Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
SIKU 100 baada ya kuingia madarakani katika awamu ya pili ya uongozi wake, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameleta neema kwa wakazi wa Mji wa Igunga Mkoani hapa kwa kuwawezesha kupata huduma ya maji kwa masaa 24 kila siku.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Igunga (IGUWASA) Alex Ntonge ameeleza kuwa kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Rais imemaliza changamoto za huduma ya maji.
Amebainisha kuwa maboresho makubwa ya miundombinu na kupanuliwa kwa mradi wa maji ya Ziwa Victoria kumewezesha wakazi wote wa Mji huo na maeneo jirani kupata huduma ya maji safi na salama wakati wote, kwa masaa 24 kila siku.
‘Kazi nzuri iliyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika siku 100 za kwanza tangu aingie Ofisini, imeleta neema, mabilioni aliyotuletea yameendelea kuboresha huduma ya maji na usafi wa mazingira Mji wote’, amesema.

Mkurugenzi amefafanua kuwa zaidi ya asilimia 98 ya wakazi wote wa Mji huo ikiwemo Kata za Mbutu, Mwamashimba, Isakamaliwa na Mwalala, wamenufaika na maboresho makubwa ya huduma hiyo yaliyofanywa na IGUWASA.
Amedokeza kuwa mahitaji ya maji katika Mji huo ni mita za ujazo 6,700 kwa siku lakini kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa, sasa Mamlaka inazalisha mita za ujazo 8,500 kwa siku, hivyo kuwa na maji ya ziada.
Aidha jitihada za kusogeza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi na katika maeneo yote ambayo hayajafikiwa na mtandao huo zimeendelea kufanywa na IGUWASA kupitia fedha za ndani na miradi mingine inayofadhiliwa na Serikali.
Kwa upande wa usafi wa mazingira, Mkurugenzi amepongeza serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwawezesha magari 2 maalumu kwa ajili ya uondoshaji majitaka katika makazi ya wananchi kwa njia iliyo bora, salama na endelevu, kazi inaendelea.

Amedokeza kuwa serikali iliwapatia kiasi cha shilingi bilioni 1.86 kwa ajili ya kufanikisha mradi wa uboreshaji huduma ya usafi wa mazingira na kutibu maji taka na shilingi bilioni 3.47 za mradi wa uboreshaji mfumo wa uzalishaji maji.
Ntonge amefafanua kuwa mradi wa ukarabati wa mfumo wa uzalishaji maji ulilenga kuboreshwa Bwawa la Bulenya na mfumo wa kutibu maji wa Igogo na ujenzi wa mtandao wa uhakika wa kusafirisha maji hayo.


