Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Karatu

Wazazi na walezi wametakiwa kufahamu na kuzingatia Kanuni za Vituo vya Kulea Watoto Mchana na Watoto Wachanga za mwaka 2012 ili kuhakikisha watoto wanapata malezi sahihi kulingana na umri wao.

Akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari, Mratibu wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMAAM) ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Arusha, Denis Mgiye amesema lengo kuu la vituo vya kulea watoto ni kutoa malezi na makuzi kupitia michezo na burudani siyo elimu rasmi kama inayotolewa shuleni.

Amesisitiza kuwa kituo cha kulea watoto si shule bali ni mazingira ya kumlea na kumkuza mtoto kwa kutumia michezo na shughuli zinazomjenga kiakili, kihisia na kijamii.

“Kituo cha kulea watoto siyo shule, kwa bahati mbaya baadhi ya wazazi na walezi hawajui kuwa mtoto wa chini ya miaka mitano hapaswi kufundishwa masomo rasmi bali hujengwa kupitia michezo,” alisema Mgiye.

Ameongeza kuwa baadhi ya vituo vimekuwa vikikiuka kanuni kwa kuwafundisha watoto masomo rasmi, kuwapa majaribio ya nyumbani (homework) na hata mitihani jambo ambalo halipo katika mwongozo wa kitaifa.

“Unakuta mtoto anapewa homework na mitihani, na wazazi wanafurahia kuona mtoto anajua kuhesabu, kusoma au kuandika katika umri huo mdogo bila kujua athari zake,” alieleza.

Kwa mujibu wa tafiti za kisaikolojia kuhusu ukuaji wa mtoto, Mgiye amesema watoto walio chini ya miaka mitano wapo katika hatua ya ukuaji inayojikita zaidi kwenye michezo, hisia na uzoefu wa moja kwa moja, siyo kujifunza darasani kwa mfumo wa kitaaluma.

Ametaja baadhi ya athari za kuwafundisha watoto masomo rasmi mapema kuwa ni pamoja na msongo wa mawazo kutokana na hofu ya kukosea, kupungua kwa ubunifu, kujenga mtazamo hasi kuhusu shule pamoja na uchovu wa akili unaoweza kusababisha kupungua kwa umakini.

Mgiye amesema Mkoa wa Arusha una jumla ya vituo 256 vya kulea watoto na katika kuhakikisha vinazingatia kanuni, takribani vituo kumi vimefungiwa baada ya kubainika kuwa havikidhi vigezo vya kutoa malezi stahiki.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Malezi Mbadala kutoka shirika la SOS Children’s Villages, Husna Selungwi, amesema matarajio ya baadhi ya wazazi yanakinzana na muongozo wa kitaifa unaosimamia vituo vya kulea watoto, hali inayochangia baadhi ya vituo kuanza kutoa huduma zisizoendana na kanuni.

Naye mwandishi wa habari na kinara wa masuala ya malezi na makuzi ya mtoto, Beatrice Gerald, amewataka waandishi wa habari kuandika habari zenye kulinda utu wa mtoto na kusaidia jamii kupata elimu sahihi kuhusu maendeleo ya awali ya mtoto badala ya kuchapisha maudhui yanayoweza kudhalilisha watoto.

Amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kushirikiana na wataalamu wa ustawi wa jamii katika kuelimisha umma kuhusu malezi bora na makuzi sahihi ya watoto wadogo.