Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Chama cha Wasambazaji wa Bidhaa na Watoa Huduma Migodini (TAMISA) kimezitaka kampuni za kigeni zinazowekeza katika sekta ya madini nchini kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwa Watanzania katika ajira, utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa, kwa mujibu wa sheria ya maudhui ya ndani (Local Content).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TAMISA, Bw. Peter Kumalilwa, alisema kuwa lengo la uwekezaji katika sekta ya madini ni kuhakikisha Watanzania wananufaika moja kwa moja na rasilimali zao kupitia ajira, zabuni na fursa za kiuchumi zinazotokana na shughuli za migodini..

Alisema kuwa bado kuna changamoto katika utekelezaji wa sera ya maudhui ya ndani, huku akibainisha kuwa TAMISA inaendelea kupokea taarifa kuhusu baadhi ya migodi inayokiuka miongozo hiyo kwa kutoa zabuni kwa kampuni zisizo na umiliki wa wazawa, pamoja na kuweka masharti magumu yasiyo rafiki katika mifumo ya manunuzi.

“Vitendo hivi vinawakatisha tamaa wazawa wanaotoa huduma na kusambaza bidhaa migodini, na kuwavunja moyo kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa kama sheria inavyoelekeza,” alisema Bw. Kumalilwa.

Aliongeza kuwa TAMISA inakemea vikali vitendo hivyo na imejipanga kusimamia utekelezaji wa sheria na taratibu bila woga wala upendeleo wa aina yoyote.

“TAMISA itachukua hatua madhubuti, ikiwemo kutoa taarifa kwa mamlaka husika dhidi ya yeyote au kampuni yoyote itakayokiuka maelekezo ya Serikali na masharti ya kisheria,” alisisitiza.


Bw. Kumalilwa aliwakumbusha wadau wote kuwa ushirikishwaji wa wazawa katika sekta ya madini si suala la kisiasa bali ni sera ya kitaifa inayosimamiwa na Serikali.

Alirejea hotuba ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ya tarehe 14 Januari 2026, ambapo alisisitiza kuwa huduma zote zinazoweza kutolewa na wazawa zinapaswa kutolewa na wazawa, msimamo ambao TAMISA imesema inauunga mkono kikamilifu.

Aliongeza kuwa msimamo wa Serikali ni kuijenga Tanzania yenye msingi wa ushiriki wa wananchi wake katika rasilimali za taifa ili wanufaike kiuchumi.

“TAMISA tunaiunga mkono Serikali kwa dhati na tumejipanga kushirikiana na Tume ya Madini, Wizara ya Madini na wadau wote kuhakikisha sera ya maudhui ya ndani inatekelezwa kwa vitendo, huku tukipambana na vitendo vya upendeleo vinavyokwamisha maendeleo ya sekta na taifa kwa ujumla,” alisema.


Katika hatua hiyo hiyo, Bw. Kumalilwa alimpongeza Waziri wa Madini, Bw. Anthony Mavunde, kwa uongozi wake mzuri na miongozo anayoendelea kutoa kwa wadau wa sekta hiyo, ikiwemo kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu katika ujenzi na ukuaji wa sekta ya madini nchini.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TAMISA, Bw. Japhet Mussa, alisema kuwa taasisi hiyo itaendelea kuwa sauti ya wazawa katika sekta ya madini, ambayo ni miongoni mwa sekta zinazoongoza kwa kuchangia pato la taifa.

“Kupitia umoja wetu, tutaongeza nguvu ya pamoja katika kujenga uchumi wa kitaifa unaotegemea rasilimali zetu wenyewe,” alisema Bw. Mussa.

Aidha, alitoa wito kwa Watanzania wote wanaojihusisha na sekta ya madini kujiunga na TAMISA ili kushirikiana katika kuimarisha na kuendeleza sekta hiyo.

“TAMISA tumekuwa tukifanya kazi bega kwa bega na Serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kukua na kutoa fursa zaidi kwa Watanzania, jambo linalochangia kukuza uchumi wa taifa,” alisema.

Alitoa wito kwa watoa huduma na wasambazaji wa bidhaa migodini kujiunga na taasisi hiyo, akisisitiza kuwa chama hicho ni jukwaa la umoja, nguvu na sauti ya pamoja kwa wazawa.

“Kwa pamoja, tutaendelea kutetea maslahi ya wazawa na kuendeleza falsafa ya ‘Madini ni Maisha na Utajiri’, kwa manufaa ya Watanzania na taifa kwa ujumla,” alisema.

Mwisho