Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wakati magonjwa yasioambukiza yakiendelea kushika kasi, takwimu zinaonyesha kuwa kuna watu  milioni 450 duniani wanaugua matatizo ya akili kila mwaka

Takwimu hizo zinaeleza kuwa kati ya watu hao, takribani milioni moja hujiua kila mwaka katika nchi mbalimbali, zikiwemo baadhi ya nchi za Afrika kama Botswana.

Hayo yalibainishwa na Profesa Mstaafu wa Afya ya Akili na mshauri wa Akili Platform Tanzania, Profesa Gadi Kilonzo, wakati wa kongamano la vijana kuhusu afya ya akili lililoandaliwa na Akili plrt form Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kairuki, Dar es Salaam (KUSA Mental Health Conference ) .

Profesa Kilonzo amesema  kwa sasa duniani kuna watu takribani milioni 150 wanaoishi na tatizo la sonona (depression), huku zaidi ya milioni moja wakijiua kila mwaka.

Aidha, alieleza kuwa watu milioni 25 wana tatizo la skizofrenia, milioni 28 wanaugua kifafa na takribani milioni 90 anakabiliwa na matatizo ya ulevi wa pombe.

Kwa upande wa Tanzania, Profesa Kilonzo amesema tafiti mbalimbali zilizofanywa na watafiti akiwemo Bondestam, Ngoma na Jenkins zinaonyesha kuwa matatizo ya afya ya akili yapo kati ya asilimia 0.32 hadi 31 ya wananchi, hali inayoashiria ukubwa wa changamoto iliyopo.

Aliongeza kuwa katika kliniki za magonjwa ya kawaida, mahudhurio ya awali yanaonyesha kuwa asilimia 49 ya wagonjwa wana matatizo yanayotokana na msongo wa mawazo, jambo linaloashiria kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanyika katika kudhib

Profesa Kilonzo amedai  kuwa katika kliniki za magonjwa ya kawaida, mahudhurio ya awali yanaonyesha kuwa asilimia 49 ya wagonjwa wana matatizo yanayotokana na msongo wa mawazo, jambo linaloashiria kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanyika katika kudhibiti na kupunguza tatizo hilo.

Ameonya wazazi na walimu kutotumia viboko kwa wanafunzi kwani wao huwapiga watoto kwa nia ya kuwalea, lakini adhabu hizo za mwili huacha athari kubwa kisaikolojia ikiwemo kujenga hofu, hasira, chuki na tabia ya kutesana, hali hiyo inayochangia matatizo ya afya ya akili baadaye.

Amesema kuwa kuimarisha mahusiano chanya katika familia, jamii na taasisi za dini kupitia kuaminiana, kuthaminiana na kushirikiana kunasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha afya ya akili.

“Takribani asilimia 25 ya familia zina angalau mtu mmoja mwenye tatizo la afya ya akili. Mtu huyo mmoja anaweza kuathiri maendeleo ya kiuchumi ya familia nzima pamoja na majirani na wafanyakazi wenzake,” amesema Profesa Kilonzo.

Alisisitiza kuwa utulivu wa mawazo na hisia katika jamii ni msingi muhimu wa afya ya akili, kwani huongeza tija kazini, masomoni, katika burudani, uhusiano mzuri na jamii pamoja na kujithamini.

Alifafanua kuwa afya ya akili ni hali ya ustawi inayomuwezesha mtu kufikia malengo yake, kukabiliana na changamoto za maisha, kufanya kazi kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya jamii.

Akizungumzia sonona, Profesa Kilonzo amesema ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya matatizo ya afya ya akili, ambapo huleta hali ya kukata tamaa, kuona maisha hayana maana, kutamani kifo na wakati mwingine kujaribu kujiua.

Profesa kilonzo amesema  msongo wa mawazo wa muda mrefu, husababisha pia kushuka kwa kinga ya mwili na hivyo kusababisha afya kuteteleka.

“Katika nchi zinazoendelea, mgonjwa wa afya ya akili huwaathiri wanafamilia, ndugu na majirani kwa kusababisha msongo wa mawazo, migogoro, kubaguana, kulaumiana kwa misingi ya ushirikina na hata kunyanyapaanana. Tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 33 ya ukosefu wa kipato unatokana na maradhi ya akili,” amesema.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Maadili wa Chuo Kikuu cha Kairuki, Abraham Mwalugeni, amesema bado kuna changamoto katika baadhi ya vyuo vikuu ambapo baadhi ya wavulana huwasumbua wasichana, hata pale wanapokataa kushiriki vitendo wasivyovipenda.

Amesema ni muhimu kwa wanafunzi, hususan wa kike, kutumia huduma za mentors, wanasaikolojia na kuripoti mapema ili kuepuka kunyanyaswa na hatimaye kupata matatizo ya afya ya akili.

“Mwanafunzi usikae kimya,hapa chuoni tuna wataalamu wa saikolojia na hospitali, wewe sema shida yako mapema kwani kila mtu ana haki ya kusema ndiyo au hapana kwani ukikaa kimya, madhara yake yanaweza kuwa makubwa,” amesema

Aliongeza kuwa afya ya akili ni sehemu muhimu ya maisha ya mwanafunzi, lakini bado kuna changamoto nyingi hasa kwa wanafunzi wa kike, hivyo ni vyema kutafuta msaada kutoka kwa mentors, wataalamu wa saikolojia na madawati ya jinsia.

Mwalugeni alisisitiza kuwa mwanafunzi anapaswa kuzingatia afya yake kwa kupanga muda vizuri, kuepuka msongo wa mawazo usio wa lazima, kupata usingizi wa kutosha na kujikita zaidi katika masomo.

Mkurugenzi wa Akili Platform Tanzania, Roghat Robert, amesema kwa sasa vijana ndio wanaoongoza kuathiriwa na changamoto zinazoathiri afya ya akili, zikiwemo hali ngumu ya uchumi, matumizi ya dawa za kulevya na kuporomoka kwa maadili katika jamii.

“Tunalenga kupaza sauti za vijana na kuwahamasisha kuvunja ukimya kwani  hauponyi afya ya akili

Ndiyo maana kwa sasa ,tumeanzisha programu za kutembelea vyuo vikuu  ili kuwahamasisha vijana kubadilika kabla ya kurejea kwenye jamii kwani tunawategemea wawe bora,” amesema

Robert aliongeza kuwa ushirikiano na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Milembe na Hospitali ya Taifa Muhimbili ni muhimu kwani kuna wataalamu wanaoweza kusaidia vijana wanaokumbwa na changamoto za afya ya akili.

Rais wa Tanzania Mental Health Journalists Organisation, Veronica Mrema, aliwataka wanafunzi na jamii wakipata changamoto waangalie  platform sahihi za maswala ya Afya ya Akili  ili kupa msaada  badala ya kukaa kimya .

“Ni muhimu kuwafuata wataalamu na kutembelea tovuti sahihi zinazotoa elimu na huduma za afya ya akili,kwani kukaa kimya ndiko kunasababisha madhara makubwa zaidi,” amesema.

Amesema waandishi wa habari wana nafasi kubwa, katika kukuza uelewa wa afya ya akili kwa jamii kwa kutoa taarifa sahihi na kuhamasisha watu kutafuta msaada mapema.

Kongamano hilo la siku moja liliwakutanisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kairuki pamoja na wadau mbalimbali wa afya ya akili, wakiwemo Akili Platform Tanzania na Tanzania Mental Health Journalists Organisation, kwa lengo la kujadili na kutafuta suluhisho la changamoto za afya ya akili kwa vijana.