Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wanne kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 45 na gramu 785 katika nyakati tofauti.

Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Wilfred Komba (24), mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Iringa, Lenad Shamba maarufu Paulo (21) mkazi wa Tarime mkoani Mara, James Mwakalebela (26) mkazi wa Ngonga – Kyela na Joseph Mkwara maarufu Aliki (26) mkazi wa Kyela.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa wanasafirisha dawa hizo zikiwa zimehifadhiwa katika mabegi matatu na mifuko miwili ya sandarusi wakitumia mabasi ya abiria kutoka Mbeya kuelekea Dar es Salaam. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa dawa hizo ziliingizwa nchini kutoka nchi jirani.