Na Mwandishi wa OMH
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imehitimisha semina ya siku tano kwa Kamati za Kudumu za Bunge za Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na ile ya Hesabu za Serikali (PAC), iliyofanyika kuanzia Februari 9 hadi 13, 2026, ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa kujenga uwezo wa Waheshimiwa Wabunge katika eneo la usimamizi na tathmini ya uwekezaji wa Serikali.
Kwa kipindi chote cha semina, OMH imewasilisha mada za kimkakati zilizolenga kuimarisha uelewa wa Kamati kuhusu nafasi ya Ofisi katika kuhifadhi, kusimamia na kuongeza thamani ya mitaji ya umma.
Mafunzo haya yalijikita katika kuoanisha wajibu wa kikatiba wa Kamati za PIC, PAC na jukumu la kisheria la OMH chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura 370, ili kuhakikisha kuna uelewa wa pamoja kuhusu mifumo ya usimamizi, tathmini na uwajibikaji.
Katika mada ya ufanisi wa mitaji ya umma kupitia uanzishaji, uendelezaji na usimamizi wa kampuni tanzu, OMH ilieleza misingi ya kisheria na kiutendaji inayotumika kuanzisha kampuni hizo, kuanzia upembuzi yakinifu, idhini za mamlaka husika, hadi mifumo ya uendeshaji na tathmini.
Ilisisitizwa kuwa kampuni tanzu zimekuwa nyenzo ya kimkakati katika kukuza sekta za nishati, maji, kilimo na uchukuzi, kuongeza mapato yasiyo ya kodi na kupunguza utegemezi wa bajeti kuu ya Serikali.
Kwa upande wa mada kuhusu uainishaji na usimamizi wa mashirika ya umma kwa mujibu wa umiliki wa hisa, OMH iliwasilisha takwimu zinazoonesha kuwa inasimamia taasisi, mashirika na kampuni 308, zikiwemo 252 zinazomilikiwa na Serikali na 56 ambazo Serikali ina hisa chache.
Kamati zilielezwa mifumo tofauti ya usimamizi kwa mashirika ya umiliki mkubwa na yale ya ubia, pamoja na namna tathmini ya utendaji inavyofanyika kwa kuzingatia matokeo ya kifedha, ubora wa huduma, utawala bora na mchango wa kiuchumi.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, uwekezaji wa Serikali umeongezeka kutoka Sh67 trilioni hadi Sh92.3 trilioni, huku mapato yasiyo ya kodi yakiongezeka kutoka Sh637 bilioni hadi Sh1.028 trilioni.
Takwimu hizi ziliwasilishwa kama kiashiria cha kuimarika kwa usimamizi wa mitaji ya umma na mageuzi yanayoendelea ndani ya mashirika.
Aidha, semina ilijumuisha mada mahsusi kuhusu matumizi ya Mpango Mkakati, Mpango wa Uwekezaji na Mpango wa Biashara katika kutathmini ufanisi wa uwekezaji.
OMH ilieleza kuwa nyaraka hizi tatu ndizo msingi wa upangaji, utekelezaji na tathmini ya shughuli za taasisi na mashirika ya umma.
Mpango Mkakati wa miaka mitano huweka dira, dhamira, malengo ya kimkakati na viashiria vya kupima mafanikio.
Mpango wa Uwekezaji hubainisha miradi ya kipaumbele, tathmini za uwezekano na vyanzo vya fedha, wakati Mpango wa Biashara hutafsiri malengo ya kimkakati kuwa shughuli za kila mwaka na bajeti za utekelezaji.
Ilifafanuliwa kuwa mipango hii hufanya kazi kama mfumo mmoja uliounganishwa. Mpango Mkakati hutoa mwelekeo wa muda mrefu, Mpango wa Uwekezaji huainisha miradi itakayotekeleza mwelekeo huo, na Mpango wa Biashara huongoza utekelezaji wa kila siku.
Kupitia mfumo huu, OMH hutathmini kama rasilimali za umma zinawekezwa kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha.
Kwa mfano, katika mashirika ya miundombinu, utekelezaji wa miradi hupimwa kwa kuoanisha ratiba, bajeti na matokeo yaliyotarajiwa.
Katika mashirika ya kifedha ambako Serikali ina hisa, tathmini huzingatia gawio, thamani ya hisa na mchango katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Aidha, OMH hutumia viashiria vya utendaji (KPIs) vilivyomo kwenye Mipango Mkakati kupima ROI, uendelevu wa kifedha na mchango wa kiuchumi.
Semina pia ilijadili maeneo yanayohitaji maboresho, ikiwemo kutooanishwa kwa baadhi ya mipango, udhaifu wa viashiria visivyopimika na ucheleweshaji wa taarifa za utendaji.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, OMH imeanza kuimarisha mikataba ya utendaji kwa kutumia washauri elekezi kuanzia mwaka wa fedha 2025/26, kuanzisha mfumo wa kidijitali wa ufuatiliaji wa mipango kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango, pamoja na kuendeleza maboresho ya mwongozo wa usimamizi wa uwekezaji wa umma (Public Investment Management – PIM).
Kwa ujumla, semina ya siku tano imeonesha ushirikiano wa karibu kati ya OMH na Kamati ya PIC katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa usimamizi wa mitaji ya umma.
OMH imeweka wazi kuwa itaendelea kutoa taarifa, mafunzo na ushauri wa kitaalamu kwa Bunge ili kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaleta thamani endelevu kwa uchumi wa Taifa na kwa wananchi.








