Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema takriban nyumba 280 zimeezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa iliyonyesha mwanzoni mwa mwezi huu wilayani Rufiji mkoani humo.

Kunenge aliyasema hayo alipokuwa akizungumza wilayani humo, akieleza kuwa licha ya athari hizo za mvua na upepo, hakuna kifo kilichotokea.

“Tumepata changamoto ya upepo, Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na wadau mbalimbali kwa kuwakimbilia wananchi na kutoa huduma muhimu, bado tunaendelea kupokea misaada ili wananchi hao warejee katika hali ya kawaida,” alieleza Kunenge.

Baadhi ya kata zilizoathirika ni Utete na Chemchem, ambapo makazi na miundombinu ya taasisi imeharibika, ikiwemo vyumba vya madarasa na ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Mapinduzi, miundombinu ya umeme lakini TANESCO wilaya imefanya jitihada za kurejesha huduma hiyo.

Hata hivyo, masomo hayajasitishwa, kwani wanafunzi wanaendelea na masomo wakitumia vyumba vingine ambavyo havikuathirika.

Kuhusu masuala ya uwekezaji katika sekta ya kilimo na umwagiliaji Kunenge alieleza, serikali inaendelea kukamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi wa mabwawa makubwa mawili ya umwagiliaji, ikiwemo bwawa la Kibiti, ambayo yatasaidia kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kupunguza athari za mafuriko wakati wa mvua kubwa.

Vilevile, alieleza mbali ya changamoto ya mvua, mkoa unaendelea kufanya vizuri katika sekta ya kilimo na unatarajia kuwa na uwekezaji mkubwa ndani ya Afrika, kufuatia kampuni inayotarajia kuanza uzalishaji mkubwa wa ndizi Rufiji kwa ajili ya usafirishaji nje ya nchi, ikiwa na mpango wa kusafirisha kontena 50 za ndizi kila siku.

Kwa mujibu wa mkuu huyo mkoa upo salama na unaendelea kuinua sekta ya viwanda na uwekezaji.