwa milioni 2,700,000.00 Huku ni kuumizana. Jambo alilolifanya Mhe.Rais ni kubwa kwani litawezesha Vijana wengi kujiari na kuinuka kiuchumi” ameongeza Bahati.

Mariam Mabula (35) mkazi wa Mkoa wa Shinyanga mjasiliamali anayejishulisha na Kazi za Mama lishe amesema fedha hiyo itamwezesha kuboresha biashara yake ili aweze kulisha tenda kubwa zikiwemo harusi na mikutano mbalimbali ya kidini na kiserikali.