Bunge la Tanzania limeitaka Serikali kulinda na kuendeleza Mradi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) unaotekelezwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile Februari 14, 2026 , wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu katika mradi wa SGR. Ziara hiyo ililenga kuwapatia Wabunge uelewa wa kina kuhusu majukumu ya TRC pamoja na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya reli.
Kwa niaba ya Serikali na Waziri wa Uchukuzi, Naibu Waziri alipokea na kupongeza mapendekezo ya Kamati hiyo, yaliyoiomba Serikali kuhakikisha utoaji wa huduma zenye ubora wa juu na kuzingatia viwango vya ubora katika ununuzi wa vichwa vya treni (locomotives) na mabehewa (wagons). Aidha, Kamati iliielekeza TRC kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine ili kupanua huduma za usafirishaji wa mizigo kwa Watanzania na nchi jirani.
Awali, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Abubakari Assenga, ilieleza kuunga mkono mikakati ya uwekezaji na malengo ya utendaji ya TRC, ikiwemo azma ya kununua vichwa vya treni 30 ifikapo Machi 2026 kati ya mahitaji ya jumla ya vichwa 58.
Kamati hiyo pia ililipongeza Shirika hilo kwa kuanzisha ajira 894 na kupandisha vyeo wafanyakazi 3,153, ambapo 1,055 walipandishwa kwa mfumo wa madaraja ya kupishana na 2,098 kupitia upandishaji wa kawaida.
Wakati huohuo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Tito Mateshi, alieleza mafanikio ya Shirika licha ya changamoto za kiuendeshaji. Alisema tangu Desemba 2025, TRC imeanza kujiendesha kwa kujitegemea na imepunguza mzigo wa matumizi ya kawaida ya Serikali kwa wastani wa shilingi bilioni 12.9 kwa mwaka. Mafanikio hayo yanawezesha fedha za umma kuelekezwa kwenye miradi mingine ya maendeleo huku yakiiimarisha TRC kuelekea uendelevu wa kibiashara.






