Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imeanza kuchukua hatua za makusudi kupunguza mzigo wa tozo na ada katika sekta ya vyombo vya habari, kufuatia kilio cha wadau kuhusu mdororo mkubwa wa kiuchumi unaoendelea kuzikumba taasisi za utangazaji tangu janga la ugonjwa wa Corona (COVID-19).
Hatua hiyo inalenga kuokoa sekta ya habari dhidi ya anguko la kiuchumi, kuboresha mazingira ya uendeshaji na kuhakikisha huduma za utangazaji zinaendelea kuwafikia wananchi, hususan waliopo vijijini.

Akizungumza leo Februari 12, 2026 jiijini Dodoma kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa vyombo vvya utangazaji Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema Serikali inalenga kuifanya Tanzania kuwa mshiriki mkubwa katika soko la kimataifa la uzalishaji wa maudhui kwa kuweka mazingira rafiki kwa wadau wa habari.
Amesema katika utekelezaji wa mkakati huo, Serikali imeanza kupunguza ada ya leseni ya utangazaji kutoka Sh500,000 hadi Sh50,000, pamoja na ada ya maombi kupunguzwa hadi Sh10,000, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa kifedha kwa watoa huduma.
Amesisitiza kuwa mapitio ya tozo nyingine yanaendelea ili kuiondoa sekta ya habari katika mdororo wa kiuchumi na kuhakikisha huduma za utangazaji zinawafikia wananchi wote kwa usawa.
“Badala ya kudhibiti kupita kiasi, Serikali inalenga kuwawezesha watoa huduma ili kukuza sekta ya habari na utangazaji,” amesema Mwinjuma.
Awali, Mwenyekiti wa Vyombo vya Habari Tanzania (NIBA), Amos Ngosha, amesema sekta ya vyombo vya habari inaendelea kukumbwa na mdororo mkubwa wa kiuchumi ulioanza tangu kipindi cha Corona na kuziacha taasisi nyingi katika mazingira magumu ya uendeshaji.

Ameeleza kuwa mdororo huo umeathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya vyombo vya habari kutokana na kushuka kwa matangazo ya biashara, udhamini wa vipindi na mzunguko wa fedha kwa ujumla, hali inayowafanya waajiri wengi kushindwa kukidhi mahitaji ya watumishi wao.
“Vyombo vingi vinashindwa kulipa mishahara kwa wakati, kutoa posho na kutekeleza majukumu mengine ya kiutumishi,hili ni ombwe la kiuchumi ambalo bado halijazibwa,” amesema Ngosha.
Ameongeza kuwa changamoto hiyo imeongezwa uzito na uwepo wa tozo na ada nyingi, zipatazo 19, zikiwemo ada za leseni za utangazaji, ada za maudhui, ada za marudio ya leseni, ada za matumizi ya masafa na ada nyingine za kisheria.
Kwa mujibu wa Ngosha, mzigo huo wa kifedha umepelekea baadhi ya vyombo kushindwa kuhuisha leseni na kulipa ada stahiki, hali iliyopelekea kufungiwa.
Kutokana na hali hiyo, ameomba Serikali kuacha kufungia vyombo vinavyoshindwa kulipa tozo na badala yake kuviruhusu kuendelea kufanya kazi ili vijitafutie kipato cha kulipa madeni yao, akisisitiza kuwa sekta ya habari inahitaji kuokolewa kwa mtazamo wa kizalendo.

Mjadala huo umefanyika katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji, ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ukiwa na kaulimbiu isemayo “Matumizi ya Teknolojia katika Kupanua na Kuboresha Huduma za Utangazaji Vijijini.”
Mkutano huo umejikita katika kutathmini nafasi ya teknolojia za kisasa katika kuboresha upatikanaji, ubora na usawa wa huduma za utangazaji, hususan kwa jamii zinazoishi vijijini ambako bado kuna changamoto za miundombinu, gharama na upatikanaji wa taarifa sahihi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume ya Maudhui kutoka TCRA, Isack Mruma, amesema mamlaka imebaini ukiukwaji katika maeneo tisa ya utoaji wa maudhui, ikiwemo baadhi ya vituo kutumia muda mwingi kurusha michezo, hususan mpira wa miguu, badala ya maudhui ya kielimu na kijamii.
Amesema TCRA imeandaa mwongozo mpya unaolenga kuboresha ubora wa maudhui, ikiwemo kuwataka waandishi kuwa na leseni na kuthibitishwa na Bodi ya Ithibati ili kuhakikisha maudhui yanayotolewa yanazingatia viwango vinavyotakiwa.

