Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini leo tarehe 12 Februari 2026 kuelekea Addis Ababa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika tarehe 14 hadi 15 Februari 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari S. Machumu, kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu, tarehe 13 Februari 2026 Rais Samia atashiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC) chini ya uenyeji wa Rais wa Kenya, Mheshimiwa William Samoei Ruto, na baadaye kuhudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mheshimiwa Abiy Ahmed Ali.

“Rais Samia pia anatarajiwa kufanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na maendeleo,” alisema Machumu.

Aliongeza kuwa mazungumzo hayo yatamkutanisha Rais Samia na viongozi akiwemo Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini, Mheshimiwa Russell Mmiso Dlamini; Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Mheshimiwa Azali Assoumani; Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi. Amina Mohammed; pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Sidi Ould Tah.

Machumu alieleza kuwa Mkutano huo utafunguliwa rasmi tarehe 14 Februari 2026 ukiongozwa na Kaulimbiu ya mwaka 2026 isemayo: “Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji na Huduma Salama za Usafi wa Mazingira ili Kufikia Malengo ya Ajenda 2063,” inayolenga kuhimiza hatua za pamoja barani Afrika katika usalama wa rasilimali maji, afya ya jamii na maendeleo endelevu.

Aidha, alisema Tanzania inakamilisha muda wake wa kulitumikia Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika baada ya vipindi viwili mfululizo kuanzia mwaka 2022 hadi 2026, ambapo imetoa mchango mkubwa katika kuimarisha amani, utulivu na usalama barani Afrika.

Katika hatua nyingine, mkutano huo unatarajiwa kutangaza rasmi uongozi wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2026, ambapo Jamhuri ya Burundi inatarajiwa kuchukua nafasi ya Uenyekiti wa Umoja huo, huku Tanzania ikiteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Mwenyekiti ikiwakilisha Kanda ya Mashariki.

Vilevile, Rais Samia amependekezwa kuteuliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto, uteuzi unaotarajiwa kupitishwa rasmi na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.

Machumu alisisitiza kuwa ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unaendelea kuimarisha nafasi ya nchi katika diplomasia ya kikanda na kimataifa, pamoja na kutetea maslahi ya taifa na kuchangia ujenzi wa Afrika yenye amani, mshikamano na maendeleo endelevu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiagana na viongozi mbalimbali katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Februari, 2026 kabla ya kuondoka nchini kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiondoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam, tarehe 12 Februari, 2026, kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).